1: 2012/13 Loans Allocations List 1-A (AK -DU)
Wednesday, September 19, 2012
Visit Bukoba pamoja blog for Loan Allocations 2012/2013
1: 2012/13 Loans Allocations List 1-A (AK -DU)
RC Kagera amnyang'anya mbunge shule na kuikabidhi kwa wananchi
![]() |
| Baadhi ya wananchi wa Katoke wakielekea katika shule iliyokabidhiwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Kagera |
MKUU wa Mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian Massawe
ameingilia kati mgogoro wa shule iliyodaiwa kumilikiwa na Mbunge wa zamani wa
Jimbo la Muleba Kaskazini Ruth Msafiri na kuamua kuikabidhi kwa wananchi.
Mgogoro wa shule ya sekondari ya wasichana ya Ruth Msafiri
umedumu kwa zaidi ya miaka miwili na ulioibuka baada ya Ruth kubwagwa katika
kura za maoni (CCM)na hivyo kushindwa kutetea nafasi yake na baadaye kudai
shule hiyo ni mali yake binafsi.
Shule hiyo imejengwa katika Kitongoji cha Kimbugu,Kata ya
Katoke na inadaiwa ilianzishwa na mbunge huyo wakati wa kipindi chake cha
uwakilishi baada ya kupewa ardhi na Serikali ya Kijiji kwa makubaliano kuwa iwe
ya wananchi wa Kata hiyo.
Pia mgogoro wa sekondari hiyo mapema mwaka huu uliibukia
katika Baraza la Madiwani wa Wilaya ya Muleba baada ya tume iliyoundwa kubaini
kuwa Ruth alipewa ekali arobaini na
serikali ya kijiji na kuanza kutafuta michango ya ujenzi kwa niaba ya wananchi.
Kwa mujibu wa tume iliyoundwa na Baraza la Madiwani miongoni
mwa waliochangia ni Rais wa Jakaya Kikwete aliyetoa mabati mia tatu,mfuko wa
maendeleo ya jimbo 3,000,000,benk ya NMB 5,000,000 NA Wizara ya Malisili na
Utalii 6,000,000.
Kabla ya Kanali Massawe kukabidhi shule hiyo kwa wananchi
juzi,Februari 20,2012 alitembelea kijiji cha Katoke na kufanya mkutano wa
hadhara na wananchi na kupewa maelezo ya mgogoro huo.
Baadaye aliwaagiza wananchi kupitia ngazi mbalimbali za
kisheria kuanzia kijiji,Baraza la Kata na Baraza la Madiwani wa halmashauri ya
Wilaya ya Muleba ili kuridhia kama shule hiyo inastahili kuwa mali ya wananchi.
Kwa mujibu wa Kanali Massawe ameridhika na hatua
zilizofikiwa na juzi aliamua kukabidhi shule hiyo kwa wananchi na kuwataka
waendeleze ujenzi kwa ajili ya kupokea wanafunzi watakaochaguliwa kujiunga na
kidato cha kwanza mwakani.
Baada ya kukabidhi shule hiyo alifanya uhamasishaji na
kupatikana zaidi ya shilingi milioni mbili,huku wananchi wakihaidi kutoa mchango
wa mawe,mchanga saruji na mbao na
kumhaidi kuwa msingi wa vyumba vitatu utakuwa umekamilika kufikia mwezi Januari.
Pamoja na kuhudhuriwa na kundi kubwa la
wananchi,makabidhiano ya shule hiyo pia yalishuhudiwa na Mkuu wa Wilaya ya
Muleba Limbres Kipuyo na viongozi
wengine wa Serikali.
Hata hivyo Ruth Msafiri hakuweza kupatikana kutoa maoni yake
kufuatia hatua iliyochukuliwa na Serikali ya kukabidhi shule hiyo kwa wananchi
ambayo awali alidai ni mali yake binafsi.
Tuesday, September 18, 2012
Dk Magufuli aombwa kumulika malipo ya fidia Kyaka-Bugene
![]() |
| Mzee Theobard Kishenye akiondoka katika hali ya kukata tamaa katika ofisi za Wilaya ya Karagwe baada ya jina lake kukosekana kwa wanaotakiwa kupewa fidia |
![]() |
| Mbunge wa viti maalumu CCM Bernadetha Mushashu akisikiliza malalamiko ya baadhi ya wananchi wa wilaya ya Karagwe ambao hawatapata fidia kupisha ujenzi wa barabara ya Kyaka-Bugene |
BAADHI ya wakazi wa Wilaya ya Karagwe wamemuomba Waziri wa
Ujenzi Pombe Magufuli kumulika zoezi la ulipaji wa fidia ya kupisha ujenzi wa
barabara ya Kyaka Bugene kwa madai kuwa uthamini wa mali ulifanyika kwa upendeleo.
