Friday, October 19, 2012

Maandamano ya waislamu Dar,hali tete katikati ya jiji


Waziri ashangaa abiria kulala kwenye sakafu ya kokoto

Naibu Waziri wa Uchukuzi Dk Charles Tizeba akitoa ufafanuzi wa jambo linaloihusu Wizara yake katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera
Dk Tizeba akisalimiana na baadhi ya Maofisa waliofika kumpokea katika uwanja wa ndege Bukoba
Baadhi ya wageni walioambatana na Waziri Tizeba wakiwa katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera
Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Uchukuzi White Majula akitoa ufafanuzi wa malipo ya fidia kwa wananchi wa Bukoba shilingi bilioni 1.9 ili kupisha ujenzi wa jengo la abiria katika uwanja wa ndege wa Bukoba
Phinias Bashaya,Bukoba
NAIBU Waziri wa Uchukuzi Dokta Charles Tizeba ameshangazwa na hali inayowakabili  abiria wa mikoa ya Tabora na Kigoma ambao hulazimika kulala kwenye sakafu ya kokoto wakati wakisubiri usafiri wa treni.

Alionyesha kukerwa na hali hiyo alipokuwa katika ziara yake mjini Bukoba mapema wiki hii wakati akizungumzia uchakavu wa miundombinu ya reli na kulaumu  wahusika kupuuzia suala la ujenzi wa maeneo ya kupumzikia abiria.

“Nilishanga abiria wa Tabora na Kigoma kulala kwenye sakafu ya kokoto wanaposubiri usafiri wa treni,huwezi kuamini kuwa hawa ndio abiria wa Kitanzania wa mwaka 2012”alilalama Tizeba

Alihoji iweje Shirika la  Reli(TRA)lishindwe kuboresha maeneo ya kupumzikia abiria na kuwa kwa kushindwa kufanya hivyo baadhi ya abiria hukwepa kutumia huduma za usafiri zinazotolewa na shirika hilo.

Pia Waziri Dokta Charles Tizeba alisema kuwa wananchi wanalazimika kutumia usafiri wa mabasi kwa sababu  meli na treni havitoe huduma zinazoridhisha, huku akiubeza usafiri wa mabasi na kuufananisha na majeneza yanayotembea.

Aidha alikagua maeneo mbalimbali yaliyopo chini ya Wizara yake ikiwa ni pamoja na uwanja wa ndege wa Bukoba,eneo la Omukajunguti unapotarajiwa kujengwa uwanja wa ndege wa Kimataifa Wilayani Missenye na bandari za Kemondo na Bukoba.

Akizungumzia hali mbaya ya vyombo vya usafiri majini alisema abiria wanakerwa na hali ya uchafu wa meli zinazosafiri ndani ya Ziwa Victoria  na kuwa abiria wanakimbilia usafiri mwingine kukwepa hali inayowafanya waonekane kama walioko mahabusu.

Kuhusu Meli ya Mv Lihemba inayofanya kazi Ziwa Tanganyika alisema itafanyiwa ukarabati mkubwa na Ujerumani.Meli ya Mv Lihemba inatajwa kuwa kongwe zaidi duniani  ikiwa na umri wa miaka mia moja ambayo tangu mwaka 1913 inaendelea kufanya kazi za kusafirisha abiria na mizigo.

Tuesday, October 16, 2012

Uchaguzi wa CCM wazua balaa Mwanza,wajumbe wapata ajali mbaya

Basi  lililopata ajali
UCHAGUZI wa Chama cha Mapinduzi (CCM), nafasi ya Uenyekiti mkoa wa Mwanza umeingia dosari baada ya basi walilokuwa wamepanda wajumbe kutoka Wilayani ya Kwimba mkoani hapa, kupata ajali mbaya ambapo wajumbe saba wamejeruhiwa vibaya, na dereva wa basi hilo amefariki dunia.

