Tuesday, May 29, 2012

Vijana wa Bukoba wamvaa Nape

TAMKO LA VIJANA WA BUKOBA MJINI WAISHIO DAR ES SALAAM

Ujio wa Nape: Kagera Tumedharauliwa na Uzalendo Umedhihakiwa

Tumejaribu kutafakari  kwa kina juu ya nini hasa kilimsukuma Nape kufika Kagera na kushiriki mazishi ya muasisi wa TAA, mzalendo na mpigania uhuru aliyetelekezwa na Taifa lake, Dr. Vedasto Kyaruzi  na bado ki-ukweli hatujapata majibu.

Tunapata shida kujua dhima ya safari ya Nape kwa kuwa shughuli hasa alizozifanya akiwa Kagera zina kinzana kimaadili na kitamaduni na maombolezo ya misiba ya Kiafrika na hasa misiba ya Kihaya.

Mjumbe aliyetumwa mahsusi toka mbali kupeleka pole kwenye msiba hategemewi atumie muda wake mwingi majukwaani kufanya siasa, tena katika mazingira ya ugenini. Lakini mpita njia ambaye amefahamishwa tukio na akahiari kufika msibani, akiendelea na shughuli zake si ajabu hata kidogo.

Nape aliingia Bukoba tarehe 25/05/2012. Na ni uungwana kukiri kuwa alifika Kashai-Matopeni msibani kutoa salamu za pole.  Lakini baada ya hapo alielekea Missenyi ambako tunaarifiwa alikuwa na mikutano ya hadhara.

Watanzania mtakumbuka vema kuwa katika mikutano hiyo ndiko Nape alitoa kauli ya kutokuwa tayari kukabidhi nchi kwa wahuni! Labda ili Watanzania muweze kupima vema uelewa na akili za Nape, tuwafahamishe kuwa Missenyi ndiko iliko Kyaka na ambako maziko ya Dr. Kyaruzi yamefanyika.

Tunashindwa kuelewa, hiyo mikutano ilikuwa safisha njia ya mazishi au inahusiana vipi na mtu aliyepeleka ujumbe wa maombolezo?

Linalochanganya zaidi ni hili la Jumamosi tarehe 26/05/2012. Hii ndiyo siku ambayo Dr. Kyaruzi alipumzishwa rasmi kaburini alale kwa amani. Lakini kwa Nape akiwa Kyaka hii ilikuwa siku maalumu ya kutangaza operation yake mpya ya kisiasa “Vua Gamba, vua Gwanda, Vaa Uzalendo”.

Katika hili, ukiachilia ukinzani wa matukio kimaadili na kitamaduni, tunapata mishangao mingine; hivi Nape alikwenda Kyaka kuzika au kuzindua operation ya kisiasa? Na Je, huyu kijana anahubiri uzalendo upi? usiokuwa na utamaduni, Uzalendo wa kuwatelekeza na kushindwa kuwaenzi watu waliopigania uhuru wa nchi hii?

Kama huo ndiyo uzalendo anaohubiri Nape, basi hauhitaji operation wala kampeni maana tayari tunao magwiji. Na hapo kwa tafsiri hii, ujio wake na matukio yake kwenye maeneo ya msiba vinanapata maana halisi.

Katika Taarifa ya Uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki,  Chama Tawala kimearifiwa kuwa moja ya kosa lililofanyika ni kumteua mgombea ambaye mila hazikuwa zinampa fursa na tafsiri njema kufanya shughuli kama ya siasa  katika muda mfupi baada ya msiba wa Baba yake.

Ikiwa kosa hili la Kitamaduni limechangia Chama kupoteza Jimbo, basi pia chama kiwe tayari kwa makosa ya Nape kupoteza zaidi zaidi ya Kijiji cha Burifani na Kata nzima ya kyaka. Na hatutoshangaa iwapo Nape au Taasisi iliyomtuma ikishindwa kuomba radhi!

