Wednesday, June 6, 2012

UMISSETA Kagera wako tayari

Mkuu wa Wilaya ya Muleba Limbres Kipuyo akikagua Timu za Mpira Tayari kwa mashindano ya UMISSETA Mkoa wa Kagera.Picha na Silvester Raphael-PR ofisi ya Mkuu wa Mkoa

RC Kagera atangaza kiama cha wahamiaji haramu

Ng'ombe wa wafugaji wanaohusishwa na uhamiaji haramu wakiwa katika malisho Wilayani Karagwe
Aina ya ng'ombe wanaofugwa Mkoa wa Kagera
MKUU wa Mkoa wa Kagera kanali mstaafu Fabian Massawe amesema wakati wowote itafanyika oparesheni kubwa ya kuwaondoa wahamiaji haramu katika wilaya zote aliosema ni tishio kubwa la usalama wa nchi.

Akizungumza juzi katika kikao cha Kamati ya ushauri ya Mkoa(RCC)kanali Massawe alisema zoezi hilo litavihusisha vikosi mbalimbali vya ulinzi na usalama na kuwaonya wenyeji watakaowahifadhi wahamiaji hao.

Kwa mujibu wa Massawe Mkoa wa Kagera una jumla ya wahamiaji haramu 35,000 aliodai wanafahamika kwa majina wakiwemo wafugaji na kuwa makundi hayo ni tishio kubwa la usalama wa mkoa na taifa.

"kuna wahamiaji haramu elfu thelathini na tano tunaowafahamu kwa majina na sehemu walipojificha,oparesheni kubwa ya kuwaondoa itaanza wakati wowote kwani ni tishio kubwa la usalama"alisema Massawe.

Aidha Massawe alisema kuwa tayari mkoa umeomba kiasi cha shilingi milioni mia sita kwa ajili ya oparesheni hiyo na kuwa kufumbia macho suala la wahamiaji haramu unaweza kuwa mwanzo wa kukaribisha makundi ya waasi kutoka nchi jirani na kujificha katika nchi yetu.

Hata hivyo Mkuu wa Mkoa wa Kagera kanali mstaafu Fabian Massawe alionyesha wasi wasi wa kuwadhibiti wahamiaji hao wasirudi tena baada ya kubainika kuwa baadhi ya wananchi wanahusika na kuwahifadhi wahamiaji hao.

Friday, June 1, 2012

JK ahusishwa kwenye mgogoro wa shule wilayani Muleba

MGOGORO wa mmiliki halali wa shule ya sekondari Katoke wilayani Muleba kati ya Mbunge wa zamani wa Muleba Kaskazini Ruth Msafiri na wananchi umechukua sura mpya baada ya madiwani  kudai kuwa Rais Jakaya Kikwete alitoa mchango wa mabati kuunga mkono juhudi za wananchi.

Kufuatia kuendelea kufukuta kwa mgogoro huo Kamati ya elimu,afya na maji kupitia kwa mwenyekiti wake Geofrey Samson imewasilisha ushahidi wake mbele ya Baraza la Madiwani wa Wilaya hiyo kuthibitisha kuwa sekondari hiyo sio mali binafsi ya Ruth Msafiri.

Katika ushahidi huo kamati hiyo katika baraza la madiwani lililofanyika juzi ilisema kuwa Rais Jkaya Kikwete alitoa mchango wa mabati 350 baada ya kuelezwa kuwa ilikuwa shule ya sekondari ya kata ya Katoke.

Kwa mujibu wa Geofrey Rais Kikwete aliitikia kilio cha wananchi wakati amefika Wilayani humo kuhudhuria sherehe za siku ya Mashujaa zilizofanyika miaka mitatu iliyopita na kuhaidi kutoa mchango wa mabati kusaidia kukamilika kwa ujenzi wa shule hiyo.

Pia ushahidi mwingine uliowasilishwa na kamati hiyo ni jinsi vyanzo mbalimbali vya mapato ikiwemo fedha ya mfuko wa maendeleo ya Jimbo milioni 13,harambee iliyochangiwa na wadau mbalimbali ikiwemo Benki ya NMB tawi la Muleba shilingi milioni tano na Wizara ya Maliasili na Utalii milioni sita.

"Shule ya sekondari ya Kata ya Katoke ijulikanayo kama sekondari ya Ruth Msafiri ilianzishwa kama shule ya sekondari ya kata chini ya ufadhili wa vyanzo mbalimbali ikiwemo fedha ya mfuko wa maendeleo ya jimbo"anasema sehemu ya taarifa ya Kamati hiyo.

