Monday, April 30, 2012

Haikuwa kazi rahisi kwa Dk Mbasa kunyakua ubunge Biharamulo

Dk Athony Mbasa mbunge wa Biharaumlo siku alipofunga kampeini za uchaguzi mkuu mwaka 2010 katika Mji wa Biharamulo
Kabla ya Dk Mbasa  kutangazwa mshidi hali ilikuwa hivi katika viwanja vya Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo.Matokeo yalitangazwa usiku huku kukiwa na ulinzi mkali wa askali Polisi 

Wanafunzi wa Kahororo Sec ndani ya Chumba cha Habari

Wanafunzi wa Kahororo Sekondari iliyopo nje kidogo ya Mji wa Bukoba wakiwa katika Ofisi za Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Kagera mjini Bukoba

Hapa wakinukuu mambo muhimu yaliyotolewa ufafanuzi na Waandishi jinsi wanavyofanya kazi na changamoto zinazowakabiri

Kiongozi wa wanafunzi James Ludovick kutoka Kahororo Sekondari akiuliza mbinu zinazotumiwa na waandishi kupata habari sahihi hasa pale wahusika wanapokataa kutoa ushirikiano kwa kukataa kuhojiwa juu ya suala husika

Mwandishi wa Kampuni ya IPP LTD Prudence Kibuka akitoa ufafanuzi kwa wanafunzi hao

Ili kukidhi hamu ya wanafunzi hao juu ya masuala ya habari,majibu mengine ilibidi yatafutwe kwenye mtandao wa Intanet.Hapa ni Lilian Lugakingira mwandishi wa Mwananchi Communication

Thursday, April 26, 2012

Kutana na wanafunzi wa Nshamba

Masomo na kifungua kinywa nje ya darasa
Baadhi ya Tafiti zinadai kuwa uji huongeza mahudhurio ya wanafunzi shuleni
Muda wa mapumziko umekwisha,ni wakati wa kuendelea na masomo darasani

Historia ya Tanganyika itawakumbuka

Toka kushoto juu ni Bi Sifaeli Choma aliyebeba kibuyu kilichokuwa na udongo wa Tanganyika na kumkabidhi Mwalimu. Anayefuata ni Bw Omar Hassan Mzee aliyebeba chungu kikubwa ambacho ndicho kilichobeba udongo wa Tanganyika na Zanzibar ambao ulipochanganywa tu ndipo Muungano ukawa umezaliwa, na kulia ni Bi Khadija Rajab Abbas, aliyebeba kibuyu chenye udongo wa Zanzibar. Mara zoezi hilo lilipokamilika ndipo jina Tanzania likaanza kutumika rasmi. Picha ndogo ya kati inaonesha waasisi wa Muungano wakipita mitaani kusherehekea siku hiyo ya kihistoria, huku wananchi wakiwa wamejipanga barabarani jijini Dar es salaam kuwashangilia wakitokea uwanja wa Uhuru.LEO NI MIAKA 48 TANGU KUASISIWA KWA MUUNGANO

Usinipige picha,nafunika uso!

Huyu ametoa sharti la kupigwa picha akiwa amefunikwa uso.Hapa ni eneo la Bohari ya Mkoa
Wiki jana katika Kijiji cha Rusumo wilayani Ngara.Mkuu wa Mkoa wa Kagera Fabian Massawe akiungana na wananchi katika maadhimisho ya kilimo cha Migomba.
Watoto wakionyesha umahili  katika sanaa za maonyesho wilayani Karagwe wakati wa kuzindua mashamba ya mfano ya miti rafiki wa amazingira