Mbali na vioja vya Nape hapo juu, kwa wasifu wa marehemu Dr. Kyaruzi, kila mmoja atakubaliana nasi kuwa Taasisi yoyote (iwe dola au chama) kuwakilishwa na mtu wa ngazi ya Nape ni dharau ya hali ya juu na ichukuliwe ni dhihaka si kwa jamii iliyostaharabika tu, bali hata kwa watu walipendao Taifa lao na kuuenzi Uzalendo. Inakuwa vigumu kuamini kuwa pamoja na ugumu wa ratiba, Rais alikosa muwakilishi makini wa hadhi inayobeba uzito sawia na mchango wa Dr. Kyaruzi katika Taifa hili.

Tukio hili linaleta hisia za ubaguzi wa Taasisi za dola na chama katika kutoa uzito kwenye majanga, matatizo na misiba ya watu wa Taifa hili. Ni majuzi tu Taifa lilipotelewa na Mcheza Sinema nguli ambaye hapo awali hakuwahi kupata heshima yoyote ya Kitaifa.

Lakini tuliona jinsi viongozi wa Serikali na Chama walivyohamia msibani na Serikali kujipa jukumu la kuubeba msiba na shughuli za maziko. Haikupita muda, Rais akiwa ziarani Marekani, Rais wa Malawi alifariki duniani. Pamoja na uchovu wa safari tulimwona Rais akiingia nchini na kutoka kuwahi mazishi ya Rais wa nchi jirani.

Kulingana na umuhimu wa msiba huu, Rais hakusubiri hata atatue matatizo makubwa yaliyokuwa yanaikabili serikali yake kiasi cha kutishiwa kuanguka. Lakini pia ni kawaida kusoma taarifa za Rais anazoandika katika mitandao ya kijamii kila anapokuwa njiani kuelekea kwenye misiba ya watu wa kawaida walioko katika maeneo mbalimbali Jijini Dar es Salaam. 

Hili linatuongezea huzuni na kutuongoza kuamini kuwa misiba ya watu wa maeneo nje na Dar es Salaam haigusi hisia za Rais hata kama ni ya Watu waliotoa mchango mkubwa kwa Taifa hili.

Haya yaliyotokea kwa Dr. Kyaruzi alimanusura yatokee pia kwenye msiba wa MKUU wa Majeshi Mstaafu Jenerali  Ernest Mwita Kyaro. Huyu alikufa siku chache baada ya mazishi ya Kanumba na msiba wake ulikosa sura ya Kitaifa. Isingekuwa kelele za wana-Mitandao ya Kijamii (MyKj) na wahandishi wa habari, hata Bunge lisingesimama kwa dakika moja kutoa salamu.

Tabia hii ya kutelekeza wazalendo wa Taifa hili inaonekana kumea kwa kasi. Na uthaminisho wa serikali kwa watu wa Dar es Salaam unaonekana kuwa juu kuliko wa wale walioko nje ya Dar es Salaam.

Kwa Tamko hili tunamtaka Nape Nnauye, Katibu Mwenezi wa CCM kama kweli alikuja kuwakilisha Taasisi yoyote katika msiba wa Dr. Kyaruzi, basi aiombe radhi jamii yetu kwa dharau kubwa aliyoonyesha katika msiba huu. Na kama alikuwa mpita njia tu, basi atujuze ili Jamii na historia ya Taifa imwandike rasmi Dr. Kyaruzi kama muasisi wa TAA na mzalendo aliyepigania uhuru wa Taifa lake ambaye hakuenziwa wakati wa uhai wake na hata mazishi yake hayakuhudhuriwa na mwakilishi wa Kitaifa.

Na mwisho tunamtaka Rais wa Jamhuri ya Tanzania kama Taasisi awe Rais wa Watanzania wote; wa Dar es Salaam na Mikoani.


Asiye na utamaduni ni mtumwa. Tanzania ni moja

Imetolewa na:
Erick Mwemezi Kimasha
Mhamasishaji Jamii Mkuu
Vijana wa Bukoba Mjini Waishio Dar es Salaam

Barua Pepe:       ekimasha@ksgroup.co.tz
Simu:           0713-177-372

Monday, May 28, 2012

Cheo ni Dhamana

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Samwel Kamote(kushoto)na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi Omary Nundu(mwenye miwani kifuani) siku walipotembelea Bandari ya Kemondo,anayetoa maelezo ni Meneja wa bandari hiyo Bwana Minja

