Chelsea wakishangilia ushindi |
Klabu ya soka ya Chelsea ya Uingereza imefuzu kuingia fainali ya klabu bingwa barani Ulaya, licha ya nahodha John Terry kuonyeshwa kadi nyekundu.
Mchezo wa Jumanne ulikwisha kwa sare ya 2-2, lakini Chelsea ikapata ushindi ikiwa na jumla ya magoli 3-2.
Timu ya The Blues (Chelsea) ilikuwa imelemewa baada ya Sergio Busquets na Andres Iniesta kuiwezesha Barca kuongoza katika mechi hiyo.
Lakini Ramires kwa ustadi aliuinua mpira juu na kuandikisha bao safi la Chelsea katika mechi hiyo.
Barca walipata penalty, lakini Lionel Messi, licha ya maarifa yake na sifa nyingi katika ufundi wa penalty, aliishia kugonga mwamba.
Wakati wa muda wa majeruhi wa dakika tatu zilizoongezwa, Fernando Torres alionyesha utulivu wa hali ya juu sio tu kwa kushambulia ngome ya Barca ambayo kwa muda mrefu ilikuwa haiguswi, lakini vile vile kwa kumchenga hata kipa Valdes na kuutia mpira wavuni kwa makini.
Mapema wiki hii, Torres alikuwa amenukuliwa akisema “sio siku zote timu bora hupata ushindi”, matamshi ambayo ni ndoto iliyotimia.
Sasa vijana wa Chelsea wa Roberto di Matteo wanasubiri kufahamu kama watacheza na timu ya kocha wao wa zamani, Jose Mourinho, akiwa mkufunzi wa Real Madrid, au pengine watakutana na Bayern Munich, ambao uwanja wao ndio utakaotumiwa kuandaa fainali ya ligi ya klabu bingwa.
Real Madrid na Bayern zinapambana LEO jioni, 25 Aprili 2012.
Tatizo la Chelsea ni kwamba katika fainali ya Jumamosi tarehe 19 Mei, sasa watazikosa huduma za nahodha John Terry, Ramires, Branislav Ivanovic na Raul Meireles mjini Munich, kutokana na kuadhibiwa kwa kucheza mchezo wa kuumizana katika nusu fainali.
No comments:
Post a Comment