Tuesday, August 21, 2012

Dk Kafumu avuliwa ubunge wa Igunga na mahakama

Mahakama Kuu Kanda ya Tabora imetoa hukumu ya kesi ya ubunge iliyokuwa ikimkabili mshindi wa ubunge jimbo la Igunda Dk Peter Kafumu (CCM). 

Hukumu hiyo ya kupinga matokeo yaliyompatia ushindi Dk Kafumu imetolewa leo ambapo imemuengua mbunge huyo katika nafasi yake ya ubunge. 

Shauri hilo lilifunguliwa na mlalamikaji Joseph Kashindye dhidi ya Dk Kafumu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na msimamizi wa uchaguzi.

Wednesday, August 15, 2012

Sheria yadaiwa kuwabagua walemavu wa akili

Mtetezi wa Haki za Watu wenye Ulemavu na Rais wa Shirika la Kutetea Haki za Binadamu(POTA)Idrisa Masalu akitoa mada katika semina ya kutetea haki za walemavu wa akili iliyofanyika mjini Bukoba
Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Kagera Rebeca Gwambasa akifungua semina
Washiriki wa semina
Picha ya pamoja na mgeni Rasmi
Mtaalamu wa kitengo cha watoto wenye ulemavu wa akili kutoka Bunazi Wilayani Missenye Mwl Gervase Anatory akitoa mchango wake wakati wa semina
Phinias Bashaya,Bukoba
SHERIA ya watu wenye ulemavu imetajwa kuwabagua watu wenye ulemavu wa akili baada ya haki zao kutofikiwa kwa urahisi tofauti na walemavu wengine huku sheria ikishindwa kulitaja moja kwa moja kundi hilo.

Hayo yamebainishwa katika semina iliyoandaliwa na Chama kwa Ajili ya Watu wenye Ulemavu wa Akili(TAMH)na kuwakutanisha wataalamu wa watu wenye ulemavu wa akili kutoka wilaya mbalimbali za Mkoa wa Kagera.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa chama hicho Anacret Rugaihuruza watu wenye ulemavu wa akili wana mahitaji makubwa zaidi ya wenzao na sheria ilitakiwa kufafanua haki zao bila kujumuishwa moja kwa moja katika sheria ya jumla ya haki za walemavu.

Alisema chama hicho pamoja na jukumu la kuwasemea walemavu wa akili ni muhimu jamii kutambua kuwa hata walemavu wa kundi hilo wana haki ya kupata mahitaji mengine kama kuoa na kuwa na familia.

Katika semina hiyo iliyofadhiliwa na Shirika la The Foundation for Civil Society,Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Kagera Rebeca Gwambasa alikiri sheria ya walemavu kuwa na mapungufu  yanayolitenga kundi la walemavu wa akili.

“Katika haki za walemavu kundi la walemavu wa akili halifikiwi na haki hizo inaonekana wakati sheria inatungwa makundi yote hayakushirikishwa hata hivyo Serikali iko tayari kupokea ushauri”alisema Gwambasa

Miongoni mwa washiriki wa semina hiyo Gervase Anatory ambaye ni mtaalamu wa Kitengo cha watoto wenye ulemavu wa akili Bunazi Wilayani Missenye alisema hata elimu jumuishi inayowachanganya kundi hilo na wasio na ulemavu bado haiwasaidii kutokana na kuwepo vitendo vya unyanyapaa.

Alisema watoto wenye ulemavu wa akili wanapochanganywa na wengine tatizo lao linakuwa kubwa zaidi na kuwa jamii inatakiwa kuwa na mapenzi mema kwa walemavu na kuwasaidia kupata mahitaji mbalimbali.

Naye mshauri wa watu wenye ulemavu ambaye pia ni Rais wa Shirika la Kutetea haki za binadamu(POTA)Idrisa Massalu alisema umefika wakati wa kutengeneza sehemu maalumu 'Camps'kwa ajili ya kundi hilo kwani hukosa mwelekeo wanapomaliza masomo yao.