Madiwani wa Missenyi watimuliwa kwenye majengo ya Saccos


Aliyewahi kuwa Mbunge wa Nkenge Balozi Dkt Diodorus Kamala akizindua Chama cha Kuweka na Kukopa (Saccos)katika Kata ya Buyango ambapo wakati wa kipindi chake alijenga majengo ya Ofisi hizo kwa kila Kata.Picha hii ilipigwa mwaka jana
CHAMA Cha Mapinduzi(CCM)kimewataka madiwani wa Wilaya ya Missenyi Mkoani Kagera wanaotumia majengo ya vyama vya kuweka na kukopa(Saccos)kama ofisi zao kuondoka katika majengo hayo.

Agizo hilo lilitolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho Nape Nnauye siku ya Ijumaa baada ya kupokea malalamiko ya Umoja wa Vijana wa chama hicho(UVCCM)waliodai baadhi ya madiwani wamegeuza majengo ya Saccos kwa ajili ya matumizi ya ofisi zao.
Nape alikuwa Wilayani humo kufungua Baraza la vijana wa UVCCM ambalo pia lilihudhuriwa na wanachama wa chama hicho na viongozi mbalimbali huku kukiwa na mwitikio mdogo wa vijana.
Nape aliwataka madiwani hao kujenga ofisi zao na kuwa wanatakiwa kuondoka katika majengo hayo na kuwa wasisubiri vijana waendelee kulalamikia suala hilo linaloathiri ukuaji wa vyama hivyo.
"Madiwani jengeni ofisi zenu acheni zifanye kazi ya Saccos,kama madiwani mliweza kushawishi wapiga kura wakawachagua tushawishi pia tukujengee ofisi"alisema Nape
Aidha Nape alisema endapo madiwani hao wataendelea kutumia majengo ya Saccos kama ofisi zao wanaweza pia kuhatarisha ukuaji  na lengo zuri la kuanzisha wa vyama hivyo vya kuweka na kukopa.
Awali Katibu wa UVCCM Wilayani Missenyi Philbert Ngemera katika taarifa yake kwa Nape alisema majengo ya Saccos yalioyengwa kila Kata na aliyekuwa mbunge wa Jimbo hilo Dk Diodorus Kamara yametekwa na baadhi ya madiwani na kuzifanya kuwa ofisi zao.
Pia alihainisha changamoto mbalimbali zinazowakabiri vijana  kuwa ni pamoja na upandaji holela wa bidhaa na vijana kukimbia chama hicho kwa madai ya kutowajali huku wakiendelea kuwa na maisha magumu.
Aidha alisema katika baadhi ya maeneo wamekosa vijana wakujitokeza kugombea uongozi kwa kile alichodai ni wengi wao kukosa sifa na kuwa hadi sasa vijana 178 wamekimbia chama hicho na kuhamia Chadema idadi aliyosema ni ndogo ikilinganishwa na vijana wengi wanaoendelea kuiunga mkono CCM.
Kaatika hotuba yake pia Nape aliwaeleza vijana kuwa wana nafasi ya kuchagua viongozi wanaofaa kukiimarisha chama na kuwa wasikubari kurubuniwa hasa katika kipindi hikia mbacho CCM inaendelea na uchaguzi wa ndani.
Mbali na kusema kuwa mageuzi ni lazima ndani ya chama hicho ili kuendana na wakati pia alisema hata wakuu wa Wilaya walioteuliwa hivi karibuni chama kimewaeleza wasifanye mchezo katika maeneo yao kwani nyumbani kwao ni CCM.
Kwa mujibu wa Nape wakuu hao wa wilaya wanatakiwa kufanya kazi kwa masirahi ya chama na kuongeza kuwa ikitokea chama kingine kinachukua dola nacho kinachagua viongozi wake.

Sunday, May 27, 2012

Kutana na wasanii wanaotikisa Bukoba

Nshomile family akiwajibika na kundi lake mwishoni mwa wiki Wilayani Missenyi

Msanii'BK SUNDAY'anayetikisa na ngoma yake ya Secdo na nyingine nyingi.

