Phinias Bashaya
PAMOJA na ushindi wa majeshi ya
Tanzania wakati wa vita ya kumng’oa Idd Amin aliyekuwa Dikteta wa Uganda wapo
wananchi wenye kumbukumbu mbaya zilizotokana na athari za mapambano.
Kwamba vita haina macho,hukumba kila
mtu bila kujali kama yuko mstali wa mbele katika uwanja wa mapambano au
amejificha uvunguni kwa hofu ya mirindimo ya risasi na milipuko ya mabomu.
Vita ya Tanzania na Uganda maarufu
kama “Vita ya Kagera”iliyotokea mwaka 1978 hadi 1979 iliacha athari kubwa
za kiuchumi na kijamii hususani kwa wakazi wa Mkoa huo na baadhi ya
wananchi hata baada ya miaka 33 ya vita bado wana makovu moyoni.
Ndivyo ilivyotokea kwa Protase
Nshombo mkazi wa kijiji cha Buhanga Kata ya Bujugo Wilaya ya Bukoba
Vijijini.Alionja udhalimu wa Idd Amin na majeshi yake baada ya watoto wake
watano na wake watatu kuchinjwa hadharani.
Anasema wakati wa vita familia yake
ilivamiwa akiwa safari katika jiji la Nairobi nchini Kenya na baada ya kupewa
taarifa aliruka kwa ndege hadi jijini Kampala.
“Wakati familia inavamiwa nilikuwa
Nairobi nilikuta wameuwa watoto wangu watano na wake watatu eti hawataki
kumuona Mtanzania yeyote katika nchi yao”anasema Nshombo
Anabainisha kuwa wakati huo
alijaliwa watoto saba kutoka kwa wake sita aliokuwa nao ambao wote
walishirikiana kuendesha mradi wa kupika pombe ya moshi maarufu nchini humo kwa
jina la Waragi.
Baada ya kufika na kushuhudia unyama
aliotendewa na majeshi ya Amin naye alikamatwa na kupewa mateso ikiwa ni pamoja
na kupakwa kinyesi na kucharazwa viboko.
Watoto wote waliouawa walikuwa
wavulana na wanawake watatu walionusurika pamoja na mabinti wawili walikimbia
baada ya kushuhudia wenzao wakifanyiwa unyama.
Kwamba aliishi katika mtaa wa Jinja
na alinusurika kifo baada ya kutoroshwa na mwanamke aliyemkumbuka kwa jina moja
la Rooza aliyemficha katika kijiji cha Bukedi kilichopo mpakani mwa nchi hiyo
na Kenya.
Mwanamke huyo alijawa na huruma
baada ya kumkumbuka kuwa waliwahi kufanya kazi wote katika ofisi ya Kabaka na
alimpeleka katika kijiji chao ili kumnusuru na kifo.
Akumbuka utajiri wake
Mradi wake ulimwezesha kujipatia
pato kubwa hata kuwa mtu maarufu katika jiji la Kampala akimiliki magari
sita,mashamba na nyumba za kupangisha.
Hakuwa na hofu ya kushindwa kutosheleza
mahitaji ya familia yake kwani alimiliki miradi mingi iliyompatia pato kubwa na
hata kuwa miongoni mwa wafanyabiashara maarufu.
Hata hivyo wakati wa vita hiyo
pamoja na kusambaratishwa kwa familia yake pia hakuna mali aliyookoa zaidi ya
mashamba machache aliyokuwa ameyanunua nje ya mji.
“Mali za pembeni ndizo zilizopona
watoto waliobaki walikimbilia ujombani nchi humo mimi nikaendelea na maisha
nikiwa mafichoni”anabainisha
Anasema wake wake sita walikuwa wa
Kabila la Wasoga na anakumbuka vurugu mauaji,uporaji na vitisho vilivyokuwa
vikifanywa na wanajeshi wa Amin.
Safari ya Uganda
Mwaka 1962 damu ya ujana ilimsukuma
Protase Nshombo kwenda kutafuta maisha katika jiji la Kampala na kufanikiwa
kujiunga na vijana wengine katika kazi za kibarua.
Lengo ilikuwa ni kukusanya fedha
zitakazomwezesha kurudi kijijini na kuoa hasa baada ya kununua kitanda cha
‘vono’ ambacho kilikuwa ni fasheni ya vijana wa enzi zake.
Anasema akiwa jijini Kampala alishawishiwa
na familia moja iliyotaka wakaishi wote na kukuta katika familia hiyo kuna
watoto waliokuwa wakisoma shule.
“Waligundua kuwa nilikuwa na akili
wakamua kunipeleka chuo cha ufundi Kyambogo na kusomea fani ya ujenzi baada ya
miezi sita nilihitimu na kupata kazi”
Anasema uwezo mkubwa aliokuwa nao
katika shughuli za ujenzi ulimwezesha kuajiliwa katika maeneo mbalimbali na
hata kusafiri kwenda jijini Nairobi kama mwangalizi wa miradi ya ujenzi.
Kazi yake aliifanya kwa uaminifu
mkubwa huku akisafiri miji mbalimbali ndani ya nchi.Pato lake liliongezeka na
hata kuanzisha miradi mbalimbali ya biashara zikiwemo nyumba za kupangisha.