Pia wanachama na viongozi wa chama hicho wakati wa semina hiyo watajifunza usimamizi na udhibiti wa fedha na kuandaa mpango mkakati utakaotekelezeka.
Tuesday, August 14, 2012

Uzinduzi wa jengo la VIP katika hospital ya Mkoa wa Kagera

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian Massawe akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi
Ugua pole.Mmoja wa wagonjwa katika jengo lililozinduliwa rasmi leo
'Unajisikiaje hali yako mgonjwa'
Ndani ya chumba cha gharama ya shilingi 75,000 kwa siku
Chumba cha kujifungulia mama wajawazito,gharama ni shilingi laki moja
Mkuu wa Mkoa akipima uzito ikiwa ni moja ya huduma zinazopatikana katika jengo jipya la daraja la Kwanza
Tuko Pamoja mama
Msanii 'Babu Ayoub' akituzwa na mgeni Rasmi baada ya kulitawala jukwaa

Monday, August 13, 2012

Chato kubinafsisha ujenzi wa nyumba za walimu

Mwanafunzi Leah Sebastian anayesoma darasa la tano shule ya Msingi Katoju iliyopo Kijiji cha Buhanga Kata ya Bujugo Wilaya ya Bukoba Vijijini akitoka katika shughuli za shamba.
Hawa ni wanafunzi wa shule ya Msingi Kajure iliyopo katika Kisiwa cha Bumbire Wilayani Muleba
Phinias Bashaya,Chato
Halmashauri ya wilaya ya Chato Mkoani Kagera inakusudia kubinafsisha mpango wa ujenzi wa nyumba za walimu baada ya majadiliano yanayoendelea baina yake na serikali za vijiji ili kupata ardhi kwa ajili ya mpango huo.
 Hatua hiyo inalenga kukabiliana na tatizo la uhaba mkubwa wa nyumba za walimu ambalo  wadau wanalinaelezea kuwa miongoni mwa sababu za kudorora kwa maendeleo ya elimu wilayani humo.
Katika ripoti ya utafiti wa Mradi wa  Uwezo Tanzania 2011, wilaya ya Chato ilishika nafasi ya 66 miongoni mwa wilaya 132 zilizofanyiwa utafiti nchini katika stadi za kusoma Kiswahili, Kiingereza na kufanya Hisabati za kiwango cha darasa la pili.
 Kwa mujibu wa viongozi wa  halmashauri, wilaya ya chato ilikuwa na upungufu wa nyumba  1615 za walimu ambao ni sawa na aslimia  87.5 ya mahitaji ya nyumba 1845  kwa ajili ya kuwawezesha walimu kuishi kwenye mazingira ya shule zao.
Ofisa elimu wa Wilaya ya Chato Ishengoma Kyaruzi alisema uhaba wa nyumba za walimu ni miongoni mwa maeneo ya vipaumbele vya halmashauri hiyo ambayo yanakwazwa na ukosefu wa raslimali ikiwamo fedha na ardhi.
Alisema  kuwa mbali na kutafuta ardhi, halmashauri ya wilaya hiyo ilikuwa inaandaa utaratibu wa kuwapata wawekezaji ambao watajenga nyumba na baadaye kuzipangisha kwa walimu kwa malipo nafuu.
Alidokeza mkakati huo wakati akitoa mada kwenye mdahalo ulionadaliwa na Asasi za Kiraia Mkoani Kagera kwa ubia na The Foundation for Civil Society kujadili changamoto za elimu.
Naye katibu wa Chama Cha Walimu wilayani Chato Victoria Laurent alisema kuwa kukosekana kwa nyumba za walimu kwenye maeneo ya shule kumeathiri viwango vya taaluma kwa kiasi kikubwa.
“ Tunaomba mamlaka kujenga mazingira mazuri ya kufundishia na kujifunzia ambayo bila kuwapo ndoto zakufikia malengo ya millennia zitakuwa zimeishia hewani” alisema Kiongozi huyo wa CWT.
 Alisema kutokana na walimu kuishi mbali na shule ilikuwa vigumu kuwahi ratiba za masomo sambamba na kushindwa kuzuia uharibifu wa mali na samani za shule unaotokea  baada ya saa za masomo.