Hapa BK Sunday akitoa misaada kwa makundi ya kijamii.Mcheki akiwa katika kituo cha kulea watoto yatima cha Hamugembe mjini Bukoba
Huyu naye mziki wake si polepole

Saturday, May 26, 2012

Nape uso kwa uso na Mgombea uraisi!

Mzee Leopord Rwizandekwe mkazi wa kijiji cha Katendaguro Tarafa ya Kiziba Wilaya ya Missenyi Mkoani Kagera ambaye mwaka 1965 alitaka kumng'oa mwalimu Nyerere kabla ya jina lake kuenguliwa na vikao vya Chama akisalimiana na Katibu wa Itikadi na uenezi wa CCM ngazi ya Taifa Nape Nnauye aliyetembelea wilaya hiyo jana.

Nape Nnauye akivishwa skafu na kijana wa Umoja wa Vijana wa CCM wa Wilaya ya Missenyi baada ya kuwasili katika uwanja wa Mashujaa kufungua Baraza la Vijana

Hotuba inaendelea
Na Mwandishi wetu-Missenyi
KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa CCM Nape Nnauye amesema chama chake kimejaa mamluki ambao ndani ya chama hicho wamebaki kama kiwiliwili huku mioyo na mapenzi yao yakiwa kwa vyama vya upinzani.
Kiongozi huyo wa ngazi ya juu ya chama hicho ametoa kauli hiyo jana wilayani Missenyi Mkoani Kagera wakati akifungua Baraza la Vijana ambalo pia lilihudhuriwa na viongozi wa ngazi ya Mkoa na baadhi ya wananchi.
Katika ufunguzi huo Nape alisisitiza wanataka kukirudisha chama kwa wananchi badala ya kundi la watu wenye fedha na kuwa chama hicho hakiwezi kutetereka hata kikibaki na wanachama wachache.
"Kuna mamluki ambao ndani ya chama wamebaki mwili tu wakifikilia upinzani,lazima tufanye mageuzi ili tuendane na wakati hata nikibaki peke yangu CCM haitakufa"alisema Nape
Katibu huyo wa Uenezi na Itikadi wa CCM alilazimika kutumia muda mwingi kuweka sawa hali ya mambo baada ya muasisi wa Chama hicho Abdul Mwanandege awali katika salamu zake kumuonya Nape kuwa chama kinaweza kumfia mikononi.
Kwa mujibu wa muasisi huyo alisema kuwa amefuata nyayo za baba yake aliyekuwa CCM tangu ujana wake na kumkumbusha kuwa wamemkabidhi chama ila awe makini kisije kikamfia mikononi.
Katika hali iliyoonekana kuwaondolea hofu wazee wa chama hicho Nape alisema anawahakikishia kuwa CCM kiko imara na kuwa hawatakuwa tayari kukabidhi nchi kwa watu aliodai ni makundi ya wanaharakati.
"Dola wanapewa chama cha siasa hatuwapi makundi ya wanaharakati kazi yetu kubwa ni kutekeleza ahadi zetu wapiga kura hawatatuuliza tulijibuje kelele za hao wahuni"alitahadharisha Nape
Aidha Nape alilieleza Baraza hilo na baadhi ya wananchi waliohudhuria kuwa wataendelea kusimamia mageuzi ya kukibadilisha chama ili kiendelee kuwa salama huku akijifananisha na panya aliyedai hakosi mkia.
Katika hotuba yake Nape alionyesha hofu iliyokikumba chama hicho baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) siku za karibuni kuvuna mamia ya wanachama kupitia kampeini yake ya Vua gamba vaa gwanda kuwa pia CCM itazindua kampeini ya Vua gwanda vaa Uzalendo.
Kwa mujibu wa Nape kampeini hiyo itaanza hivi karibuni na kuwa uzalendo ndiyo dawa pekee unaoweza kupandwa ndani ya mwananchi kuliko hayo magwanda yanayovaliwa na kuvulia wakati wa kulala.
Awali Katibu wa UVCCM Wilaya ya Missenyi Philbert Ngemera katika taarifa yake alimwambia Nape kuwa miongoni mwa mambo yayaochangia vijana kukikimbia chama hicho ni ugumu wa maisha kwa madai kuwa chama hakiwajali na hata baadhi ya maeneo kukosa vijana wanaojitokeza kugombea uongozi.
Mbali na Katibu huyo kusema kuwa maeneo mengine hakuna uongozi unaoaminiwa katika kuweka matarajio ya vijana pia alisema kuna malalamiko ya vijana kuwa wanaopata nafasi za uongozi ni wale watoto wa vigogo.
"Vijana hawajitokezi wanasema maisha yamekuwa magumu na chama hakiwajali,kuna kero ya upandishaji holela wa bidhaa tunaomba mbinu"alisema Katibu huyo.
Baraza hilo lilifanyika katika uwanja wa Mashujaa Wilayani Missenyi ambapo miongoni mwa viongozi wa Chama waliohudhuria ni Mjumbe wa Halmashauri kuu ya chama hicho(Nec) Costansia Buhiye ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera.

