Naibu Waziri wa Uchukuzi Dk Charles Tizeba akitoa ufafanuzi wa jambo linaloihusu Wizara yake katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera |
Dk Tizeba akisalimiana na baadhi ya Maofisa waliofika kumpokea katika uwanja wa ndege Bukoba |
Baadhi ya wageni walioambatana na Waziri Tizeba wakiwa katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera |
Phinias Bashaya,Bukoba
NAIBU Waziri wa Uchukuzi Dokta
Charles Tizeba ameshangazwa na hali inayowakabili abiria wa mikoa ya Tabora na Kigoma ambao
hulazimika kulala kwenye sakafu ya kokoto wakati wakisubiri usafiri wa treni.
Alionyesha kukerwa na hali hiyo
alipokuwa katika ziara yake mjini Bukoba mapema wiki hii wakati akizungumzia
uchakavu wa miundombinu ya reli na kulaumu
wahusika kupuuzia suala la ujenzi wa maeneo ya kupumzikia abiria.
“Nilishanga abiria wa Tabora na
Kigoma kulala kwenye sakafu ya kokoto wanaposubiri usafiri wa treni,huwezi
kuamini kuwa hawa ndio abiria wa Kitanzania wa mwaka 2012”alilalama Tizeba
Alihoji iweje Shirika la Reli(TRA)lishindwe kuboresha maeneo ya
kupumzikia abiria na kuwa kwa kushindwa kufanya hivyo baadhi ya abiria hukwepa
kutumia huduma za usafiri zinazotolewa na shirika hilo.
Pia Waziri Dokta Charles Tizeba alisema
kuwa wananchi wanalazimika kutumia usafiri wa mabasi kwa sababu meli na treni havitoe huduma zinazoridhisha,
huku akiubeza usafiri wa mabasi na kuufananisha na majeneza yanayotembea.
Aidha alikagua maeneo mbalimbali
yaliyopo chini ya Wizara yake ikiwa ni pamoja na uwanja wa ndege wa Bukoba,eneo
la Omukajunguti unapotarajiwa kujengwa uwanja wa ndege wa Kimataifa Wilayani Missenye
na bandari za Kemondo na Bukoba.
Akizungumzia hali mbaya ya vyombo
vya usafiri majini alisema abiria wanakerwa na hali ya uchafu wa meli
zinazosafiri ndani ya Ziwa Victoria na
kuwa abiria wanakimbilia usafiri mwingine kukwepa hali inayowafanya waonekane
kama walioko mahabusu.
Kuhusu Meli ya Mv Lihemba
inayofanya kazi Ziwa Tanganyika alisema itafanyiwa ukarabati mkubwa na
Ujerumani.Meli ya Mv Lihemba inatajwa kuwa kongwe zaidi duniani ikiwa na umri wa miaka mia moja ambayo tangu
mwaka 1913 inaendelea kufanya kazi za kusafirisha abiria na mizigo.
No comments:
Post a Comment