Friday, August 10, 2012

Baada ya kumaliza vidato,anasubiri kwenda Chuo Kikuu

Kijana aliyemaliza kidato cha sita mwaka jana katika Shule ya Sekondari ya wavulana Rungwe iliyoko Tukuyu Mkoani Mbeya katika mchepuo wa Kemia,Biologia na Geografia(CBG)na kupata daraja la pili(Division II)Frolian Protace akichora bango la shule ya Sekondari Kaagya wilaya ya Bukoba Vijijini.


Thursday, August 9, 2012

Balozi Profesa Mahalu aibwaga Serikali mahakamani

Balozi Profesa Mahalu akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kushinda kesi yake katika mahakama ya Kisutu leo

Waandishi wa habari wakimfuata Balozi Profesa Mahalu akiwa pamoja na Mdogo wake Mirasi Rama wakitoka nje ya Mahakama ya Kisutu Mchana huu mara baada ya kushinda kesi iliyokuwa ikimkabili akidaiwa kununua nyumba ya Ubalozi wa Tanzania nchini Italia, Akisoma hukumu iliyosomwa kuanzia Saa sita leo na Hakimu Mfawidhi mkazi wa mahakama ya Kisutu Mh. Ilivin Mugeta imemtoa Balozi Profesa Mahalu katika hatia na kumwachia huru

Balozi Profesa Mahalu katikati akitoka nje ya mahaka ya Kisutu huku akiwa ameongozana na mdogo wake Mirasi Rama kulia ni Wakili wa kujitegemea Mabere Nyaucho Marando.

Aliyekua Balozi wa Tanzania nchini Italia,Balozi Costa Mahalu alikua mshitakiwa namba moja kwenye kesi ya matumizimabaya ya fedha za ununuzi wa jengo la ubalozi wa Tanzania nchini Italia, pamoja na mshitakiwa namba mbili Grace Martin  wameshinda leo baada ya  kuonekana hawana hatia yeyote baada ya kukosekana ushahidi wa kuwatia hatiaani.


CCM Kagera yawaonya wagombea

Katibu wa CCM Mkoa wa Kagera Avelin Moshi
Mgombea nafasi ya UVCCM ngazi ya Mkoa wa Kagera Yahya Kateme
Katibu wa UVCCM Mkoa wa Kagera Adia Rashid
Mgombea nafasi ya Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Kagera(aliyekaa katikati)Wilbroad Mutabuzi
Wapambe!
Hawa nao walikuwepo kushuhudia urejeshaji wa fomu za mgombea wanayemuunga mkono
Phinias Bashaya,Bukoba
CHAMA Cha Mapinduzi(CCM)Mkoani Kagera kimewaonya wagombea kupitia Jumuiya ya Umoja wa Vijana(UVCCM)dhidi ya uvunjaji wa kanuni za umoja huo kufuatia kuibuka kwa siasa za kupakana matope.

Akizungumzia zoezi la kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali ikiwemo nafasi ya Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa lililokamilika wiki iliyopita,Katibu wa chama hicho Mkoa wa Kagera Avelin Moshi alisema hawatasita kuwaengua wagombea watakaokiuka kanuni.

Alisema ni kinyume cha kanuni mgombea kuandaliwa vikao visivyo rasmi vya kukutana na wajumbe na kuwa hilo likiruhusiwa linaweza kuwanyima fursa ya kuchaguliwa wagombea ambao hawana uwezo wa kuwazungukia wajumbe.

