POLISI Mkoani Kagera wamemuua jambazi anayedaiwa kutoka nchi jirani ya Burundi na mwingine kujeruhiwa vibaya baada ya kufanya uporaji katika kijiji cha Murukukumbo Wilayani Ngara.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoani Kagera Henry Salewi usiku wa April 17,watu watatu walivamia kijiji hicho na kufanya uporaji katika duka la Paschal Timotheo(36)na baada ya kufanya uporaji walipiga risasi hewani.
Amesema majambazi hao wakiwa na bunduki aina ya SMG waliamuru wananchi kulala chini na kupora simu tatu aina ya Nokia,kilo 20 za sukari viroba vya pombe aina ya Konyagi na fedha kiasi cha shilingi laki moja na nusu.
"Baada ya kusikia mlio wa risasi askali waliokuwa doria walifuatilia hadi eneo la tukio na kukuta umefanyika uporaji na kuamua kwenda kuweka mtego katika njia inayovuka kwenda Burundi"alibainisha Salewi.
Pia amesema ilipofika majira ya saa sita na nusu usiku majambazi hao walifika katika eno hilo wakiwa wamebeba vitu walivyopora na baada ya kukataa amri ya kujisalimisha yalifyatuliwa risasi nao kujibu na kumuua mmoja huku wengine wakikimbia.
Hata hivyo Kamanda Salewi amesema majambazi wawili waliosalimika walikimbia na kuvuka mpaka na kuwa jambazi mmoja amelazwa katika hospitali moja nchini humo kutokana na majeraha aliyopata.
Amesema jambazi aliyeuwawa katika eneo la tukio baada ya kupekuliwa alikutwa na bomu lenye namba 82-256-94650,simu zilizoporwa na kitambulisho kilichomtaja kwa jina la Kongera Mutabilolele Mkazi wa kijiji Murama Mkoa wa Muyinga nchini Burundi.
Pia Kamanda Salewi amewakumbusha wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo hasa kwa kutoa taarifa za wageni wanaowatilia shaka katika maeneo yao.
No comments:
Post a Comment