Tuesday, April 24, 2012

CHELSEA yatangulia Allianz Arena

Chelsea wakishangilia ushindi
Klabu ya soka ya Chelsea ya Uingereza imefuzu kuingia fainali ya klabu bingwa barani Ulaya, licha ya nahodha John Terry kuonyeshwa kadi nyekundu.
Mchezo wa Jumanne ulikwisha kwa sare ya 2-2, lakini Chelsea ikapata ushindi ikiwa na jumla ya magoli 3-2.
Timu ya The Blues (Chelsea) ilikuwa imelemewa baada ya Sergio Busquets na Andres Iniesta kuiwezesha Barca kuongoza katika mechi hiyo.
Lakini Ramires kwa ustadi aliuinua mpira juu na kuandikisha bao safi la Chelsea katika mechi hiyo.
Barca walipata penalty, lakini Lionel Messi, licha ya maarifa yake na sifa nyingi katika ufundi wa penalty, aliishia kugonga mwamba.
Wakati wa muda wa majeruhi wa dakika tatu zilizoongezwa, Fernando Torres alionyesha utulivu wa hali ya juu sio tu kwa kushambulia ngome ya Barca ambayo kwa muda mrefu ilikuwa haiguswi, lakini vile vile kwa kumchenga hata kipa Valdes na kuutia mpira wavuni kwa makini.
Mapema wiki hii, Torres alikuwa amenukuliwa akisema “sio siku zote timu bora hupata ushindi”, matamshi ambayo ni ndoto iliyotimia.
Sasa vijana wa Chelsea wa Roberto di Matteo wanasubiri kufahamu kama watacheza na timu ya kocha wao wa zamani, Jose Mourinho, akiwa mkufunzi wa Real Madrid, au pengine watakutana na Bayern Munich, ambao uwanja wao ndio utakaotumiwa kuandaa fainali ya ligi ya klabu bingwa.
Real Madrid na Bayern zinapambana LEO jioni, 25 Aprili 2012.
Tatizo la Chelsea ni kwamba katika fainali ya Jumamosi tarehe 19 Mei, sasa watazikosa huduma za nahodha John Terry, Ramires, Branislav Ivanovic na Raul Meireles mjini Munich, kutokana na kuadhibiwa kwa kucheza mchezo wa kuumizana katika nusu fainali.

Mkutano wa KCU ulivyofanyika leo mjini Bukoba

Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Kagera John Binushu akijadiri jambo na Mrajisi wa Vyama Vya Ushirika Mkoani Kagera Rwenkiko Shorosi
Mjumbe kutoka Chama Cha Msingi Rukurungo Charles Kihima kwa umakini mkubwa akipitia kabla wakati wa mkutano wa KCU  uliofanyika leo
Mzee Super Kalugaba Mwenyekiti wa Chama Cha Msingi Kamachumu kisisitiza uboreshaji wa Hotel ya Lake na kuonyesha mashaka juu ya usimamizi wa Hotel hiyo
Mwanasheria kutoka Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika Dk Audax Rutabanzibwa naye amehudhuria Mkutano huo
Mjumbe kutoka Chama Cha Msingi Ibwera Wilaya ya Bukoba Vijijini Sadru Nyangasha akichangia moja ya hoja zilizojitokeza wakati wa Mkutano
Mjumbe kutoka Kmachumu Archard Muhandiki akitoa maoni ya kuboresha Hotel ya Lake inayomilikiwa na KCU ambayo wajumbe wametuhumu usimamizi mbaya unaosababisha iendeshwe kwa hasara inayomrudia Mkulima
Mkutano wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Kagera(KCU)umefanyika leo mjini Bukoba katika Hotel ya COOP inayomilikiwa pia na Chama hicho kinachoundwa na vyama vya  msingi vya Wilaya za Muleba,Missenyi na Bukoba.

Mkutano huo uliokuwa unajadiri hesabu za Mizania na Mapato,wajumbe  pamoja na mambo mengine walishangazwa na taarifa za Hotel ya Lake inayomikikiwa na KCU kupata faida ya shilingi milioni moja baada ya kuwekeza milioni 87 kwa mwaka uliopita.

Monday, April 23, 2012

Wananchi walioiliza Kamati ya Profesa David Mwakyusa

Moja ya familia katika Kitongoji cha Kazizi Kijiji cha Bubare Wilayani Missenyi ambayo haina makazi baada ya nyumba yao kubomolewa kufuatia mgogoro unaoendelea kufukuta kati ya wananchi na wawekezaji
Mwanamke katika kitongoji cha Kazizi akiwa nje ya mabaki ya nyumba yake ikiwa ni sehemu ya nyumba 36 zilizoteketezwa moto wananchi wakishinikizwa kuwapisha wawekezaji.Mama huyu pia anaonekana ni shabiki wa Arsenal
Wanafunzi katika Kijiji cha Bugango Wilayani Missenyi ambao wameathiriwa na mgogoro kati ya wananchi na wawekezaji
Faustin Mukasa,mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya Sekondari Bugango akiwa na kovu la risasi aliyopigwa kwa madai ya kukatiza katika eneo la Mwekezaji wakati akienda shule