“Vijana inabidi wawe na subira tunataka wapatikane viongozi wapya watakaokisaidia chama sio bora viongozi,mgombea atakayekusanya wajumbe jina lake litaondolewa hilo halihitaji kikao”alisema Mushi

Pia vuguvugu la uchaguzi ndani ya umoja huo linaonekana kuwagawa wenyeviti wa UVCCM ngazi za Wilaya ambao baadhi yao walijitokeza kupiga madai ya kumuunga mkono mgombea mmoja Yahya Kateme ambaye pia ni Mwenyekiti wa umoja huo wilaya ya Karagwe.

Wiki iliyopita wenyeviti wa wilaya za Muleba(Athumani Kahara)Ngara(Faris Mohamed) na Missenye(Revocatus Babeiya) walinukuliwa wakitangaza msimamo wa kumuunga mkono mgombea huyo wakati akirejesha fomu huku wakitaka wagombea wanaokimbilia mikoani uchaguzi unapofika kukataliwa.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Wilaya ya Bukoba Vijijini Prudence Kibuka na Chifu Kalumuna wa Bukoba Mjini waliueleza mtandao wa www.bukobapamoja.blogspot kuwa kauli za wenzao zilijaa ubaguzi na wao kutangaza kumuunga mkono Wilbrod Mutabuzi ambaye pia anawania nafasi hiyo.

Kwa mujibu wa Mutabuzi alisema huu sio wakati wa majigambo na kutafuta kuchafuana na kuwa hizo ni dalili za woga wa mpinzani wake na kutaka isubiliwe siku ya uamuzi wa wanachama wa umoja huo wakati wa uchaguzi.

Alisema uongozi wa chama unaanzia kwenye Jumuiya hiyo na kuwa hajakurupuka kuwania nafasi hiyo kwani ana uzoefu katika nyanja mbalimbali za uongozi  na uwezo mkubwa wa ubunifu wa miradi ianyoweza kuisaidia Jumuiya kujiendesha kwa mafanikio.

Mwenyekiti  anayemaliza muda wake Deusdedith Katwale hatetei tena nafasi yake ya Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa kwa kile alichodai kuwa ni kukabiliwa na majukumu mengine.Hata hivyo Wilaya anayotoka ya Chato ilimegwa kutoka Mkoa wa Kagera na kuwa sehemu ya Mkoa mpya wa Geita.

Wednesday, August 8, 2012

Wadau wa maendeleo Bukoba wakutana

Phinias Bashaya,Bukoba
 ASKOFU Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba Methodius Kilaini amewashauri wananchi wa Mkoa wa Kagera kubadilika na kutobweteka kuwa maendeleo katika Nyanja mbalimbali hayapatikani bila kuyatolea jasho.

Akichangia katika Mkutano wa wadau wa maendeleo ya Mji wa Bukoba uliofanyika katika ukumbi wa Mtakatifu Fransis alisema mtu anayetafu maendeleo hatakiwi kukata tama hata kama anakumbana na vikwazo mbalimbali katika juhudi zake.

Kiongozi huyo wa kiroho alihusisha kuduma kwa maendeleo ya mji huo na kile alichokiita kuwa ni siasa mfuniko zilizokwamisha mji huo na kupongeza jitihada mpya zinazofanyika kuuboresha na kuvutia shughuli  za kiuchumi.

“Miaka arobaini iliyopita tumekuwa na siasa mfuniko zilizofunika akili za watu,naunga mkono jitihada za kuuondoa na sasa tunatakiwa kusonga mbele,mji umeanza kupanuka na amendeleo lazima uyatolee jasho”alisema Kilaini

Katika Mkutano huo Meya wa Manispaa ya Bukoba Dokta Anatory Aman alisema utekelezaji wa miradi mbali iliyoidhinishwa na Manispaa inalenga kuongeza ajira na kuboresha taswira ya mji huo tofauti na mika mingi iliyopita.

Kwa mujibu wa  Dokta Aman miradi inayotarajiwa kutekelezwa ambayo pia imepata ufadhili ni pamoja na ujenzi wa soko jipya,kituo cha mabasi,jingo la kitega uchumi na upimaji wa viwanja elfu tano katika viunga vya mji wa Bukoba.