Kwa mujibu wa Kamati hiyo Ruth Msafiri alianza kudai shule hiyo ni mali yake binafsi baada ya muda wake wa Ubunge kumalizika na kutochaguliwa tena na kuwa tangu wakati huo ushirikishwaji wa kamati ya ujenzi ulikoma pamoja na kuwa uanzishwaji wa shule hiyo ulipitia vikao mbalimbali katika ngazi ya kijiji na kata.

Katika Baraza hilo msemaji wa kambi ya upinzani Julius Rwakyendera alisema ushahidi uliotolewa unathibitisha kuwa shule ya sekondari ya Katoke ni mali halali ya wananchi na kuwa inasikitisha mtu aliyewahi kupewa dhamana ya uongozi na wananchi kuonyesha kuwa sio mwamnifu.

Pia katika mchango wa ushahidi uliotolewa na Kamati ya elimu.afya na maji Diwani wa Kata ya Muleba Mjini Hassan Milanga(CUF) alishangaa ukimya wa Serikali katika mgogoro huo na kuwa kama suala hilo lingemhusisha yeyote kutoka kambi ya upinzani angekuwa tayari amefikishwa mahakamani.

Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Msaafu Fabian Massawe alifanya ziara katika Kata ya Katoke ambapo Ofisa Mtendaji wa Kata hiyo Faustine Rweyemamu alisema shule hiyo sio mali binafsi ya Ruth Msafiri kwani February,28,2009 serikali ya kijiji cha Katoke iliitisha kikao cha dharula chini ya Ruth na kuamua kutenga ekali 20 kwa ajili ya ujenzi wa sekondari.

Kwa mujibu wa Ofisa huyo  kuanzia wakati huo harakati za michango ya ujenzi zilianza ambapo Ruth Msafiri alikuwa msimamaizi mkuu akisaidiana na kamati ya ujenzi iliyochaguliwa.

Tuesday, May 29, 2012

Vijana wa Bukoba wamvaa Nape

TAMKO LA VIJANA WA BUKOBA MJINI WAISHIO DAR ES SALAAM

Ujio wa Nape: Kagera Tumedharauliwa na Uzalendo Umedhihakiwa

Tumejaribu kutafakari  kwa kina juu ya nini hasa kilimsukuma Nape kufika Kagera na kushiriki mazishi ya muasisi wa TAA, mzalendo na mpigania uhuru aliyetelekezwa na Taifa lake, Dr. Vedasto Kyaruzi  na bado ki-ukweli hatujapata majibu.

Tunapata shida kujua dhima ya safari ya Nape kwa kuwa shughuli hasa alizozifanya akiwa Kagera zina kinzana kimaadili na kitamaduni na maombolezo ya misiba ya Kiafrika na hasa misiba ya Kihaya.

Mjumbe aliyetumwa mahsusi toka mbali kupeleka pole kwenye msiba hategemewi atumie muda wake mwingi majukwaani kufanya siasa, tena katika mazingira ya ugenini. Lakini mpita njia ambaye amefahamishwa tukio na akahiari kufika msibani, akiendelea na shughuli zake si ajabu hata kidogo.

Nape aliingia Bukoba tarehe 25/05/2012. Na ni uungwana kukiri kuwa alifika Kashai-Matopeni msibani kutoa salamu za pole.  Lakini baada ya hapo alielekea Missenyi ambako tunaarifiwa alikuwa na mikutano ya hadhara.

Watanzania mtakumbuka vema kuwa katika mikutano hiyo ndiko Nape alitoa kauli ya kutokuwa tayari kukabidhi nchi kwa wahuni! Labda ili Watanzania muweze kupima vema uelewa na akili za Nape, tuwafahamishe kuwa Missenyi ndiko iliko Kyaka na ambako maziko ya Dr. Kyaruzi yamefanyika.

Tunashindwa kuelewa, hiyo mikutano ilikuwa safisha njia ya mazishi au inahusiana vipi na mtu aliyepeleka ujumbe wa maombolezo?

Linalochanganya zaidi ni hili la Jumamosi tarehe 26/05/2012. Hii ndiyo siku ambayo Dr. Kyaruzi alipumzishwa rasmi kaburini alale kwa amani. Lakini kwa Nape akiwa Kyaka hii ilikuwa siku maalumu ya kutangaza operation yake mpya ya kisiasa “Vua Gamba, vua Gwanda, Vaa Uzalendo”.

Katika hili, ukiachilia ukinzani wa matukio kimaadili na kitamaduni, tunapata mishangao mingine; hivi Nape alikwenda Kyaka kuzika au kuzindua operation ya kisiasa? Na Je, huyu kijana anahubiri uzalendo upi? usiokuwa na utamaduni, Uzalendo wa kuwatelekeza na kushindwa kuwaenzi watu waliopigania uhuru wa nchi hii?