Thursday, May 24, 2012

Shamrashamra za Ushindi wa Mheshimiwa John Mnyika


John Mnyika(Chadema) akiwa amebebwa na mashabiki wake baada ya kushinda kesi ya kupinga Ubunge wake wa Jimbo la Ubungo

Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema)Taifa Freeman Mbowe akiteta na Wanahabari baada ya hukumu nje ya viwanja vya Mahakama Kuu Dar es salaamu


Baada ya hukumu Polisi jamii nayo ilichukua nafasi yake,hawa wameamua kuvua GAMBA na kuvaa GWANDA


Mlalamikaji wa matokeo ya Ubunge wa Ubungo Hawa Ng'umbi akisalimiana na baadhi ya wapenzi na mashabiki wa chama chake cha(CCM)na kumpa pole ya kushindwa kesi

John Mnyika ashinda kesi ya Ubunge Ubungo

Mbunge wa Jimbo la Ubungo (Chadema), John Mnyika.
Hawa Nghumbi (CCM)
Mbunge wa Jimbo la Ubungo (Chadema), John Mnyika ameshinda kesi iliyokuwa inamkabili ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa  mwaka 2010, baada ya Mahakama kutupilia mbali mashitaka yote matano yaliyokuwa yakimkabili ambayo ni :
1)Kwamba Mnyika alimtuhumu mlalamikaji kuuza nyumba za UWT
2)Kutumia Laptop za Mnyika Kuhesabu kura
3)Kuingia watu wengi wa CHADEMA katika chumba cha kuhesabia kura
4)Kuwepo kwa kura hewa 16,000
5)Kukosewa kwa karatasi za kujumulisha kura (form)

Mlalamikaji Hawa Nghumbi (CCM) anatakiwa kulipa gharama zote za kesi hiyo kama ilivyoamriwa na Mahakama.

Domestic Tourism in Serengeti Nation Park

ALL PHOTOS BY PHILBERT THEOPHIL FROM GEITA
Serengeti National Park (1°30'-3°20'S, 34°00'-35°15'E) is a World Heritage Site located in Tanzania. Twice a year ungulate herds of unrivaled size pour across the immense savanna plains of Serengeti on their annual migrations between grazing grounds. The river of wildebeests, zebras and gazelles, closely followed by predators are a sight from another age: one of the most impressive in the world.

Geographical Location

Between the Great Rift Valley and Lake Victoria in northern Tanzania, 200 kilometers (km) northwest of Arusha. It is contiguous in the north with the Maasai-Mara National Reserve in Kenya which it parallels along the border; on the northeast with the Loliondo Game Controlled Area; on the south east with Ngorongoro Conservation Area, on the southwest with Maswa Game Reserve and by the Ikorongo-Grumeti Game Controlled Area in the west: 1°30'-3°20'S, 34°00'-35°15'E.

