Friday, September 28, 2012

'Iddi Amin aliua watoto wangu watano na wake watatu'


Phinias Bashaya
PAMOJA na ushindi wa majeshi ya Tanzania wakati wa vita ya kumng’oa Idd Amin aliyekuwa Dikteta wa Uganda wapo wananchi wenye kumbukumbu mbaya zilizotokana na athari za mapambano.

Kwamba vita haina macho,hukumba kila mtu bila kujali kama yuko mstali wa mbele katika uwanja wa mapambano au amejificha uvunguni kwa hofu ya mirindimo ya risasi na milipuko ya mabomu.

Vita ya Tanzania na Uganda maarufu kama “Vita ya Kagera”iliyotokea  mwaka 1978 hadi 1979 iliacha athari kubwa za kiuchumi na kijamii hususani kwa wakazi wa Mkoa huo  na baadhi ya wananchi hata baada ya miaka 33 ya vita bado wana makovu moyoni.

Ndivyo ilivyotokea kwa Protase Nshombo mkazi wa kijiji cha Buhanga Kata ya Bujugo Wilaya ya Bukoba Vijijini.Alionja udhalimu wa Idd Amin na majeshi yake baada ya watoto wake watano na wake watatu kuchinjwa hadharani.

Anasema wakati wa vita familia yake ilivamiwa akiwa safari katika jiji la Nairobi nchini Kenya na baada ya kupewa taarifa aliruka kwa ndege hadi jijini Kampala.

“Wakati familia inavamiwa nilikuwa Nairobi nilikuta wameuwa watoto wangu watano na wake watatu eti hawataki kumuona Mtanzania yeyote katika nchi yao”anasema Nshombo

Anabainisha kuwa wakati huo alijaliwa watoto saba kutoka kwa wake sita aliokuwa nao ambao wote walishirikiana kuendesha mradi wa kupika pombe ya moshi maarufu nchini humo kwa jina la Waragi.

Baada ya kufika na kushuhudia unyama aliotendewa na majeshi ya Amin naye alikamatwa na kupewa mateso ikiwa ni pamoja na kupakwa kinyesi na kucharazwa viboko.

Watoto wote waliouawa walikuwa wavulana na wanawake watatu walionusurika pamoja na mabinti wawili walikimbia baada ya kushuhudia wenzao wakifanyiwa unyama.

Kwamba aliishi katika mtaa wa Jinja na alinusurika kifo baada ya kutoroshwa na mwanamke aliyemkumbuka kwa jina moja la Rooza aliyemficha katika kijiji cha Bukedi kilichopo mpakani mwa nchi hiyo na Kenya.

Mwanamke huyo alijawa na huruma baada ya kumkumbuka kuwa waliwahi kufanya kazi wote katika ofisi ya Kabaka na alimpeleka katika kijiji chao ili kumnusuru na kifo.

Akumbuka utajiri wake
Mradi wake ulimwezesha kujipatia pato kubwa hata kuwa mtu maarufu katika jiji la Kampala akimiliki magari sita,mashamba na nyumba za kupangisha.

Hakuwa na hofu ya kushindwa kutosheleza mahitaji ya familia yake kwani alimiliki miradi mingi iliyompatia pato kubwa na hata kuwa miongoni mwa wafanyabiashara maarufu.

Hata hivyo wakati wa vita hiyo pamoja na kusambaratishwa kwa familia yake pia hakuna mali aliyookoa zaidi ya mashamba machache aliyokuwa ameyanunua nje ya mji.

“Mali za pembeni ndizo zilizopona watoto waliobaki walikimbilia ujombani nchi humo mimi nikaendelea na maisha nikiwa mafichoni”anabainisha

Anasema wake wake sita walikuwa wa Kabila la Wasoga na anakumbuka vurugu mauaji,uporaji na vitisho vilivyokuwa vikifanywa na wanajeshi wa Amin.

Safari ya Uganda
Mwaka 1962 damu ya ujana ilimsukuma Protase Nshombo kwenda kutafuta maisha katika jiji la Kampala na kufanikiwa kujiunga na vijana wengine katika kazi za kibarua.

