HOTUBA FUPI YA KUPOKEA MAANDAMANO YA KULAANI KIFO CHA DAUD
MWANGOSI NA RAIA WENGINE WALIOUWAWA KATIKA MAZINGIRA YENYE UTATA NA POLISI
Ndugu waandishi wa habari wa Mkoa wa Kagera leo tumeungana
na waandishi wengine kote nchini kulaani
tukio la kuuawa kwa aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha
television cha Chanel Ten Daud Mwangosi,pamoja na raia wengine waliopoteza
maisha katika mazingira yenye utata.
Kifo cha marehemu Daud Mwangosi sio tu kuwa kiliishitua
jamii ya waandishi wa habari hapa nchini,bali pia kifo chake kimekuwa sehemu ya
mjadara katika vyombo vya habari vya Kimataifa hasa baada ya mazingira ya kifo
chake kuonyesha alifia mikononi mwa Polisi.
Leo tumefanya maandamano ya amani kuonyesha kutoridhishwa
kwetu na matumizi makubwa ya nguvu za jeshi la Polisi ambao mara nyingi
wamehusishwa na vifo vya raia wasio na hatia yakiwemo mauaji ya Daud Mwangosi
ambaye alikuwa akitekeleza majukumu yake ya kazi.
Matukio ya vifo katika maeneo mbalimbali nchini yameliweka
jeshi la Polisi katika uhusiano wenye shaka kati yao na waandishi wa habari
ambapo wajibu wa msingi wa askali Polsi ni kuwalinda raia na mali zao.
Kwa mujibu wa ushahidi wa picha katika eneo la tukio,mauaji ya
Mwangosi yalikuwa ya kikatiri,unyama na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.Ni
mauaji yaliyolifedhehesha taifa ambalo tangu mwaka 1961 tumejipatia sifa ya
taifa lenye utulivu na linaloheshimu na kulinda haki ya kuishi kwa raia wake.
Hivyo wakati tukiendelea kuomboleza kifo cha mwenzetu pamoja
na raia wengine waliopoteza maisha katika mazingira yenye utata unaohusishwa na
nguvu kubwa za jeshi la Polisi sisi waandishi wa habari wa Mkoa wa Kagera
tunatoa tamko lifuatalo.
Kwamba tunataka
askali wanaohushwa na tukio la kifo cha Daud Mwangosi wasimamishwe kazi
ili kupisha uchunguzi unaoendelea ufanyike kwa uhuru na haki.
Kwamba kwa kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa Michael
Kamuhanda alikuwepo katika tukio hilo na alikataa kutoa msaada wa kuokoa maisha
ya Mwangosi wakati askali wake wakiendelea kumsurubu, tunamtaka awajibike au wajibishwe
na nafasi yake apewe RPC atakayekuwa tayari kutekeleza kwa vitendo ulinzi na
usalama wa raia.
Kwamba kama tutaona mwenendo wa suala hili hauleti tija na
kutoridhishwa na majibu ya tume iliyoundwa tutashirikiana na taasisi nyingine
zinazotetea haki za binadamu ili kutafuta njia bora ya kuishitaki Serikali.
MWISHO tunalitaka Jeshi la Polisi kuweka utaratibu
utakaowawezesha wanahabari kufanya kazi yao bila dharau na kujengewa hofu
inayotokana na vitisho vya Polisi. Tunataka
Serikali iandae utaratibu ambao
wanahabari,wanasiasa na polisi watautumia kufanya kazi hasa katika
kipindi hiki ambapo nchi inakua katika demokrasia ya vyama vingi ili kuepusha
nchi isitumbukie katika mazingira ya hatari zaidi.
No comments:
Post a Comment