Wednesday, May 23, 2012

Sisi Bakongoman tunapenda sana mambo ya Free Movement in Tanzania

Mmoja wa wananchi aneyusishwa na uraia wa nchi ya Kongo(DRC)akikata mitaa katika mji wa Bukoba.Inawezekana pia akawa ni Mtanzania mwenye asili ya Kongo

Wahariri wa Tanzania Daima Tuko Pamoja

Wahariri wa Gazeti la Tanzania Daima wakiwa katika Ofisi za Kagera Press Club.Kutoka kushoto ni Martin Malera,Edson Kamulara,Amana Nyebo na Sarehe Mohamed wakisaini kitabu cha wageni
Mhariri wa Makala wa Gazeti la Tanzania Daima Amana Nyembo akihakiki picha katika kamera yake
Kila mtu yuko busy

Mwanafunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA)cha mjini Bukoba Bwana Julius Mkandara akikishangaza kikosi kazi cha wahariri wa Gazeti la Tanzania Daima jinsi alivyobuni kifaa kinachomwezesha mlemavu wa aina yake kuendesha gari bila shida.


Tuesday, May 22, 2012

Monday, May 21, 2012

Ujasiliamali Ngara na Bukoba

Akina mama wa kijiji cha Rulenge Wilayani Ngara wakijishughulisha na biashara ndogo ndogo za kuuza maandazi na vitumbua
Uuzaji na ununuzi wa senene nje ya soko kuu la Mji wa Bukoba

Leo ni kumbukumbu ya kuzama kwa Meli ya Mv Bukoba

Meli ya Mv Bukoba ikizama usiku wa kuamkia tarehe 21,May,1996
Mnara wa kumbukumbu ya abiria waliopoteza maisha uliopo eneo la Igoma Jijijini Mwanza
Mmoja wa abiria walionusurika katika ajali hiyo David Mtensa mkazi wa mjini Bukoba
LEO ikiwa ni kumbukumbu ya miaka kumi na sita tangu kuzama kwa meli ya Mv Bukoba,baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Kagera wamehoji utekelezaji wa ahadi ya Rais Kikwete ya ununuzi wa meli mpya.
Meli ya Mv Bukoba ilizama May 21,1996 na kusababisha vifo vya zaidi ya watu mia tisa,ambapo wakati wa kampeini za uchaguzi Mkuu mwaka 2010 Rais Kikwete alihaidi ununuzi wa meli mpya kama mbadala wa meli iliyozama.
Wakihojiwa kwa nyakati tofauti juu ya kumbukumbu ya tukio hilo baadhi ya wananchi wamesema hawajaona juhudi zozote za utekelezaji wa ahadi hiyo na kuwa tangu wakati huo usafiri wa majini umezorota.
Mmoja wa wananchi hao Selestine Mwebesa mkazi wa kijiji cha Ruhunga wilaya ya Bukoba alisema mbali na kupoteza ndugu mmoja katika ajali hiyo,hakuna jitihada zozote zinazoonekana katika utekelezaji wa ahadi ya rais Kikwete.
Alisema utekelezaji wa ahadi hiyo haupashwi kuchelewa kwani kuzama kwa meli ya Mv Bukoba iliongeza pengo la usafiri kati ya wananchi wa Mkoa wa Kagera na Mkoa wa Mwanza.
Pia mwananchi mwingine Pontian Kaiza mkazi wa Kijiji cha Kibeta nje kidogo ya mji wa Bukoba alisema pamoja na ahadi ya meli mpya kuonekana imewekwa kando,pia alidai kuna malalamiko mengi ya wananchi ambao hawakupata kifuta machozi kama kilivyodaiwa kutolewa na serikali.
Alisema mmoja wa jamaa zake aliyemtaja kwa jina la Joseph Peter ambaye alimpoteza mke wake katika ajali hiyo ni miongoni mwa wananchi wengi ambao hawakupata kifuta machozi kilichotolewa huku wengine wakilalamikia kiwango kidogo walichopewa.
Mmoja wa wananchi waliopona katika ajali hiyo David Mtensa mkazi wa mjini Bukoba wakati wa kumbukumbu ya tukio hilo mwaka jana alinukuliwa akiilalamikia Serikali juu ya kiwango kidogo cha fedha zilizotolewa kwa waathirika wa ajali hiyo.
Alidai kiasi cha shilingi laki moja kilichotolewa kwa abiria aliyenusurika na laki tano waliopoteza ndugu hakikulingana na madhara waliyopata kwa kuzingatia kuwa baadhi yao walikuwa wafanyabiashara waliolazimika kuanza upya.
Miongoni mwa ahadi nyingi alizozitoa Rais Jakaya Kikwete wakati akitafuta muhura wa pili wa uongozi ni ununuzi wa meli mpya,ambapo mpaka sasa hakuna jitihada za wazi zinazoonekana juu ya utekelezaji wa ahadi hiyo.

