Mtetezi wa Haki za Watu wenye Ulemavu na Rais wa Shirika la Kutetea Haki za Binadamu(POTA)Idrisa Masalu akitoa mada katika semina ya kutetea haki za walemavu wa akili iliyofanyika mjini Bukoba |
Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Kagera Rebeca Gwambasa akifungua semina |
Washiriki wa semina |
Picha ya pamoja na mgeni Rasmi |
Mtaalamu wa kitengo cha watoto wenye ulemavu wa akili kutoka Bunazi Wilayani Missenye Mwl Gervase Anatory akitoa mchango wake wakati wa semina |
Phinias Bashaya,Bukoba
SHERIA ya watu wenye ulemavu imetajwa kuwabagua watu wenye
ulemavu wa akili baada ya haki zao kutofikiwa kwa urahisi tofauti na walemavu
wengine huku sheria ikishindwa kulitaja moja kwa moja kundi hilo.
Hayo yamebainishwa katika semina iliyoandaliwa na Chama kwa
Ajili ya Watu wenye Ulemavu wa Akili(TAMH)na kuwakutanisha wataalamu wa watu
wenye ulemavu wa akili kutoka wilaya mbalimbali za Mkoa wa Kagera.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa chama hicho Anacret Rugaihuruza
watu wenye ulemavu wa akili wana mahitaji makubwa zaidi ya wenzao na sheria
ilitakiwa kufafanua haki zao bila kujumuishwa moja kwa moja katika sheria ya
jumla ya haki za walemavu.
Alisema chama hicho pamoja na jukumu la kuwasemea walemavu
wa akili ni muhimu jamii kutambua kuwa hata walemavu wa kundi hilo wana haki ya
kupata mahitaji mengine kama kuoa na kuwa na familia.
Katika semina hiyo iliyofadhiliwa na Shirika la The
Foundation for Civil Society,Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Kagera Rebeca
Gwambasa alikiri sheria ya walemavu kuwa na mapungufu yanayolitenga kundi la walemavu wa akili.
“Katika haki za walemavu kundi la walemavu wa akili
halifikiwi na haki hizo inaonekana wakati sheria inatungwa makundi yote
hayakushirikishwa hata hivyo Serikali iko tayari kupokea ushauri”alisema
Gwambasa
Miongoni mwa washiriki wa semina hiyo Gervase Anatory ambaye
ni mtaalamu wa Kitengo cha watoto wenye ulemavu wa akili Bunazi Wilayani
Missenye alisema hata elimu jumuishi inayowachanganya kundi hilo na wasio na
ulemavu bado haiwasaidii kutokana na kuwepo vitendo vya unyanyapaa.
Alisema watoto wenye ulemavu wa akili wanapochanganywa na
wengine tatizo lao linakuwa kubwa zaidi na kuwa jamii inatakiwa kuwa na mapenzi
mema kwa walemavu na kuwasaidia kupata mahitaji mbalimbali.
Naye mshauri wa watu wenye ulemavu ambaye pia ni Rais wa Shirika la Kutetea haki za binadamu(POTA)Idrisa Massalu alisema umefika wakati wa kutengeneza sehemu maalumu 'Camps'kwa ajili ya kundi hilo kwani hukosa mwelekeo wanapomaliza masomo yao.
Pia wanachama na viongozi wa chama hicho wakati wa semina
hiyo watajifunza usimamizi na udhibiti wa fedha na kuandaa mpango mkakati
utakaotekelezeka.
No comments:
Post a Comment