Mwanafunzi Leah Sebastian anayesoma darasa la tano shule ya Msingi Katoju iliyopo Kijiji cha Buhanga Kata ya Bujugo Wilaya ya Bukoba Vijijini akitoka katika shughuli za shamba. |
Hawa ni wanafunzi wa shule ya Msingi Kajure iliyopo katika Kisiwa cha Bumbire Wilayani Muleba |
Phinias Bashaya,Chato
Halmashauri ya wilaya ya Chato Mkoani Kagera
inakusudia kubinafsisha mpango wa ujenzi wa nyumba za walimu baada ya
majadiliano yanayoendelea baina yake na serikali za vijiji ili kupata ardhi kwa
ajili ya mpango huo.
Hatua hiyo inalenga kukabiliana na tatizo
la uhaba mkubwa wa nyumba za walimu ambalo wadau wanalinaelezea kuwa
miongoni mwa sababu za kudorora kwa maendeleo ya elimu wilayani humo.
Katika ripoti ya utafiti wa Mradi wa Uwezo
Tanzania 2011, wilaya ya Chato ilishika nafasi ya 66 miongoni mwa wilaya 132
zilizofanyiwa utafiti nchini katika stadi za kusoma Kiswahili, Kiingereza na
kufanya Hisabati za kiwango cha darasa la pili.
Kwa mujibu wa viongozi wa
halmashauri, wilaya ya chato ilikuwa na upungufu wa nyumba 1615 za walimu
ambao ni sawa na aslimia 87.5 ya mahitaji ya nyumba 1845 kwa ajili
ya kuwawezesha walimu kuishi kwenye mazingira ya shule zao.
Ofisa elimu wa Wilaya ya Chato Ishengoma Kyaruzi
alisema uhaba wa nyumba za walimu ni miongoni mwa maeneo ya vipaumbele vya
halmashauri hiyo ambayo yanakwazwa na ukosefu wa raslimali ikiwamo fedha na
ardhi.
Alisema kuwa mbali na kutafuta ardhi,
halmashauri ya wilaya hiyo ilikuwa inaandaa utaratibu wa kuwapata wawekezaji
ambao watajenga nyumba na baadaye kuzipangisha kwa walimu kwa malipo nafuu.
Alidokeza mkakati huo wakati akitoa mada kwenye
mdahalo ulionadaliwa na Asasi za Kiraia Mkoani Kagera kwa ubia na The
Foundation for Civil Society kujadili changamoto za elimu.
Naye katibu wa Chama Cha Walimu wilayani Chato Victoria
Laurent alisema kuwa kukosekana kwa nyumba za walimu kwenye maeneo ya shule
kumeathiri viwango vya taaluma kwa kiasi kikubwa.
“ Tunaomba mamlaka kujenga mazingira mazuri ya
kufundishia na kujifunzia ambayo bila kuwapo ndoto zakufikia malengo ya millennia
zitakuwa zimeishia hewani” alisema Kiongozi huyo wa CWT.
Alisema kutokana na walimu kuishi mbali na shule ilikuwa vigumu kuwahi
ratiba za masomo sambamba na kushindwa kuzuia uharibifu wa mali na samani za
shule unaotokea baada ya saa za masomo.
No comments:
Post a Comment