Mzee Theobard Kishenye akiondoka katika hali ya kukata tamaa katika ofisi za Wilaya ya Karagwe baada ya jina lake kukosekana kwa wanaotakiwa kupewa fidia |
Mbunge wa viti maalumu CCM Bernadetha Mushashu akisikiliza malalamiko ya baadhi ya wananchi wa wilaya ya Karagwe ambao hawatapata fidia kupisha ujenzi wa barabara ya Kyaka-Bugene |
BAADHI ya wakazi wa Wilaya ya Karagwe wamemuomba Waziri wa
Ujenzi Pombe Magufuli kumulika zoezi la ulipaji wa fidia ya kupisha ujenzi wa
barabara ya Kyaka Bugene kwa madai kuwa uthamini wa mali ulifanyika kwa upendeleo.
Wananchi wa vijiji vya Kihanga na Kishao wametoa kilio hicho
baada ya kubainika kuwa katika orodha ya watakaolipwa fidia zipo nyumba zilizojengwa miaka ya karibuni
huku zenye miaka zaidi ya hamsini zikiondolewa katika orodha ya kufidiwa.
Mkazi wa kijiji cha
Kishao Magreth Peter ambaye ni mama mjane alisema amejulishwa na Tanroads Mkoa
wa Kagera kuwa nyumba yake itabomolewa bila fidia,wakati huo jirani zake ambao
wako ndani ya mita 22.5 kama yeye wakiwa wameanza kulipwa.
Mwananchi mwingine wa kijiji hicho Adventina Furuka ambaye
pia ni mjane alishangazwa na baadhi ya nyumba za kifahari zilizojengwa miaka ya
karibuni katika ukanda ule ule kuonekana
katika orodha ya watakaolipwa huku wao majina yakikosekana.
“Nimeolewa hapa tangu mwaka 1950 naishi na watoto na wajukuu
,nimeambiwa nyumba yangu itabomolewa bila kulipwa fidia wazee wote wamezikwa
hapa nyumbani na kuna makaburi saba”anabainisha mama huyo.
Pia waliwatuhumu walioendesha zoezi la utahamini baada ya
kudaiwa kuwataka wale wenye nyumba zenye umri mkubwa kupeleka uthibitisho wa
stakabadhi za kununua mabati ya kuezekea
ili waingizwe kwenye orodha ya watakaofidiwa.
Aidha mzee Theobard Kishenye alidai zoezi la uthamini
lilijaa mazingira yenye utata kwani baadhi ya wananchi waliitwa kwa ajili ya
majadiliano na walioendesha zoezi hilo.Alisema majirani zake walioko kwenye
mita zile zile wameanza kupokea malipo na kuwa amejulishwa kuwa hatalipwa
fidia.
Naye Mchungaji Japhet Runyoro alisema kuna utata mkubwa
katika majina yaliyopitishwa kwa ajili ya fidia ikiwemo nyumba mpya za hivi
karibuni na kutaka Waziri Magufuli kuingilia kati suala la malipo ya wananchi
wanaotakiwa kupisha ujenzi wa barabara.
Naye ofisa wa Tanroads Mkoa wa Kagera Gasper Kyaruzi
aliyekuwa akitoa malipo ya fidia juzi kwa baadhi ya wananchi alikataa kutoa ufafanuzi kwa kundi kubwa la
wananchi waliokuwa wakidai hawana imani na zoezi la uthamni lilivyoendeshwa.
Alisema kazi aliyokuwa ametumwa ni kulipa fedha kwa wananchi wanaostahili fidia ambao pia majina
yao yalikuwa yametundikwa katika mbao za matangazo katika Halmashauri ya Wilaya
hiyo na kuwa mwenye malalamiko ayapeleke ofisi za Tanroad Mkoa.
No comments:
Post a Comment