Jana kabla ya kuhairishwa kwa kikao cha Bunge,Kamati ya Mifugo Kilimo na Maji ilitoa taarifa ya kile ilichoshuhudia baada ya kutembelea maeneo yenye migogoro kati ya wananchi na wawekezaji kwenye lanchi zilizoko Mkoani Kagera.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Profesa David Mwakyusa alisema mmoja wa wajumbe wa Kamati hiyo alitoa machozi baada ya kujionea hali halisi katika lanchi za Missenyi na ukiukwaji mkubwa wa haki za Binadamu.
Moja ya mapendekezo ya Kamati hiyo kwa Serikali ni kurudiwa kwa mipaka na kuwa wawekezaji ambao wanaishi nje ya nchi bila kuendeleza maeneo yao huku wakiendesha unyanyasaji kwa wananchi wanyang’anywe maeneo yao.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema Serikali itazingatia mapendekezo na ushauri.Tume ilifika  Kagera mwezi Februari ikiongozwa na Neema Mgaya(Viti maalumu Vijana CCM) akiambatana na Titus Kamani(Busega)Seleman Jafo(Kisarawe)Waride Jabu na Asaa Hamad wote kutoka Zanzibar.

Mliosoma Ihungo Sekondari

Historia inawataja Askofu wa Jimbo Kathoriki la Bukoba Nestory Timanywa,Mwenyekiti wa CHADEMA,Freeman Mbowe na aliyewahi kuwa Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dk Diodorus Kamala.
Pia Waziri wa Nishati na Madini William Ngereja,mhadhili wa chuo Kikuu cha Dar es salaam Ally Bashiru na mamia ya wengine katika nyanja tofauti tangu mwaka 1929.
Sifa pekee inayoitofautisha na shule nyingine kongwe hapa nchini ni mafanikio ya mwaka 1968 wanafunzi wake walipoongoza katika matokeo ya mitihani miongoni mwa shule za Jumuiya ya Madola.
Maabara ya kemia enzi hizo ilijenga kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi 18,hivi sasa inatakiwa kutumiwa na wanafunzi 176 na hivyo kusababisha changamoto kubwa kwa walimu na wanafunzi.
“Maabara ya kemia ina uwezo wa kutumiwa na wanafunzi 18 hii ni changamoto kubwa inayosababisha utendaji kuwa mdogo”anafafanua mwalimu wa somo la Kemia Tumwesige Philemon

Bei ya viwanja Bukoba karibu na bure!

TANGAZO LA VIWANJA
Manispaa ya Bukoba kwa kushirikiana na Dhamana ya Uwekezaji Tanzania (UTT) imekamilisha upimaji wa viwanja takribani 5,000 katika maeneo  mbalimbali.
HivyoMkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba anawatangazia wananchi  wote kuwa, viwanja 5,000 sasa vitauzwa kwa utaratibu ufuatao:-
1.      Kununua Fomu ya maombi ya kiwanja Tshs. 10,000/=(haitarejeshwa) katika Benki ya Posta tawi la Bukoba tu, ambapo itapaswa kujazwa na kurejeshwa.
2.       Fomu za viwanja zitauzwa kuanzia tarehe 23/04/2012 hadi 22/05/2012.
3.      Muombaji atapaswa kulipa Tshs.200,000 kama dhamana (Security Deposit) ya kupata kiwanja cha makazi na Tshs.500,000 kama kiwanja si makazi au muombaji ni taasis/shirika. Fedha hii itarejeshwa kama muombaji hatafanikiwa kupata kiwanja kupitia Benki ya Posta.
4.       Kila mita ya mraba ya eneo (1M2 ) itauzwa kati ya Tshs.3,000 – 4,500 kwa kutegemea matumizi ya kiwanja na eneo  ambalo kiwanja kipo.
5.       Wale waliotwaliwa maeneo yao kwa ajili ya upimaji viwanja pamoja na wale waliowahi kuchangia gharama za upimaji toka mwaka 2002 nao watapaswa kununua fomu. Punguzo lao maalum la bei litakuwepo wakati wa kuuza kiwanja.
6.       Viwanja vyote vimewekewa barabara na vipo jirani na miundombinu muhimu ya  maji na umeme.
7.       Bei ya kiwanja ni pamoja na kutayarishiwa hati miliki ya kiwanja atakachopewa mnunuzi.


                            Robert Kwela
KAIMU MKURUGENZI WA MANISPAA
BUKOBA.