Lengo ilikuwa ni kukusanya fedha zitakazomwezesha kurudi kijijini na kuoa hasa baada ya kununua kitanda cha ‘vono’ ambacho kilikuwa ni fasheni ya vijana wa enzi zake.

Anasema akiwa jijini Kampala alishawishiwa na familia moja iliyotaka wakaishi wote na kukuta katika familia hiyo kuna watoto waliokuwa wakisoma shule.

“Waligundua kuwa nilikuwa na akili wakamua kunipeleka chuo cha ufundi Kyambogo na kusomea fani ya ujenzi baada ya miezi sita nilihitimu na kupata kazi”

Anasema uwezo mkubwa aliokuwa nao katika shughuli za ujenzi ulimwezesha kuajiliwa katika maeneo mbalimbali na hata kusafiri kwenda jijini Nairobi kama mwangalizi wa miradi ya ujenzi.

Kazi yake aliifanya kwa uaminifu mkubwa huku akisafiri miji mbalimbali ndani ya nchi.Pato lake liliongezeka na hata kuanzisha miradi mbalimbali ya biashara zikiwemo nyumba za kupangisha.

Hata hivyo baada ya maisha kumnyokea alifutilia mbali wazo lake la  awali la kupata fedha za kuoa na kurudi nyumbani badala yake kuamua kuishi katika jiji la Kampala.

Kurejea nyumbani
Baada ya kuishi mafichoni Protase Nshombo mwaka 1992 aliamua kurejea nyumbani akiongozana na mke na watoto wawili,aliowapata baada ya mauaji ya familia yake.

Hata hivyo haikuwa kazi rahisi kwani anasema njiani alikumbana na matatizo mengi ikiwemo kunyang’anywa mizigo yake yote na hivyo kurejea kijijini bila kitu.

Anasema kijiji kilipatwa na mshituko baada ya kupata taarifa za kurejea kwake kwani hata baba yake aliwahi kwenda kumtafuta nchini Uganda na hakufanikiwa kumpata.

Anasema baba yake aliwahi kupata taarifa kuwa mtoto wake alikuwa anafanya kazi kwa Kabaka,na kuwa hata hivyo baada ya kufunga safari ya kumfuata hakuweza kumkuta.

“Nilirudi nyumbani bila kitu nilikuta wazazi wangu wote wakiwa hai nilifanyiwa sherehe kwa wiki nzima mimi ndiye mtoto wa kwanza katika familia yetu”anabainisha

Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Kijiji hicho Simon Kyakaraba anakumbuka jinsi Protase Nshombo alivyopotea kwa muda mrefu na hata yeye ni shahidi katika migogoro iliyoibuka baada ya kurejea kwake.

Ni wakati huo alipofananishwa na kondoo aliyepotea na kuifanya familia ilipuke kwa furaha kwani hakuna aliyeamini kuwa alikuwa bado hai.

Mateso uzeeni
Baada ya kifo cha baba yake mwaka 1998 ilianza misukosuko katika familia huku akiwatuhumu baadhi ya ndugu zake kuandaa mipango ya kumnyang’anya mashamba.

“Wanaona mimi ni mnyonge sina fedha na sehemu ya kukimbilia walianza kuninyang’anya mashamba hawakutaka nione hata wosia tulioachiwa”anabainisha.

Hivi sasa familia ina maisha ya kubahatisha pamoja na kudai baba yao alikuwa na mashamba mengi na kuwa haridhiki na mgawanyo wa mali ulivyokwenda.

Hakukaa kimya,amejaribu kutetea haki yake katika ngazi ya kijiji na Baraza la ardhi la Kata ya Bujugo na mara zote amegonga mwamba huku walalamikiwa wakiibuka washindi.

Hata shauri la madai namba 14/2006 lililofunguliwa katika Baraza la Ardhi Bujugo bado matokeo ya hukumu yalizidi kuididimiza zaidi familia hiyo.

Wajumbe wanne wa Baraza hilo chini ya Mwenyekiti wao Levelian  Rwabyo waliona ushahidi uliotolewa unatosha Protase Nshombo kustahili kunyang’anywa sehemu ya shamba.

Watoto wao Theofilda na Samwel ambao ni wanafunzi wa shule ya msingi Katoju mara nyingi hukatisha masomo ili kupeleka mawese katika magulio mbalimbali.

