Wednesday, June 6, 2012

UMISSETA Kagera wako tayari

Mkuu wa Wilaya ya Muleba Limbres Kipuyo akikagua Timu za Mpira Tayari kwa mashindano ya UMISSETA Mkoa wa Kagera.Picha na Silvester Raphael-PR ofisi ya Mkuu wa Mkoa

RC Kagera atangaza kiama cha wahamiaji haramu

Ng'ombe wa wafugaji wanaohusishwa na uhamiaji haramu wakiwa katika malisho Wilayani Karagwe
Aina ya ng'ombe wanaofugwa Mkoa wa Kagera
MKUU wa Mkoa wa Kagera kanali mstaafu Fabian Massawe amesema wakati wowote itafanyika oparesheni kubwa ya kuwaondoa wahamiaji haramu katika wilaya zote aliosema ni tishio kubwa la usalama wa nchi.

Akizungumza juzi katika kikao cha Kamati ya ushauri ya Mkoa(RCC)kanali Massawe alisema zoezi hilo litavihusisha vikosi mbalimbali vya ulinzi na usalama na kuwaonya wenyeji watakaowahifadhi wahamiaji hao.

Kwa mujibu wa Massawe Mkoa wa Kagera una jumla ya wahamiaji haramu 35,000 aliodai wanafahamika kwa majina wakiwemo wafugaji na kuwa makundi hayo ni tishio kubwa la usalama wa mkoa na taifa.

"kuna wahamiaji haramu elfu thelathini na tano tunaowafahamu kwa majina na sehemu walipojificha,oparesheni kubwa ya kuwaondoa itaanza wakati wowote kwani ni tishio kubwa la usalama"alisema Massawe.

Aidha Massawe alisema kuwa tayari mkoa umeomba kiasi cha shilingi milioni mia sita kwa ajili ya oparesheni hiyo na kuwa kufumbia macho suala la wahamiaji haramu unaweza kuwa mwanzo wa kukaribisha makundi ya waasi kutoka nchi jirani na kujificha katika nchi yetu.

Hata hivyo Mkuu wa Mkoa wa Kagera kanali mstaafu Fabian Massawe alionyesha wasi wasi wa kuwadhibiti wahamiaji hao wasirudi tena baada ya kubainika kuwa baadhi ya wananchi wanahusika na kuwahifadhi wahamiaji hao.

Friday, June 1, 2012

JK ahusishwa kwenye mgogoro wa shule wilayani Muleba

MGOGORO wa mmiliki halali wa shule ya sekondari Katoke wilayani Muleba kati ya Mbunge wa zamani wa Muleba Kaskazini Ruth Msafiri na wananchi umechukua sura mpya baada ya madiwani  kudai kuwa Rais Jakaya Kikwete alitoa mchango wa mabati kuunga mkono juhudi za wananchi.

Kufuatia kuendelea kufukuta kwa mgogoro huo Kamati ya elimu,afya na maji kupitia kwa mwenyekiti wake Geofrey Samson imewasilisha ushahidi wake mbele ya Baraza la Madiwani wa Wilaya hiyo kuthibitisha kuwa sekondari hiyo sio mali binafsi ya Ruth Msafiri.

Katika ushahidi huo kamati hiyo katika baraza la madiwani lililofanyika juzi ilisema kuwa Rais Jkaya Kikwete alitoa mchango wa mabati 350 baada ya kuelezwa kuwa ilikuwa shule ya sekondari ya kata ya Katoke.

Kwa mujibu wa Geofrey Rais Kikwete aliitikia kilio cha wananchi wakati amefika Wilayani humo kuhudhuria sherehe za siku ya Mashujaa zilizofanyika miaka mitatu iliyopita na kuhaidi kutoa mchango wa mabati kusaidia kukamilika kwa ujenzi wa shule hiyo.

Pia ushahidi mwingine uliowasilishwa na kamati hiyo ni jinsi vyanzo mbalimbali vya mapato ikiwemo fedha ya mfuko wa maendeleo ya Jimbo milioni 13,harambee iliyochangiwa na wadau mbalimbali ikiwemo Benki ya NMB tawi la Muleba shilingi milioni tano na Wizara ya Maliasili na Utalii milioni sita.

"Shule ya sekondari ya Kata ya Katoke ijulikanayo kama sekondari ya Ruth Msafiri ilianzishwa kama shule ya sekondari ya kata chini ya ufadhili wa vyanzo mbalimbali ikiwemo fedha ya mfuko wa maendeleo ya jimbo"anasema sehemu ya taarifa ya Kamati hiyo.

Kwa mujibu wa Kamati hiyo Ruth Msafiri alianza kudai shule hiyo ni mali yake binafsi baada ya muda wake wa Ubunge kumalizika na kutochaguliwa tena na kuwa tangu wakati huo ushirikishwaji wa kamati ya ujenzi ulikoma pamoja na kuwa uanzishwaji wa shule hiyo ulipitia vikao mbalimbali katika ngazi ya kijiji na kata.

Katika Baraza hilo msemaji wa kambi ya upinzani Julius Rwakyendera alisema ushahidi uliotolewa unathibitisha kuwa shule ya sekondari ya Katoke ni mali halali ya wananchi na kuwa inasikitisha mtu aliyewahi kupewa dhamana ya uongozi na wananchi kuonyesha kuwa sio mwamnifu.

Pia katika mchango wa ushahidi uliotolewa na Kamati ya elimu.afya na maji Diwani wa Kata ya Muleba Mjini Hassan Milanga(CUF) alishangaa ukimya wa Serikali katika mgogoro huo na kuwa kama suala hilo lingemhusisha yeyote kutoka kambi ya upinzani angekuwa tayari amefikishwa mahakamani.

Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Msaafu Fabian Massawe alifanya ziara katika Kata ya Katoke ambapo Ofisa Mtendaji wa Kata hiyo Faustine Rweyemamu alisema shule hiyo sio mali binafsi ya Ruth Msafiri kwani February,28,2009 serikali ya kijiji cha Katoke iliitisha kikao cha dharula chini ya Ruth na kuamua kutenga ekali 20 kwa ajili ya ujenzi wa sekondari.

Kwa mujibu wa Ofisa huyo  kuanzia wakati huo harakati za michango ya ujenzi zilianza ambapo Ruth Msafiri alikuwa msimamaizi mkuu akisaidiana na kamati ya ujenzi iliyochaguliwa.