Baadhi ya abiria wakinunua bidhaa mbalimbali baada ya kuchimba 'dawa'katika kituo cha Gairo Mkoani Dodoma |
Phinias Bashaya,Morogoro
AGIZO la Waziri wa Uchukuzi Dokta Harrison Mwakyembe la
kupiga marufuku abiria wanaosafiri na mabasi kujisitiri vichakani limenza kushika kasi kwa
mabasi yanayotoa huduma ya usafiri maeneo mbalimbali mikoani.
Katika agizo lake alilolitoa miezi michache iliyopita
Bungeni,Waziri Mwakyembe alisema utekelezaji wa marufuku hiyo utaanza Septemba mosi kwa
mabasi yote yanayosafirisha abiria kwenda mikoa mbalimbali nchini.
Mwandishi wa habari ambaye amesafiri kwa nyakati tofauti na mabasi yanayotoa huduma ya usafiri kati
ya mikoa ya Kanda ya ziwa na jijini Dar es salaam ameshuhudia jinsi
yanavyokwepa kuwasimamaisha abiria vichakani na badala yake kuegesha katika
vituo maalumu vya kuchimba dawa.
Aidha katika moja ya basi la kampuni inayosafirisha abiria kutoka Bukoba kwenda Dar
es salaam alisikika mmoja wa wahudumu wa basi hilo akiwatahadharisha abiria
wake kuwa hawataweza kusimama vichakani kwani wanaogopa kupigwa faini.
Mhudumu huyo alikuwa akiwahamasisha abiria wake wachimbe’dawa’katika
kituo maalumu kilichopo nje kidogo ya mji wa Kahama na kuwa wasingeweza
kusimama tena mpaka watakapofika kituo kingine kwa ajili hiyo.
Hata hivyo baadhi ya abiria walilalamikia uongozi wa Kampuni
hiyo kuwa na maegesho ya magari yao mjini Morogoro eneo walilodai vyoo vilikuwa
vichafu na kutaka kupewa maelezo ya basi hilo kutofikia kituo cha Mabasi cha
Msanvu usiku wakati likisubiri kuendelea
na safari alfajili.
Kwa mujibu wa malalamiko ya baadhi ya abiria walidai pamoja
na vyoo kuwa vichafu,pia vilikuwa uchochoroni maeneo yasiyokuwa na mwanga hali iliyokuwa
inahatarisha maisha yao hasa akina mama na watoto.
Wakati akitoa agizo hilo Bungeni Waziri Mwakyembe alisema
kitendo cha abiria kujisitiri vichakani kinachangia uharibifu wa mazingira na
hata kuhatarisha usalama wa maisha ya abiria wanaoweza kukumbana na wanyama
wakali.
Pia alisema kuchimba dawa vichakani ni kitendo kilichipitwa
na wakati na pia kinawadhalilisha abiria ambao hulazimika kuvua nguo hadharani
hali aliyosema Serikali haiwezi kuendelea kuifumbia macho.
No comments:
Post a Comment