Ajali hiyo imetokea katika eneo la Bugongwa jijini Mwanza,  Jumanne saa 4:45 asubuhi. Chanzo cha ajali kinadaiwa kuwa dereva wa gari aina ya fuso alipokuwa akigeuza katikakati ya barabara, ambapo dereva wa basi la Bedui alishindwa aliliparamia fuso hilo.

Shija Malado ni shuhuda aliyenusurika katika ajali hiyo mbaya, alimtaja dereva wa basi hilo lenye namba za usajili T 853 BRB aliyefariki papo hapo kwa jina moja tu la Mihayo.

“Watu 10 waliopata ajali hiyo saba kati yao ni madiwani wa wilaya ya Kwimba. Mimi nimeruhusiwa muda mfupi baada ya kupata matibabu katika hospitali ya Bugando”, alisema Malando.
Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – Mwanza,

Saturday, October 13, 2012

Breaking News.RPC wa Mwanza Liberatus Barlow auwawa

Marehemu Liberatus Barlow enzi za uhai wake
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Kamishina Mwandamizi wa Polisi (SACP) Liberatus Barlow ameuawa usiku wa kuamkia leo katika tukio linalohusishwa na ujambazi.

Taarifa kutoka Mwanza ambazo zimethibitishwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Said Mwema zinasema kuwa Kamanda Barlow aliuawa baada ya kumrudisha dada yake kutoka katika kikao cha harusi ya ndugu yao huko Kitangili.

Kwa mujibu wa Mwema tarai jeshi la Polisi limetuma askali wa kupeleleza maujai hayo na ameomba ushirikinao wa wananchi ili kufanikisha kuwatia mbaroni wahusika wa mauaji.

Friday, October 12, 2012

RCC ya Kagera yapiga 'stop'mradi wa bilioni kumi na moja

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian Massawe
Phinias Bashaya,Bukoba
KAMATI ya Ushauri ya Maendeleo ya Mkoa wa Kagera (RCC)imesitisha mkataba wa ujenzi wa  mradi wa jengo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa utakaogharimu zaidi ya shilingi bilioni kumi na moja  na kuagiza yawepo mazungumzo  na Serikali kutafuta njia nzuri ya kutekeleza mradi huo.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya mjadara mkali wa wajumbe ambao baadhi yao ilikiwemo kundi la wabunge wakidai mradi huo ambao hadi unasitishwa ulikuwa umetumia zaidi ya bilioni moja kuwa ulikuwa ni mzigo kwa kuendelea kuzalisha madeni.

Walisema kuwa pamoja na lengo zuri la kuwa na ofisi za Mkuu wa Mkoa katika Kata ya Kahororo mradi huo ulikuwa hautekelezeki kwa sasa na baadhi kushauri watafutwe wawekezaji watakaoweka vitega uchumi katika jengo hilo lenye vymba tisini.

Mbunge wa Bukoba Vijijini Jasson Rweikiza alisema Mkoa hauna uwezo wa kuendeleza mradi huo akidai uamuzi haukuwa sahihi,huku Mbunge wa Nkenge Ansupter Mshama akipendekeza jengo hilo litumike kwa shughuli za utalii.

“Mlianza vyema lakini huu sio wakati unaofaa kuwa na mradi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa yenye vyumba tisini,tulifanye jengo la utalii wananchi hawawezi kuchangia jengo wakati huo ukawataka wachangie zahanati”alisema Mshama

Hata hivyo kundi jingine la wajumbe miongoni mwao akiwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Kashunju Runyogote walitetea ujenzi wa mradi huo ingawa changamoto ilikuwa ni tatizo la upatikanaji wa fedha usiokwenda na mipango ya utekelezaji.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Nassoro Mnambila aliwaeleza wajumbe wa kikao hicho kuwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali iliutaka Mkoa utafakari tena kama kuna umuhimu wa kuendelea na mradi huo ilhali Serikali ikiwa inasuasua kutoa fedha za ujenzi wa ofisi hiyo.

Naye Mwenyekiti wa kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian Massawe alisema wataendelea kufanya mazungumzo na Serikali kushauriana jinsi ya utekelezaji wa Mradi huo na taarifa itawasilishwa katika kikao kijacho.