Kama huo ndiyo uzalendo anaohubiri Nape, basi hauhitaji operation wala kampeni maana tayari tunao magwiji. Na hapo kwa tafsiri hii, ujio wake na matukio yake kwenye maeneo ya msiba vinanapata maana halisi.

Katika Taarifa ya Uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki,  Chama Tawala kimearifiwa kuwa moja ya kosa lililofanyika ni kumteua mgombea ambaye mila hazikuwa zinampa fursa na tafsiri njema kufanya shughuli kama ya siasa  katika muda mfupi baada ya msiba wa Baba yake.

Ikiwa kosa hili la Kitamaduni limechangia Chama kupoteza Jimbo, basi pia chama kiwe tayari kwa makosa ya Nape kupoteza zaidi zaidi ya Kijiji cha Burifani na Kata nzima ya kyaka. Na hatutoshangaa iwapo Nape au Taasisi iliyomtuma ikishindwa kuomba radhi!

Mbali na vioja vya Nape hapo juu, kwa wasifu wa marehemu Dr. Kyaruzi, kila mmoja atakubaliana nasi kuwa Taasisi yoyote (iwe dola au chama) kuwakilishwa na mtu wa ngazi ya Nape ni dharau ya hali ya juu na ichukuliwe ni dhihaka si kwa jamii iliyostaharabika tu, bali hata kwa watu walipendao Taifa lao na kuuenzi Uzalendo. Inakuwa vigumu kuamini kuwa pamoja na ugumu wa ratiba, Rais alikosa muwakilishi makini wa hadhi inayobeba uzito sawia na mchango wa Dr. Kyaruzi katika Taifa hili.

Tukio hili linaleta hisia za ubaguzi wa Taasisi za dola na chama katika kutoa uzito kwenye majanga, matatizo na misiba ya watu wa Taifa hili. Ni majuzi tu Taifa lilipotelewa na Mcheza Sinema nguli ambaye hapo awali hakuwahi kupata heshima yoyote ya Kitaifa.

Lakini tuliona jinsi viongozi wa Serikali na Chama walivyohamia msibani na Serikali kujipa jukumu la kuubeba msiba na shughuli za maziko. Haikupita muda, Rais akiwa ziarani Marekani, Rais wa Malawi alifariki duniani. Pamoja na uchovu wa safari tulimwona Rais akiingia nchini na kutoka kuwahi mazishi ya Rais wa nchi jirani.

Kulingana na umuhimu wa msiba huu, Rais hakusubiri hata atatue matatizo makubwa yaliyokuwa yanaikabili serikali yake kiasi cha kutishiwa kuanguka. Lakini pia ni kawaida kusoma taarifa za Rais anazoandika katika mitandao ya kijamii kila anapokuwa njiani kuelekea kwenye misiba ya watu wa kawaida walioko katika maeneo mbalimbali Jijini Dar es Salaam. 

Hili linatuongezea huzuni na kutuongoza kuamini kuwa misiba ya watu wa maeneo nje na Dar es Salaam haigusi hisia za Rais hata kama ni ya Watu waliotoa mchango mkubwa kwa Taifa hili.

Haya yaliyotokea kwa Dr. Kyaruzi alimanusura yatokee pia kwenye msiba wa MKUU wa Majeshi Mstaafu Jenerali  Ernest Mwita Kyaro. Huyu alikufa siku chache baada ya mazishi ya Kanumba na msiba wake ulikosa sura ya Kitaifa. Isingekuwa kelele za wana-Mitandao ya Kijamii (MyKj) na wahandishi wa habari, hata Bunge lisingesimama kwa dakika moja kutoa salamu.

Tabia hii ya kutelekeza wazalendo wa Taifa hili inaonekana kumea kwa kasi. Na uthaminisho wa serikali kwa watu wa Dar es Salaam unaonekana kuwa juu kuliko wa wale walioko nje ya Dar es Salaam.

Kwa Tamko hili tunamtaka Nape Nnauye, Katibu Mwenezi wa CCM kama kweli alikuja kuwakilisha Taasisi yoyote katika msiba wa Dr. Kyaruzi, basi aiombe radhi jamii yetu kwa dharau kubwa aliyoonyesha katika msiba huu. Na kama alikuwa mpita njia tu, basi atujuze ili Jamii na historia ya Taifa imwandike rasmi Dr. Kyaruzi kama muasisi wa TAA na mzalendo aliyepigania uhuru wa Taifa lake ambaye hakuenziwa wakati wa uhai wake na hata mazishi yake hayakuhudhuriwa na mwakilishi wa Kitaifa.