Hata hivyo baada ya maisha kumnyokea
alifutilia mbali wazo lake la awali la kupata fedha za kuoa na kurudi
nyumbani badala yake kuamua kuishi katika jiji la Kampala.
Kurejea nyumbani
Baada ya kuishi mafichoni Protase
Nshombo mwaka 1992 aliamua kurejea nyumbani akiongozana na mke na watoto
wawili,aliowapata baada ya mauaji ya familia yake.
Hata hivyo haikuwa kazi rahisi kwani
anasema njiani alikumbana na matatizo mengi ikiwemo kunyang’anywa mizigo yake
yote na hivyo kurejea kijijini bila kitu.
Anasema kijiji kilipatwa na mshituko
baada ya kupata taarifa za kurejea kwake kwani hata baba yake aliwahi kwenda
kumtafuta nchini Uganda na hakufanikiwa kumpata.
Anasema baba yake aliwahi kupata
taarifa kuwa mtoto wake alikuwa anafanya kazi kwa Kabaka,na kuwa hata hivyo
baada ya kufunga safari ya kumfuata hakuweza kumkuta.
“Nilirudi nyumbani bila kitu
nilikuta wazazi wangu wote wakiwa hai nilifanyiwa sherehe kwa wiki nzima mimi
ndiye mtoto wa kwanza katika familia yetu”anabainisha
Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Kijiji
hicho Simon Kyakaraba anakumbuka jinsi Protase Nshombo alivyopotea kwa muda
mrefu na hata yeye ni shahidi katika migogoro iliyoibuka baada ya kurejea
kwake.
Ni wakati huo alipofananishwa na
kondoo aliyepotea na kuifanya familia ilipuke kwa furaha kwani hakuna
aliyeamini kuwa alikuwa bado hai.
Mateso uzeeni
Baada ya kifo cha baba yake mwaka
1998 ilianza misukosuko katika familia huku akiwatuhumu baadhi ya ndugu zake
kuandaa mipango ya kumnyang’anya mashamba.
“Wanaona mimi ni mnyonge sina fedha
na sehemu ya kukimbilia walianza kuninyang’anya mashamba hawakutaka nione hata
wosia tulioachiwa”anabainisha.
Hivi sasa familia ina maisha ya
kubahatisha pamoja na kudai baba yao alikuwa na mashamba mengi na kuwa
haridhiki na mgawanyo wa mali ulivyokwenda.
Hakukaa kimya,amejaribu kutetea haki
yake katika ngazi ya kijiji na Baraza la ardhi la Kata ya Bujugo na mara zote
amegonga mwamba huku walalamikiwa wakiibuka washindi.
Hata shauri la madai namba 14/2006
lililofunguliwa katika Baraza la Ardhi Bujugo bado matokeo ya hukumu yalizidi
kuididimiza zaidi familia hiyo.
Wajumbe wanne wa Baraza hilo chini
ya Mwenyekiti wao Levelian Rwabyo waliona ushahidi uliotolewa unatosha
Protase Nshombo kustahili kunyang’anywa sehemu ya shamba.
Watoto wao Theofilda na Samwel ambao
ni wanafunzi wa shule ya msingi Katoju mara nyingi hukatisha masomo ili
kupeleka mawese katika magulio mbalimbali.
Historia ya vita ya Kagera
Nduli Iddi Amin alitwaa madaraka ya
nchi yake kwa mabavu mwaka 1971,na mwaka 1978 jeuri ikamtuma kuyaamuru
majeshi yake kuivamia ardhi ya Tanzania upande wa Mkoa wa Kagera.
Wakati huo ulikuwa ni Mkoa wa Ziwa
Magharibi ambapo majeshi yake yaliua wananchi na kupora mali huku Amin
akijitapa kuwa siku sio nyingi angechakaza hadi jijini Dar es salaam.
Alibomoa daraja la Kyaka Wilayani
Missenye na hata kusambaratisha kanisa ambalo kumbukumbu yake ipo hadi leo
katika eneo la Kyaka wilayani humo.
Tunayo kazi moja nayo ni
kumpiga.Uwezo wa kumpiga tunao,nguvu za kumpiga tunazo na nia ya kumpiga
tunayo.Maneno hayo ya aliyekuwa Amiri Jeshi Mkuu Mwalimu Julius Nyerere
yaliitikiwa kwa vitendo na wanajeshi wa Tanzania.
Hiki kilikuwa ni kipindi cha miezi
kumi na nane cha kuondoa majeshi ya uvamizi na kuzima ndoto ya Iddi Amin ya
kujitwalia ardhi akitaka kuhalalisha mauaji ya wananchi.
Majeshi yetu yalipokewa kwa shangwe
katika ardhi ya Uganda,mvamizi alifanikiwa kutoroka.Mashujaa wetu walishiriki
kufungua ukurasa mpya kwa wananchi wa Uganda baada ya miaka mingi ya mateso ya
Nduli Iddi Amin.
Vita ilikuwa imekwisha.Luteni
Jenerali Silas Mayunga na mashujaa wenzake walipokewa kwa shangwe pale Bunazi
Wilayani Missenye.Sanamu ya Mayunga katika mji wa Bukoba ni kumbukumbu ya
shujaa anayestahili kuenziwa na vitabu vya historia ya taifa hili.
Mwisho
No comments:
Post a Comment