Chadema yateka ngome ya CCM Missenyi

Baadhi ya akina mama na watoto katika kijiji cha Burifani ulipo mji wa Kyaka wilayani Missenyi wakifanya biashara ya ndizi za kuchoma na mahindi, wateja wao wakubwa wakiwa ni abiria wanaosafiri kati ya miji wa Bukoba,Karagwe na mpaka wa Mutukula
 Missenyi

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema)kimeshinda uchaguzi wa Mwenyekiti wa kijiji cha Burifani Kata ya Kyaka Wilayani Missenyi ambacho ni makazi ya vigogo wa CCM akiwemo Mbunge wa Jimbo la Nkenge Ansupter Mshama.

Mgombea wa Chadema Deogratias Laurian aliibuka na kura 401 dhidi ya 129 za mgombea wa CCM Mathias Kibarwiga. Mgombea wa TLP Plasid Vedasto akiambulia kura 2,ambapo wakati wa kutangaza matokea Msimamizi Msaidizi Magreth Kamya alisema kura 4 ziliharibika.

Pia katika maeneo mbalimbali ya mji wa Kyaka ambao upo kijiji cha Burifani ulitawaliwa na askali polisi na mgambo waliokuwa wamejihami kukabiriana na vurugu zozote ambazo zingetokea.

Vigogo wengine wa CCM wanaotoka katika kijiji hicho ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Fidelis Kibarabara,Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Missenyi ambaye pia ni Diwani wa Kata hiyo,Projestus Tegamaisho,Katibu wa Jumuiya ya Vijana na Katibu wa UWT,ambapo pia Ansupter Mshama ni Mwenyekiti wa UWT.

Uchaguzi huo ambao ulifanyika jana Jumapili awali ulitawaliwa na mizengwe kwa mgombea wa Chadema kuwekewa pingamizi na upande wa CCM wakimtuhumu kwa vitendo vya rushwa na hivyo uchaguzi kuhairishwa mara mbili.

Hata hivyo pingamizi dhidi ya tuhuma za rushwa hazikuwa na uthibitisho na kutupiliwa mbali na Msimamizi wa uchaguzi wa Wilaya Issaya Mbenje ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri.

Miongoni mwa sababu zinazotajwa kukiponza Chama Cha Mapinduzi katika uchaguzi huo ni kero za vizuizi vinavyodaiwa kuwanufaisha baadhi ya viongozi, na mgogoro wa kiwanja cha Msikiti unaodaiwa kuingiliwa na kiongozi mmoja wa Wilaya.

Pia miongoni mwa sababu zilizompa ushindi mgombea wa Chadema ni wananchi kupigwa danadana kuhussu malipo ya fidia ili kupisha ujenzi wa barabara ya Kyaka Bugene inayojengwa kwa kiwango cha lami.
 
 
 
 
 
 

Sunday, April 22, 2012

Umasikini mwingine ni balaa!

Picha hii imetolewa kwenye mtandao wa FB

Rais Jacob Zuma tena

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini akiwa katika vazi la asili la Kabila lake wakati wa sherehe za kuoa mke wa nne
Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini ameoa mke wa nne, kwenye sherehe ya jadi ambapo wake zake wengine watatu pia walihudhuria sherehe hizo.
Zuma mwenye umri wa miaka 70, alivaa ngozi ya chui na kubeba mkuki na ngao, mavazi ya jadi ya Kizulu, kwenye harusi iliyofanywa jimbo la KwaZulu-Natal.
Bi arusi, Bongi Ngema, amefuatana na Rais Zuma kwenye ziara zake rasmi kwa miaka kadha ambapo imedaiwa sherehe hizo zimegharimiwa na Zuma mwenyewe.Rais Zuma ni mtu anayefuata mila za kabila lake la Zulu.
Mwenyewe amezaliwa na baba aliyekuwa na wake kadha na ndoa yake kwa Bi Ngema ni ya sita.Mmoja, ambaye ni waziri wa serikali, alimuacha naa mwingine alijiua.
Nyumba ya Rais Zuma imetengenezwa kwa ustadi na ukubwa wa kutosha ili kuweza kukidhi mahitaji ya familia yake ambapo inaaminika ana watoto zaidi ya ishirini.