Wananchi wa vijiji vya Kihanga na Kishao wametoa kilio hicho
baada ya kubainika kuwa katika orodha ya watakaolipwa fidia zipo nyumba zilizojengwa miaka ya karibuni
huku zenye miaka zaidi ya hamsini zikiondolewa katika orodha ya kufidiwa.
Mkazi wa kijiji cha
Kishao Magreth Peter ambaye ni mama mjane alisema amejulishwa na Tanroads Mkoa
wa Kagera kuwa nyumba yake itabomolewa bila fidia,wakati huo jirani zake ambao
wako ndani ya mita 22.5 kama yeye wakiwa wameanza kulipwa.
Mwananchi mwingine wa kijiji hicho Adventina Furuka ambaye
pia ni mjane alishangazwa na baadhi ya nyumba za kifahari zilizojengwa miaka ya
karibuni katika ukanda ule ule kuonekana
katika orodha ya watakaolipwa huku wao majina yakikosekana.
“Nimeolewa hapa tangu mwaka 1950 naishi na watoto na wajukuu
,nimeambiwa nyumba yangu itabomolewa bila kulipwa fidia wazee wote wamezikwa
hapa nyumbani na kuna makaburi saba”anabainisha mama huyo.
Pia waliwatuhumu walioendesha zoezi la utahamini baada ya
kudaiwa kuwataka wale wenye nyumba zenye umri mkubwa kupeleka uthibitisho wa
stakabadhi za kununua mabati ya kuezekea
ili waingizwe kwenye orodha ya watakaofidiwa.
Aidha mzee Theobard Kishenye alidai zoezi la uthamini
lilijaa mazingira yenye utata kwani baadhi ya wananchi waliitwa kwa ajili ya
majadiliano na walioendesha zoezi hilo.Alisema majirani zake walioko kwenye
mita zile zile wameanza kupokea malipo na kuwa amejulishwa kuwa hatalipwa
fidia.
Naye Mchungaji Japhet Runyoro alisema kuna utata mkubwa
katika majina yaliyopitishwa kwa ajili ya fidia ikiwemo nyumba mpya za hivi
karibuni na kutaka Waziri Magufuli kuingilia kati suala la malipo ya wananchi
wanaotakiwa kupisha ujenzi wa barabara.
Naye ofisa wa Tanroads Mkoa wa Kagera Gasper Kyaruzi
aliyekuwa akitoa malipo ya fidia juzi kwa baadhi ya wananchi alikataa kutoa ufafanuzi kwa kundi kubwa la
wananchi waliokuwa wakidai hawana imani na zoezi la uthamni lilivyoendeshwa.
Alisema kazi aliyokuwa ametumwa ni kulipa fedha kwa wananchi wanaostahili fidia ambao pia majina
yao yalikuwa yametundikwa katika mbao za matangazo katika Halmashauri ya Wilaya
hiyo na kuwa mwenye malalamiko ayapeleke ofisi za Tanroad Mkoa.
Friday, September 14, 2012
Mwandishi RFA atimuliwa kwa usaliti
MUSOMA
CHAMA cha Waandishi wa Habari mkoani Mara MRPC, kimemfukuza uanachama wa chama hicho, mwandishi wa habari wa radio Free Afrika mkoani Mara Bw Maxmilian Ngesi baada ya kukiuka makubalino ya chama hicho yaliyofikiwa juzi ya kutoandika kabisa habari za jeshi la polisi mkoani humo.
Akizungumzia kufukuzwa kwa Mwandishi huyo mwenyekiti wa chama hicho Bw Emmanuel Bwimbo,alisema kuwa Ngesi amekiuka makubaliano ya waandishi wenzake na chama kwa ujumla baada ya kusikika akitangaza habari za jeshi la polisi kwa kumkariri kamanda wa polisi wa mkoa wa Mara.
“ Sisi kwa kauli moja tumekubaliana kutofanya kazi na Jeshi la Polisi Mkoani Mara baada ya Matukio kadhaa likiwemo ya kuuawa kwa mwandishi wa habari mkoani Iringa na kutunyima kibali cha Maandamano yetu ya Amani kupinga Mauaji hayo” alisema Bw Bwimbo
Bw Bwimbo alisema kuwa kitendo hicho kinaonyesha jinsi gani mwandishi huyo alivyokiuka makubaliano ya pamoja na kuwasaliti wenzake ambao wamekubaliana kwa pamoja kuwa hawataandika habari za jeshi hilo kutokana na kuzuiwa waandishi kutoandamana katika maandamano ambayo yaliitishwa nchini kote kulaani kitendo cha mauaji ya mwandishi wa kituo cha chanel Ten mkoani Iringa Daud Mwangosi.
