|
Katibu wa CCM Mkoa wa Kagera Avelin Moshi |
|
Mgombea nafasi ya UVCCM ngazi ya Mkoa wa Kagera Yahya Kateme |
|
Katibu wa UVCCM Mkoa wa Kagera Adia Rashid |
|
Mgombea nafasi ya Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Kagera(aliyekaa katikati)Wilbroad Mutabuzi |
|
Wapambe! |
|
Hawa nao walikuwepo kushuhudia urejeshaji wa fomu za mgombea wanayemuunga mkono |
Phinias Bashaya,Bukoba
CHAMA Cha Mapinduzi(CCM)Mkoani Kagera kimewaonya wagombea kupitia
Jumuiya ya Umoja wa Vijana(UVCCM)dhidi ya uvunjaji wa kanuni za umoja huo
kufuatia kuibuka kwa siasa za kupakana matope.
Akizungumzia zoezi la kuchukua fomu za kugombea nafasi
mbalimbali ikiwemo nafasi ya Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa lililokamilika wiki
iliyopita,Katibu wa chama hicho Mkoa wa Kagera Avelin Moshi alisema hawatasita
kuwaengua wagombea watakaokiuka kanuni.
Alisema ni kinyume cha kanuni mgombea kuandaliwa vikao visivyo
rasmi vya kukutana na wajumbe na kuwa hilo likiruhusiwa linaweza kuwanyima
fursa ya kuchaguliwa wagombea ambao hawana uwezo wa kuwazungukia wajumbe.
“Vijana inabidi wawe na subira tunataka wapatikane viongozi
wapya watakaokisaidia chama sio bora viongozi,mgombea atakayekusanya wajumbe jina
lake litaondolewa hilo halihitaji kikao”alisema Mushi
Pia vuguvugu la uchaguzi ndani ya umoja huo linaonekana
kuwagawa wenyeviti wa UVCCM ngazi za Wilaya ambao baadhi yao walijitokeza
kupiga madai ya kumuunga mkono mgombea mmoja Yahya Kateme ambaye pia ni
Mwenyekiti wa umoja huo wilaya ya Karagwe.
Wiki iliyopita wenyeviti wa wilaya za Muleba(Athumani
Kahara)Ngara(Faris Mohamed) na Missenye(Revocatus Babeiya) walinukuliwa wakitangaza
msimamo wa kumuunga mkono mgombea huyo wakati akirejesha fomu huku wakitaka wagombea
wanaokimbilia mikoani uchaguzi unapofika kukataliwa.
Hata hivyo Mwenyekiti wa Wilaya ya Bukoba Vijijini Prudence
Kibuka na Chifu Kalumuna wa Bukoba Mjini waliueleza mtandao wa www.bukobapamoja.blogspot kuwa kauli za
wenzao zilijaa ubaguzi na wao kutangaza kumuunga mkono Wilbrod Mutabuzi ambaye
pia anawania nafasi hiyo.
Kwa mujibu wa Mutabuzi alisema huu sio wakati wa majigambo
na kutafuta kuchafuana na kuwa hizo ni dalili za woga wa mpinzani wake na
kutaka isubiliwe siku ya uamuzi wa wanachama wa umoja huo wakati wa uchaguzi.
Alisema uongozi wa chama unaanzia kwenye
Jumuiya hiyo na kuwa hajakurupuka kuwania nafasi hiyo kwani ana uzoefu katika nyanja
mbalimbali za uongozi na uwezo mkubwa wa
ubunifu wa miradi ianyoweza kuisaidia Jumuiya kujiendesha kwa mafanikio.
Mwenyekiti anayemaliza muda wake Deusdedith Katwale hatetei
tena nafasi yake ya Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa kwa kile alichodai kuwa ni
kukabiliwa na majukumu mengine.Hata hivyo Wilaya anayotoka ya Chato ilimegwa
kutoka Mkoa wa Kagera na kuwa sehemu ya Mkoa mpya wa Geita.