Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera Henry Salewi ambaye anastaafu na nafasi yake kuchukuliwa na aliyekuwa Ofisa wa Opareshini Mkoa wa Mwanza, ACP Philipo Kalangia
|
Wiki chache baada ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Said Mwema kupanga upya safu ya makamanda wa Polis wa Mikoa,watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wamerusha bomu na kuwaua wananchi wawili katika kijiji cha Kumwendo Kata ya Mbula Wilayani Ngara.
Katika mabadiliko yaliyofanywa na IGP Mwema aliyekuwa Ofisa wa Oparesheni Mkoa wa Mwanza ACP Philipo Kalangia ndiye Kamanda mpya wa Polisi Mkoa wa Kagera akichukua nafasi ya Henry Salewi ambaye anastaafu.
Hata hivyo Kamanda Salewi ambaye anamaliza muda wake amekanusha tukio hilo kuhusishwa na ujambazi na kuwa watu wasiofahamika ndiyo walirusha bomu katika kijiji hicho na kuua wananchi wawili na wengine watano kujeruhiwa.
Kamanda Henry Salewi alisema kuwa uchunguzi wa awali umeonesha kuwa waliohusika na tukio hilo sio majambazi kama inavyosemekana na kuwa baada ya tukio walikimbia na hawakuchukua kitu chochote.
Kamanda Salewi alisema kuwa tukio hilo lilitokea Mei 13 mwaka huu saa 3:00 usiku wakati watu hao wakiwa mbele ya nyumba moja ambao inadaiwa walikuwa wakitoka kuangalia televisheni kwenye nyumba hiyo.
Alisema kuwa katika tukio hilo watu wawili walikufa papo kwa papo ambao ni Felista William (57) mkazi wa kijiji Kumwendo na Antiba Adrian (14) mkazi wa kijiji Murugalama, na kuwa bomu hilo lilidondokea mlangoni na kulipuka.
Aliwataja watu watano waliojeruhiwa katika tukio hilo kuwa ni Anathoria John aliyejeruhiwa shavu la kushoto, Angelina Benard (29) aliyejeruhiwa paja la mguu wa kushoto na Anna William (28) aliyejeruhiwa tumboni.
Wengine waliojeruhiwa ni Dickson Matoni (28) aliyejeruhiwa paja la kulia na Ndaishimiye Daniel (17) ambaye alijeruhiwa tumboni, wote wakazi wa kijiji Kumwendo.
Kamanda Salewi alisema mama aliyeuawa na bomu hilo (Felista) pia mtoto wake aliuawa kwa kurushiwa bomu katika kipindi cha takriban miaka miwili iliyopita, hali inayoleta wasiwasi kuwa huenda kuna mambo yaliyojificha.
Alisema watu wanne waliojeruhiwa wamelazwa katika hospitali teule ya wilaya ya Ngara ya Murgwanza kwa matibabu, ambapo mtu mmoja Ndaishimiye Daniel alitibiwa na kuruhusiwa.
Amewataka wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha utakaowezesha kukamatwa kwa watu waliohusika na tukio hilo ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.
No comments:
Post a Comment