Historia ya vita ya Kagera
Nduli Iddi Amin alitwaa madaraka ya nchi yake kwa mabavu mwaka 1971,na mwaka 1978 jeuri  ikamtuma kuyaamuru majeshi yake kuivamia ardhi ya Tanzania upande wa Mkoa wa Kagera.

Wakati huo ulikuwa ni Mkoa wa Ziwa Magharibi ambapo majeshi yake yaliua wananchi na kupora mali huku Amin akijitapa kuwa siku sio nyingi angechakaza hadi jijini Dar es salaam.

Alibomoa daraja la Kyaka Wilayani Missenye na hata kusambaratisha kanisa ambalo kumbukumbu yake ipo hadi leo katika eneo la Kyaka wilayani humo.

Tunayo kazi moja nayo ni kumpiga.Uwezo wa kumpiga tunao,nguvu za kumpiga tunazo na nia ya kumpiga tunayo.Maneno hayo ya aliyekuwa Amiri Jeshi Mkuu Mwalimu Julius Nyerere yaliitikiwa kwa vitendo na wanajeshi wa Tanzania.

Hiki kilikuwa ni kipindi cha miezi kumi na nane cha kuondoa majeshi ya uvamizi na kuzima ndoto ya Iddi Amin ya kujitwalia ardhi akitaka kuhalalisha mauaji ya wananchi.

Majeshi yetu yalipokewa kwa shangwe katika ardhi ya Uganda,mvamizi alifanikiwa kutoroka.Mashujaa wetu walishiriki kufungua ukurasa mpya kwa wananchi wa Uganda baada ya miaka mingi ya mateso ya Nduli Iddi Amin.

Vita ilikuwa imekwisha.Luteni Jenerali Silas Mayunga na mashujaa wenzake walipokewa kwa shangwe pale Bunazi Wilayani Missenye.Sanamu ya Mayunga katika mji wa Bukoba ni kumbukumbu ya shujaa anayestahili kuenziwa na vitabu vya historia ya taifa hili.
Mwisho


Thursday, September 27, 2012

Marufuku ya kuchimba ‘dawa’yashika kasi


Baadhi ya abiria wakinunua bidhaa mbalimbali baada ya kuchimba 'dawa'katika kituo cha Gairo Mkoani Dodoma
 Phinias Bashaya,Morogoro
AGIZO la Waziri wa Uchukuzi Dokta Harrison Mwakyembe la kupiga marufuku abiria wanaosafiri na mabasi  kujisitiri vichakani limenza kushika kasi kwa mabasi yanayotoa huduma ya usafiri maeneo mbalimbali mikoani.

Katika agizo lake alilolitoa miezi michache iliyopita Bungeni,Waziri Mwakyembe alisema utekelezaji  wa marufuku hiyo utaanza Septemba mosi kwa mabasi yote yanayosafirisha abiria kwenda mikoa mbalimbali nchini.

Mwandishi wa habari ambaye amesafiri kwa nyakati  tofauti na mabasi yanayotoa huduma ya usafiri kati ya mikoa ya Kanda ya ziwa na jijini Dar es salaam ameshuhudia jinsi yanavyokwepa kuwasimamaisha abiria vichakani na badala yake kuegesha katika vituo maalumu vya kuchimba dawa.

Aidha katika moja ya basi la kampuni  inayosafirisha abiria kutoka Bukoba kwenda Dar es salaam alisikika mmoja wa wahudumu wa basi hilo akiwatahadharisha abiria wake kuwa hawataweza kusimama vichakani kwani wanaogopa kupigwa faini.

Mhudumu huyo alikuwa akiwahamasisha abiria wake wachimbe’dawa’katika kituo maalumu kilichopo nje kidogo ya mji wa Kahama na kuwa wasingeweza kusimama tena mpaka watakapofika kituo kingine kwa ajili hiyo.

Hata hivyo baadhi ya abiria walilalamikia uongozi wa Kampuni hiyo kuwa na maegesho ya magari yao mjini Morogoro eneo walilodai vyoo vilikuwa vichafu na kutaka kupewa maelezo ya basi hilo kutofikia kituo cha Mabasi cha Msanvu  usiku wakati likisubiri kuendelea na safari alfajili.