Ubabe wa Mfalme Simba katika mbuga ya Serengeti

Mnyama aina ya Simba mpaka leo ndiye anaaminika kuwa mfalme wa pori ambaye maisha yake yote hutegemea kitoweo cha wanyama wengine.Hata hivyo hudaiwa wakati mwingine huzidiwa na kula majani!

Simba huishi kama familia ya baba mama na watoto ambapo mara nyingi Simba jike ndiye mwindaji wakati huo dume hufanya kazi ya kulinda familia na watoto dhidi ya wanyama wengine wanaoweza kuwadhuru..

Maelezo mengine ambayo hayana ushahidi wa kisayansi ni kuwa Simba dume hupenda kubaki nyumbani kulinda mji kutokana na hofu ya kuumia wakati wa uwindaji.Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali Simba dume hufikia hadi wastani wa kilo 186 na jike 126.

Simba dume wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wana muda mfupi zaidi wa kuishi ikilinganishwa na Simba jike.Taarifa zinaonyesha kuwa Simba dume katika hifadhi hiyo anaishi hadi miaka 12,ambapo jike hifikia hadi umri wa miaka 15.

Saturday, April 21, 2012

Brigedia Adam Mwakanjuki kuzikwa kesho Zanzibar

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
21/04/2012

Aliyekuwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Brigedia Mstaafu Adam Clement Makanjuki anatarajiwa kuzikwa hapo kesho jioni katika makaburi ya Mwanakwerekwe Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Dk.Khalid Muhammed imeeleza kuwa mwili wa Marehemu unatarajiwa kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume majira ya saa tatu na nusu za asubuhi.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa mara baada ya kuwasili Mwili huo utapelekwa katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani Kikwajuni Zanzibar ambapo Viongozi wa Kitaifa,Mabalozi na Wawananchi watapata fursa ya kuuaga mwili wa Marehemu.

Mara baada ya shughuli hiyo kumalizika Mwili utapelekwa katika Kanisa la Anglikana Mkunazini mnamo saa nane za mchana kwa ajili ya Ibada maalum.

Marehemu Brigedia Mstaafu Adam Clement Makanjuki alifariki Dunia hapo Juzi katika Hospitali ya Lugalo jijini Dar es Salaam baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Kabla ya kifo chake Marehemu aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zikiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba na Utawala Bora,Waziri wa Kilimo,Mifugo na Mali Asili,Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi,Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Marehemu amefariki akiwa na umri wa miaka 70 ameacha Kizuka na watoto watano.

IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR

21/04/2012

Uyoga zamani ulipatikana kila mahali,leo ni mboga adimu

Mtoto anayekadiriwa kuwa kati ya umri wa miaka 7-8 akisaka wateja wa Uyoga mwendo mfupi kabla ya kukifikia kivuko cha Kyanyabasa Wilaya ya Bukoba Vijijini.Katika Mkoa wa Kagera Shirika la Maendeleo ya Wakulima(MAYAWA)pia linajihusisha na uhamasishaji wa jamii katika kupanda zao la uyoga.Mbegu za zao hilo zinapatikana katika ofisi zao zilizopo barabara ya kuelekea Kyakairabwa

Viroba vya konyagi vyawaponza majambazi kutoka BurundiKamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera Henry Salewi akiwa katika moja ya Mikutano ya Polisi Jamii Wilayani NgaraJeshi la Polisi lilianzisha mpango wa Polisi Jamii katika jitihada za kuwashirikisha wananchi kudhibiti uhalifu na wahalifu katika maeneo yao
 Bukoba
POLISI Mkoani Kagera wamemuua jambazi anayedaiwa kutoka nchi jirani ya Burundi na mwingine kujeruhiwa vibaya baada ya kufanya uporaji katika kijiji cha Murukukumbo Wilayani Ngara.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoani Kagera Henry Salewi usiku wa April 17,watu watatu walivamia kijiji hicho na kufanya uporaji katika duka la Paschal Timotheo(36)na baada ya kufanya uporaji walipiga risasi hewani.

Amesema majambazi hao wakiwa na bunduki aina ya SMG waliamuru wananchi kulala chini na kupora simu tatu aina ya Nokia,kilo 20 za sukari viroba vya pombe aina ya Konyagi na fedha kiasi cha shilingi laki moja na nusu.

"Baada ya kusikia mlio wa risasi askali waliokuwa doria walifuatilia hadi eneo la tukio na kukuta umefanyika uporaji na kuamua kwenda kuweka mtego katika njia inayovuka kwenda Burundi"alibainisha Salewi.

