Baadhi ya wananchi wa Katoke wakielekea katika shule iliyokabidhiwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Kagera |
MKUU wa Mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian Massawe
ameingilia kati mgogoro wa shule iliyodaiwa kumilikiwa na Mbunge wa zamani wa
Jimbo la Muleba Kaskazini Ruth Msafiri na kuamua kuikabidhi kwa wananchi.
Mgogoro wa shule ya sekondari ya wasichana ya Ruth Msafiri
umedumu kwa zaidi ya miaka miwili na ulioibuka baada ya Ruth kubwagwa katika
kura za maoni (CCM)na hivyo kushindwa kutetea nafasi yake na baadaye kudai
shule hiyo ni mali yake binafsi.
Shule hiyo imejengwa katika Kitongoji cha Kimbugu,Kata ya
Katoke na inadaiwa ilianzishwa na mbunge huyo wakati wa kipindi chake cha
uwakilishi baada ya kupewa ardhi na Serikali ya Kijiji kwa makubaliano kuwa iwe
ya wananchi wa Kata hiyo.
Pia mgogoro wa sekondari hiyo mapema mwaka huu uliibukia
katika Baraza la Madiwani wa Wilaya ya Muleba baada ya tume iliyoundwa kubaini
kuwa Ruth alipewa ekali arobaini na
serikali ya kijiji na kuanza kutafuta michango ya ujenzi kwa niaba ya wananchi.
Kwa mujibu wa tume iliyoundwa na Baraza la Madiwani miongoni
mwa waliochangia ni Rais wa Jakaya Kikwete aliyetoa mabati mia tatu,mfuko wa
maendeleo ya jimbo 3,000,000,benk ya NMB 5,000,000 NA Wizara ya Malisili na
Utalii 6,000,000.
Kabla ya Kanali Massawe kukabidhi shule hiyo kwa wananchi
juzi,Februari 20,2012 alitembelea kijiji cha Katoke na kufanya mkutano wa
hadhara na wananchi na kupewa maelezo ya mgogoro huo.
Baadaye aliwaagiza wananchi kupitia ngazi mbalimbali za
kisheria kuanzia kijiji,Baraza la Kata na Baraza la Madiwani wa halmashauri ya
Wilaya ya Muleba ili kuridhia kama shule hiyo inastahili kuwa mali ya wananchi.
Kwa mujibu wa Kanali Massawe ameridhika na hatua
zilizofikiwa na juzi aliamua kukabidhi shule hiyo kwa wananchi na kuwataka
waendeleze ujenzi kwa ajili ya kupokea wanafunzi watakaochaguliwa kujiunga na
kidato cha kwanza mwakani.
Baada ya kukabidhi shule hiyo alifanya uhamasishaji na
kupatikana zaidi ya shilingi milioni mbili,huku wananchi wakihaidi kutoa mchango
wa mawe,mchanga saruji na mbao na
kumhaidi kuwa msingi wa vyumba vitatu utakuwa umekamilika kufikia mwezi Januari.
Pamoja na kuhudhuriwa na kundi kubwa la
wananchi,makabidhiano ya shule hiyo pia yalishuhudiwa na Mkuu wa Wilaya ya
Muleba Limbres Kipuyo na viongozi
wengine wa Serikali.
Hata hivyo Ruth Msafiri hakuweza kupatikana kutoa maoni yake
kufuatia hatua iliyochukuliwa na Serikali ya kukabidhi shule hiyo kwa wananchi
ambayo awali alidai ni mali yake binafsi.
No comments:
Post a Comment