Kwa mujibu wa malalamiko ya baadhi ya abiria walidai pamoja na vyoo kuwa vichafu,pia vilikuwa uchochoroni  maeneo yasiyokuwa na mwanga hali iliyokuwa inahatarisha maisha yao hasa akina mama na watoto.

Wakati akitoa agizo hilo Bungeni Waziri Mwakyembe alisema kitendo cha abiria kujisitiri vichakani kinachangia uharibifu wa mazingira na hata kuhatarisha usalama wa maisha ya abiria wanaoweza kukumbana na wanyama wakali.

Pia alisema kuchimba dawa vichakani ni kitendo kilichipitwa na wakati na pia kinawadhalilisha abiria ambao hulazimika kuvua nguo hadharani hali aliyosema Serikali haiwezi kuendelea kuifumbia macho.



Thursday, September 20, 2012

watendaji wa Kata na vijiji Karagwe walalamikiwa

Enzi zile Kanali Mstaafu Fabian Massawe akiwa Mkuu wa Wilaya ya Karagwe,kabla ya kupanda daraja na kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera.Hapa alikuwa akikabidhi trekta lililotolewa na Rais Jakaya Kikwete kwa wananchi wa Wilaya hiyo

Phinias Bashaya,Karagwe
BAADHI ya wananchi wa Wilaya ya Karagwe wamewalalamikia maofisa watendaji wa vijiji na kata kwa kuwatoza zaidi ya shilingi 30,000 kama gharama za kuandikiwa barua za utambulisho kwenda katika ofisi na taasisi mbalimbali.

Adha hiyo imewakumba zaidi wananchi wanaohitaji barua za utambulisho kutoka kwa maofisa hao ili waweze kupewa malipo ya fidia ya kupisha ujenzi wa barabaraya kiwango cha lami kutoka Kyaka hadi Bugene.

Kwa mujibu wa maelezo ya baadhi ya wananchi ambao tayari wametozwa kiasi hicho cha fedha,walisema huojiwa kwanza kama wametoa michango ya ujenzi wa shule za sekondari za Kata na Zahanati kabla ya kunadikiwa barua za utambulisho.

Walisema mwananchi anayeshindwa kuonyesha stakabadhi za michango mbambali hulazimika kutozwa kuanzia shilingi elfu thelathini ili aweze kuandikiwa barua ya kumtambulisha ili apewe malipo yake.

Pia wananchi wanaohitaji barua za utambulisho kwa ajili ya kuwadhamini ndugu zao katika vituo vya polisi,mahakama na wanaotaka kufungua akaunti za akiba katika Benki hutakiwa kuonyesha stakabadhi za michango au kulipa kiasi icho cha fedha vinginevyo hapewi barua ya utambulisho.

“Hii ni aina mpya ya ufisadi nimeandikiwa barua ya utambulisho na Mtendaji wa Kata baada ya kulipa kiasi cha shilingi elfu thelathini nilihitaji kwenda kumdhamini ndugu yangu kituo cha Polisi”alisema mmoja wa wananchi kutoka Kata ya Bugene.

Baadhi ya wananchi waliolalamika walikiri kuwa hawajawahi kutoa michango ya shughuli za maendeleo kwa zaidi ya mwaka huku wakidai kuwa kiasi cha fedha wanayotozwa ni kubwa mno huku wakionyesha wasiwasi wa matumizi ya fedha hizo pamoja na kuwa wanapewa stakabadhi za malipo.

Pamoja na walalamikaji kuomba majina yao yahifadhiwe kwa hofu ya kupata msukosuko baadaye,mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Kishao Justus Daniel alisema utaraibu huo unatumika katika Kata nyingi za Wilaya hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Bosco Ndunguru alisema suala la kutoza wananchi fedha kwa ajili ya kuandikiwa barua halipo na kuwataka walalamikaji wafike ofisini kwake na kumtajia majina ya wahusika ili aweze kuwachukulia hatua.

Alisema yuko tayari kurudishia fedha za wananchi endapo watendaji wanaohusika na tuhuma hizo watajulikana  na kuwa ofisi yake iko tayari kuidhinisha barua hizo bila malipo kwani wanalipwa mshahara kwa ajili ya kuwatumikia wananchi.