Pia Mkutano huo ambao idadi kubwa walikuwa viongozi wa Madhehebu ya dini walikubaliana kuwahamasisha waumini wao kupitia nyumba za ibada umuhimu wa kutunza na kuhifadhi mazingira kwa kila mwananchi kufanya usafi na kupanda miti.

Pia wadau hao walibainisha changamoto mbalimbali zinazoukabili mji wa Bukoba kuwa ni pamoja na ongezeko kubwa la watu lisiloendana na uboreshaji wa huduma kama miundombinu ya maji safi na maji taka.

Tuesday, August 7, 2012

Wanafunzi Rumuli wapinga uhamisho wa Mwalimu Mkuu

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Rumuli Manispaa ya Bukoba wakiandamana kuelekea Ofisi za Manispaa kupinga uhamisho wa Mwalimu mkuu
Wamefika Ofisi za Manispaa
Ofisa Elimu wa Manispaa ya Bukoba Edwin Fande akiwatuliza wanafunzi hao baada ya kufanya maandamano ya kupinga uhamishi wa Mwalimu wao Mkuu aliyepelekwa shule ya Msingi Buyekera
Sister Victoria Vicent aliyekuwa mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Rumuli ambaye amehamishiwa shule ya Msingi Buyekera ikiwa ni wiki moja baada ya Mahakama Kuu kitengo cha Kazi kusitisha mgomo wa walimu wa kudai masrahi zaidi ya kazi

Sunday, August 5, 2012

Mshauri wa mahakama mbaroni kwa ujambazi

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera SSP Peter Matagi akionyesha bunduki aina ya SMG baada ya kumkamata Mshauri wa Mhakama ya Mwanzo Lusahunga akiwa katika harakati za kwenda kufanya uhalifu.
MSHAURI wa mahakama ya Mwanzo Lusahunga wilayani Biharamulo Mkoani Kagera Enos Kazikie(43)amekamatwa na bunduki aina ya SMG na risasi 248 akiwa katika safari ya kwenda kufanya uhalifu.

Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera Peter Matagi mtuhumiwa huyo mkazi wa kijiji na Kata ya Nyakanazi alikamatwa tarehe 1,Agosti katika kitongoji cha Kabulaitoke akiwa ameweka silaha hiyo katika buti ya gari.

Alisema polisi wilayani humo walipata taarifa kuwa katika kijiji hicho kuna jambazi anamiliki silaha ndipo ufuatlijai ulipofanyika na mtuhumiwa kunaswa na bundiki na risasi hizo.

Alitaja namba za silaha hiyo kuwa ni SMG 4707,magazine moja na risasi 248 akisema kiasi cha risasi kilichokamatwa ni kikubwa nakama zingeendelea kumilikiwa na majambazi  zingehatarisha maisha ya wananchi na mali zao.

Pia Matagi amesema mbali na kuhusishwa na uhalifu mtuhumiwa huyo inaaminika alikuwa safarini kwenda kuuza siraha hiyo na kuwa msako wa kuwatafuta majambazi wengine waliokuwa wakishirikiana na mtuhumiwa unaendelea.

“Msako wa kuwatafuta majambazi wengine waliokuwa wanashirikiana na mtuhumiwa unaendelea,bunduki alikuwa ameiweka kwenye buti ya gari hata dreva wake gari hilo hakuwa na taarifa”alibainisha Matagi

Kufuatia tukio hilo Kaimu Kamanda Peter Matagi amewataka wananchi Mkoani Kagera kutoa taarifa kwenye vyombo vya usalama wanapotilia shaka mienendo ya baadhi ya wananchi wanaotuhumiwa kujihusisha na uhalifu.

Rugambwa Sec kujifua katika ndondi

Mwakilishi wa Wanawake Maendeleo ya Vijana na Ajira kwa wachezaji kutoka Shirikisho la Ndondi nchini(BFT)Zuwena Kipingu katika ziara ya kuhamasisha mchezo wa masumbwi shule ya sekondari ya wasichana Rugambwa nje kidogo ya Mji wa Bukoba