Pia amesema ilipofika majira ya saa sita na nusu usiku majambazi hao walifika katika eno hilo wakiwa wamebeba vitu walivyopora na baada ya kukataa amri ya kujisalimisha yalifyatuliwa risasi nao kujibu na kumuua mmoja huku wengine wakikimbia.

Hata hivyo Kamanda Salewi amesema majambazi wawili waliosalimika walikimbia na kuvuka mpaka na kuwa jambazi mmoja amelazwa katika hospitali moja nchini humo kutokana na majeraha aliyopata.

Amesema jambazi aliyeuwawa katika eneo la tukio baada ya kupekuliwa alikutwa na bomu lenye namba 82-256-94650,simu zilizoporwa na kitambulisho kilichomtaja kwa jina la Kongera Mutabilolele Mkazi wa kijiji Murama Mkoa wa Muyinga nchini Burundi.

Pia Kamanda Salewi amewakumbusha wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo hasa kwa kutoa taarifa za wageni wanaowatilia shaka katika maeneo yao.

Friday, April 20, 2012

JAPAN yakabidhi pikipiki nane kukusanya takwimu za kilimo Mkoa wa Kagera

Bukoba
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian Massawe amekabidhi pikipiki nane kwa Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya na Manispaa kwa ajili ya kukusanya takwimu mbalimbali za kilimo kutoka  vijijini katika Mkoa wa Kagera.
Pikipiki hizo zimetolewa na serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika ikishirikiana na shiririka la Kimataifa Uhusiano la nchini Japan (Japan International Cooperation Agency, (JICA)   ambalo limewakilishwa na Bi. Akasaka Kyoko.
Mhe Massawe pia amewasisitiza Wakurugenzi wa Halmashauri na Manispaa kutunza pikipiki hizo na kuzifanyia kazi iliyokusudiwa na si vinginevyo. Aidha aliwaomba maafisa kilimo kutumia vitrndea kazi hivyo kukusanya taarifa sahihi.
Pamoja na pikipiki hizo JICA pia waliendesha mafunzo ya ukusanyaji takwimu na kugawa kompyuta moja na vifaa vingine  kwa kila Halmashauri ya wilaya na manispaa kwa ajili ya kusaidia kukusanya na kutunza takwimu za kilimo vijijini.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian Massawe akihakiki pikipiki zilizotolewa kama ziko imara kwa ajili ya kutumika kufanya kazi ya kukusanya takwimu za kilimo katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kagera.
Mkuu wa Mkoa aliwashukuru JICA kwa kujitolea kuleta maendeleo Tanzania na hasa katika mkoa wa Kagera. Pia amewahakikishia JICA kuwa serikali itaendelea kuhamasisha wananchi kuondokana na kilimo cha kujikimu na kuhamia katika kilimo chenye tija.
Na: Sylvester Raphael

AFISA HABARI- MKOA WA KAGERA
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian Massawe akimshukuru Bi. Akasaka Kyoko Mwakilishi wa Shirika la kimataifa la Japani (JICA) kwa ufadhili wa Pikipiki za kukusanya Takwimu za Kilimo vijijini

Mkuu wa Mkoa wa Kagera  Kanali Mstaafu Fabian Massawe akikabidhi Pikipiki kwa Wawakilishi wa Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya na Manispaa.Picha zote kwa Hisani ya Afisa Habari wa Mkoa wa Kagera.


Thursday, April 19, 2012

Ubeligiji yatumia Bilioni 120 kuboresha zao la migomba Mkoani Kagera

Ngara
Shirika la Maendeleo la Ubeligiji(BTC)kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania limetumia zaidi ya shilingi bilioni 120 kwa ajili ya mradi wa migomba unatekelezwa katika wilaya zote za Mkoa wa Kagera na Wilaya ya Kibondo Mkoani Kigoma.

Hayo yamebainishwa na Ofisa Mradi huo Bwana Cranme Chiduo wakati wa maadhimisho ya siku ya zao la ndizi yaliyofanyika katika kijiji cha Rusumo wilayani Ngara ambayo yamefunguliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian Massaawe.

Amesema tangu Mradi huo uanzishwe miaka minne iliyopita mbali na kutumia kiasi hicho cha fedha pia umepata mafanikio makubwa katika usambazaji wa mbegu bora za migomba na kuwasaidia wasindikaji na wasambazaji kuongeza thamani ya zao la ndizi.