Na mwisho tunamtaka Rais wa Jamhuri ya Tanzania kama Taasisi awe Rais wa Watanzania wote; wa Dar es Salaam na Mikoani.


Asiye na utamaduni ni mtumwa. Tanzania ni moja

Imetolewa na:
Erick Mwemezi Kimasha
Mhamasishaji Jamii Mkuu
Vijana wa Bukoba Mjini Waishio Dar es Salaam

Barua Pepe:       ekimasha@ksgroup.co.tz
Simu:           0713-177-372

Monday, May 28, 2012

Cheo ni Dhamana

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Samwel Kamote(kushoto)na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi Omary Nundu(mwenye miwani kifuani) siku walipotembelea Bandari ya Kemondo,anayetoa maelezo ni Meneja wa bandari hiyo Bwana Minja

Madiwani wa Missenyi watimuliwa kwenye majengo ya Saccos


Aliyewahi kuwa Mbunge wa Nkenge Balozi Dkt Diodorus Kamala akizindua Chama cha Kuweka na Kukopa (Saccos)katika Kata ya Buyango ambapo wakati wa kipindi chake alijenga majengo ya Ofisi hizo kwa kila Kata.Picha hii ilipigwa mwaka jana
CHAMA Cha Mapinduzi(CCM)kimewataka madiwani wa Wilaya ya Missenyi Mkoani Kagera wanaotumia majengo ya vyama vya kuweka na kukopa(Saccos)kama ofisi zao kuondoka katika majengo hayo.

Agizo hilo lilitolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho Nape Nnauye siku ya Ijumaa baada ya kupokea malalamiko ya Umoja wa Vijana wa chama hicho(UVCCM)waliodai baadhi ya madiwani wamegeuza majengo ya Saccos kwa ajili ya matumizi ya ofisi zao.
Nape alikuwa Wilayani humo kufungua Baraza la vijana wa UVCCM ambalo pia lilihudhuriwa na wanachama wa chama hicho na viongozi mbalimbali huku kukiwa na mwitikio mdogo wa vijana.
Nape aliwataka madiwani hao kujenga ofisi zao na kuwa wanatakiwa kuondoka katika majengo hayo na kuwa wasisubiri vijana waendelee kulalamikia suala hilo linaloathiri ukuaji wa vyama hivyo.
"Madiwani jengeni ofisi zenu acheni zifanye kazi ya Saccos,kama madiwani mliweza kushawishi wapiga kura wakawachagua tushawishi pia tukujengee ofisi"alisema Nape
Aidha Nape alisema endapo madiwani hao wataendelea kutumia majengo ya Saccos kama ofisi zao wanaweza pia kuhatarisha ukuaji  na lengo zuri la kuanzisha wa vyama hivyo vya kuweka na kukopa.
Awali Katibu wa UVCCM Wilayani Missenyi Philbert Ngemera katika taarifa yake kwa Nape alisema majengo ya Saccos yalioyengwa kila Kata na aliyekuwa mbunge wa Jimbo hilo Dk Diodorus Kamara yametekwa na baadhi ya madiwani na kuzifanya kuwa ofisi zao.
Pia alihainisha changamoto mbalimbali zinazowakabiri vijana  kuwa ni pamoja na upandaji holela wa bidhaa na vijana kukimbia chama hicho kwa madai ya kutowajali huku wakiendelea kuwa na maisha magumu.
Aidha alisema katika baadhi ya maeneo wamekosa vijana wakujitokeza kugombea uongozi kwa kile alichodai ni wengi wao kukosa sifa na kuwa hadi sasa vijana 178 wamekimbia chama hicho na kuhamia Chadema idadi aliyosema ni ndogo ikilinganishwa na vijana wengi wanaoendelea kuiunga mkono CCM.
Kaatika hotuba yake pia Nape aliwaeleza vijana kuwa wana nafasi ya kuchagua viongozi wanaofaa kukiimarisha chama na kuwa wasikubari kurubuniwa hasa katika kipindi hikia mbacho CCM inaendelea na uchaguzi wa ndani.
Mbali na kusema kuwa mageuzi ni lazima ndani ya chama hicho ili kuendana na wakati pia alisema hata wakuu wa Wilaya walioteuliwa hivi karibuni chama kimewaeleza wasifanye mchezo katika maeneo yao kwani nyumbani kwao ni CCM.
Kwa mujibu wa Nape wakuu hao wa wilaya wanatakiwa kufanya kazi kwa masirahi ya chama na kuongeza kuwa ikitokea chama kingine kinachukua dola nacho kinachagua viongozi wake.