Alisema Ngesi kama mwanachama alitakiwa kutii maamuzi ya chama na tamko la chama chake kwa vile tamko hilo limewataka wananchama wote na siyo kwa mkoa wa Mara tu lakini pia baadhi ya mikoa imetoa matamko na misimamo hiyo lakini cha kushangaza yeye amekaidi na kwenda kinyume.
Aidha Mwenyekiti huyo alisema kamwe chama hicho hakiwezi kuvumilia mwandishi atakaye kiuka agizo hilo na hatua ambayo imechukuliwa kwa Ngesi ni mfano kwa waandishi wengine hadi hapo tamko hilo litakapo tenguliwa.
Jumatatu wiki hii waandishi wa habari walifanya maandamano nchi nzima wakilaani mauaji ya mwandishi mwenzao Daudi Mwangosi ambapo kwa mkoa wa Mara maandamano hayo yaliuzuiwa na polisi hali iliyofanya chama cha waandishi wa habari kukataa kuandika habari za jeshi hilo mkoani Mara.
Mwandishi aliyetimuliwa alisikika akiripoti habari za jeshi la Polisi zilizomkariri Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara katika kipindi cha matukio cha Redio Free Afrika.
Tuesday, September 11, 2012
Waandishi Kagera wataka RPC Iringa ang'olewe
HOTUBA FUPI YA KUPOKEA MAANDAMANO YA KULAANI KIFO CHA DAUD
MWANGOSI NA RAIA WENGINE WALIOUWAWA KATIKA MAZINGIRA YENYE UTATA NA POLISI
Ndugu waandishi wa habari wa Mkoa wa Kagera leo tumeungana
na waandishi wengine kote nchini kulaani
tukio la kuuawa kwa aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha
television cha Chanel Ten Daud Mwangosi,pamoja na raia wengine waliopoteza
maisha katika mazingira yenye utata.
Kifo cha marehemu Daud Mwangosi sio tu kuwa kiliishitua
jamii ya waandishi wa habari hapa nchini,bali pia kifo chake kimekuwa sehemu ya
mjadara katika vyombo vya habari vya Kimataifa hasa baada ya mazingira ya kifo
chake kuonyesha alifia mikononi mwa Polisi.
Leo tumefanya maandamano ya amani kuonyesha kutoridhishwa
kwetu na matumizi makubwa ya nguvu za jeshi la Polisi ambao mara nyingi
wamehusishwa na vifo vya raia wasio na hatia yakiwemo mauaji ya Daud Mwangosi
ambaye alikuwa akitekeleza majukumu yake ya kazi.
Matukio ya vifo katika maeneo mbalimbali nchini yameliweka
jeshi la Polisi katika uhusiano wenye shaka kati yao na waandishi wa habari
ambapo wajibu wa msingi wa askali Polsi ni kuwalinda raia na mali zao.
Kwa mujibu wa ushahidi wa picha katika eneo la tukio,mauaji ya
Mwangosi yalikuwa ya kikatiri,unyama na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.Ni
mauaji yaliyolifedhehesha taifa ambalo tangu mwaka 1961 tumejipatia sifa ya
taifa lenye utulivu na linaloheshimu na kulinda haki ya kuishi kwa raia wake.
Hivyo wakati tukiendelea kuomboleza kifo cha mwenzetu pamoja
na raia wengine waliopoteza maisha katika mazingira yenye utata unaohusishwa na
nguvu kubwa za jeshi la Polisi sisi waandishi wa habari wa Mkoa wa Kagera
tunatoa tamko lifuatalo.
Kwamba tunataka
askali wanaohushwa na tukio la kifo cha Daud Mwangosi wasimamishwe kazi
ili kupisha uchunguzi unaoendelea ufanyike kwa uhuru na haki.
Kwamba kwa kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa Michael
Kamuhanda alikuwepo katika tukio hilo na alikataa kutoa msaada wa kuokoa maisha
ya Mwangosi wakati askali wake wakiendelea kumsurubu, tunamtaka awajibike au wajibishwe
na nafasi yake apewe RPC atakayekuwa tayari kutekeleza kwa vitendo ulinzi na
usalama wa raia.
Kwamba kama tutaona mwenendo wa suala hili hauleti tija na
kutoridhishwa na majibu ya tume iliyoundwa tutashirikiana na taasisi nyingine
zinazotetea haki za binadamu ili kutafuta njia bora ya kuishitaki Serikali.
MWISHO tunalitaka Jeshi la Polisi kuweka utaratibu
utakaowawezesha wanahabari kufanya kazi yao bila dharau na kujengewa hofu
inayotokana na vitisho vya Polisi. Tunataka
Serikali iandae utaratibu ambao
wanahabari,wanasiasa na polisi watautumia kufanya kazi hasa katika
kipindi hiki ambapo nchi inakua katika demokrasia ya vyama vingi ili kuepusha
nchi isitumbukie katika mazingira ya hatari zaidi.
Subscribe to:
Posts (Atom)