Mratibu wa Mradi wa migomba unaofadhiliwa na Serikali ya Tanzania na Ubeligiji Mgenzi Byabachwezi akitoa maelezo ya jinsi ya kudhibiti magonjwa yanayoshambulia migomba kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian Massawe alipotembelea shamba la kikundi cha Mshikamano Kata ya Magoma Wilayani Ngara leo asubuhi
Mwenyekiti wa Mtandao wa Vikundi vya Usindikaji wa Mazao ya Wilayani Missenyi(MVUMI)Bwana Fredrick Kitone akionyesha ustadi wa kumenya ndizi kwa ajili ya kuzianika na kuandaa makopa ambayo hutoa unga unaotumika kwa ajili ya ugali unaotokana na ndizi
Katika maadhimishisho hayo Mratibu wa Mradi wa Migomba Mkoani Kagera Mgenzi Byabachwezi amesema hadi Desemba mwaka jana zaidi ya miche bora ya migomba milioni mbili imesambazwa kwa wakulima 45,843 katika maeneo unapotekelezwa mradi huo.

Wednesday, April 18, 2012

Mlima wa Simba wasambaratishwa


Eneo maarufu kwa jina la Mlima wa Simba katika pori la Biharamulo likiwa linasambaratishwa katika utengenezaji wa barabara ya kiwango cha lami unaoendelea kuiunganisha Muleba na Biharamulo


Kambi ya wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu barabara kuu ya kuelekea Wilaya ya Ngara.Machmbo hayo yapo wilaya ya Biharamulo

Wanunuzi wakiuziwa nyama katika Kijiji cha Rusumo wilayani Ngara


Tuesday, April 17, 2012

Kanali Massawe.Kagera haichomozi kwenye vyombo vya habari


Bukoba
MKUU wa Mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian Massawe amewaasa waandishi wa habari Mkoani hapa kutoa kipaumbele kwa habari za kutangaza maendeleo na fursa mbalimbali zilizopo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo mchana Kanali Massawe amesema habari nyingi za maendeleo hazijatangazwa vya kutosha katika vyombo vingi vya habari kama ilivyo katika Mikoa mingine.

Amesema Mkoa wa Kagera unatekeleza mipango mingi ya maendeleo ambayo haipewi nafasi kubwa na waandishi wa habari na kuwataka pia kuandika habari za kuvutia fursa mbalimbali za uwekezaji.

'Mkoa wetu wa Kagera una ukame wa habari katika vyombo vingi vya habari,tunataka uanze kusikika tangazeni pia mambo yanayoweza kuwaathiri wananchi ili mradi mpate ufafanuzi wa viongozi husika'alisema Massawe

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa aliwakumbusha waandishi wa habari kwenda kwa viongozi sahihi wanaoweza kutoa ufafanuzi wa habari au mambo wanayoyafuatilia kabla ya kuyatangaza au kuchapishwa katika vyombo vya habari.

Alitumia nafasi hiyo ya kusisitiza kampeini ya usafi inayoendelea katika Wilaya zote za Mkoa wa Kagera huku akiwataka wananchi kutoa ushirikiano kuwabaini watu wanaowaachisha wanafunzi wa kike masomo baada ya kuwabebesha ujauzito.

Pia Massawe aliwaonya viongozi wa kisiasa wanaokwamisha utekelezaji wa mambo mbalimbali katika maeneo yao kwa kisingiziio cha kuwatetea wapiga kura wao.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian Massawe akiwaonyesha waandishi wa habari baadhi ya habari zilizochapishwa katika magazeti hivi karibuni zinazohusu Mkoa wa Kagera
Baadhi ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa
Waandishi wa habari wakinukuu mambo muhimu yaliyokuwa yakitolewa ufafanuzi na Mkuu wa Mkoa wa Kagera
Mkurugenzi mpya wa Radio Kasibante FM ya mjini Bukoba Richard Leo(kulia)akiwa na Katibu Tawala Msaidizi Richard Kwitega wakati wa Mkutano wa Mkuu wa Mkoa wa Kagera na waandishi wa habari
Mkurugenzi wa Radio Vision Fm ya mjini Bukoba(Valerian) akitoa ufafanuzi wa jinsi kituo chake cha Redio kinavyoshiriki mipango mbalimbali za kuhamasisha maendeleo ya Mkoa wa Kagera