Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian Massawe |
Phinias Bashaya,Bukoba
KAMATI ya Ushauri ya Maendeleo ya Mkoa wa Kagera (RCC)imesitisha
mkataba wa ujenzi wa mradi wa jengo la
ofisi ya Mkuu wa Mkoa utakaogharimu zaidi ya shilingi bilioni kumi na moja na kuagiza yawepo mazungumzo na Serikali kutafuta njia nzuri ya kutekeleza
mradi huo.
Hatua hiyo ilifikiwa baada ya mjadara mkali wa wajumbe ambao
baadhi yao ilikiwemo kundi la wabunge wakidai mradi huo ambao hadi unasitishwa
ulikuwa umetumia zaidi ya bilioni moja kuwa ulikuwa ni mzigo kwa kuendelea
kuzalisha madeni.
Walisema kuwa pamoja na lengo zuri la kuwa na ofisi za Mkuu
wa Mkoa katika Kata ya Kahororo mradi huo ulikuwa hautekelezeki kwa sasa na
baadhi kushauri watafutwe wawekezaji watakaoweka vitega uchumi katika jengo
hilo lenye vymba tisini.
Mbunge wa Bukoba Vijijini Jasson Rweikiza alisema Mkoa hauna
uwezo wa kuendeleza mradi huo akidai uamuzi haukuwa sahihi,huku Mbunge wa
Nkenge Ansupter Mshama akipendekeza jengo hilo litumike kwa shughuli za utalii.
“Mlianza vyema lakini huu sio wakati unaofaa kuwa na mradi wa
ofisi ya Mkuu wa Mkoa yenye vyumba tisini,tulifanye jengo la utalii wananchi
hawawezi kuchangia jengo wakati huo ukawataka wachangie zahanati”alisema Mshama
Hata hivyo kundi jingine la wajumbe miongoni mwao akiwa
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Kashunju Runyogote walitetea
ujenzi wa mradi huo ingawa changamoto ilikuwa ni tatizo la upatikanaji wa fedha
usiokwenda na mipango ya utekelezaji.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Nassoro Mnambila aliwaeleza
wajumbe wa kikao hicho kuwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali iliutaka Mkoa
utafakari tena kama kuna umuhimu wa kuendelea na mradi huo ilhali Serikali
ikiwa inasuasua kutoa fedha za ujenzi wa ofisi hiyo.
Naye Mwenyekiti wa kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali
Mstaafu Fabian Massawe alisema wataendelea kufanya mazungumzo na Serikali
kushauriana jinsi ya utekelezaji wa Mradi huo na taarifa itawasilishwa katika
kikao kijacho.
No comments:
Post a Comment