Sunday, May 20, 2012

Kombe la Klabu Bingwa Ulaya latua Darajani

Didier Drogba hizi ndiyo zake!
Pamoja na timu ya Chelsea ya Uingereza kutopewa nafasi kubwa ya kunyakua ubingwa mbele ya Bayern Munich waliokuwa katika uwanja wa nyumbani wa(Allience Arena)bado Chelsea walionyesha ubabe na kunyakua kombe la klabu Bingwa ya Ulaya-(champions league) katika uwanjawa ugeneni.
 
Katika mechi hiyo ambayo bingwa alipatukana kwa njia ya matuta baada ya dk 120 wakiwa sare ya goli 1-1. ilikuwa ni Bayern Munich iliyopata goli la kutangulia katika dakika ya 83 kupitia kwa Thomas Muller, dakika tano baadae Didier Drogber aliwainuwa washabiki wa Chelsea kwa kusawazisha goli kwa kuunganisha klosi safi kwa kichwa.hadi dakika 90 matokeo yalikuwa 1-1

Dakika 30 ziliongezwa, ambapo Bayern Munich walikosa penati katika dakika ya 5 ya kipindi cha kwanza cha dakika za nyongeza baada ya Drogba kumwangusha Frank Ribbery, ambapo mshambuliaji wa Bayern Roben alikosa penati hiyo baada ya kipa kuidaka.
Hadi dakika 120 zinamalizika magoli yakabaki 1-1. ndipo penati zikapigwa ambapo Chelsea walipata penati 4 na Bayern penati 3.


Friday, May 18, 2012

Wakuu wapya wa Wilaya za Mkoa wa Kagera waapishwa

Mkuu Mpya wa Wilaya ya Karagwe Darry Rwegasira akila kiapo cha kutumikia nafasi hiyo leo Mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera
Mkuu wa Wilaya mpya ya Kyerwa Luteni Kanali Mstaafu Benedict Kulikila Kitenga akila kiapo cha kuwa kushika majukumu ya kuongoza wilaya hiyo leo asubuhi 
Mkuu wa Wilaya ya Missenyi Kanali Mstaafu Issa Suleiman Njiku akila kiapo cha kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo.Katika uteuzi uliofanyika hivi karibuni Njiku hakukumbwa na mabadiliko na kuendelea kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo

Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Kagera walioapishwa leo na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian Massawe.Kutoka Kushoto waliokaa  Zipola Pangani(Bukoba)Luteni Kanali Mstaafu Benedict Kitenga(Kyerwa)Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian Massawe,Costantine Kanyasu(Ngara),Kanali Mstaafu Issa Njiku(Missenyi),Mkuu wa Mkoa Mstaafu Jenerali Tumainieri Kiwelu.Waliosimama kutoka kushoto Richard Nyamweli Mbeho (Biharamulo)Darry Rwegasira(Karagwe)na Limbres Kipuyo (Muleba).

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Samwei Kamote (kulia)ambaye ameachwa katika uteuzi uliofanyika akipongezwa na Zipora Pangani Mkuu Mpya wa Wilaya hiyo aliyerithi nafasi yake.Katika sherehe hizo Kamote ametajwa kama mfano wa viongozi wenye heshima ya utumishi uliotukuka baada ya kufanya kazi hiyo kwa muda mrefu na mafanikio

Baadhi ya viongozi wa madhehebu mbali mbali ya dini wakifuatilia zoezi la kuwaapisha wakuu wapya wa Wilaya za Mkoa wa Kagera
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM)Wilaya ya Bukoba Magreth Abuhoro akisalimiana na Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Kagera Bwana Fumbuka baada ya kuapishwa kwa wakuu wapya wa Wilaya
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera Costansia Buhiye akisalimiana na viongozi mbalimbali baada ya kuapishwa kwa wakuu wapya wa Wilaya za Mkoa wa Kagera.Kushoto kwake ni Askofu wa Jimbo Kathoriki la Bukoba Baba Askofu Nestory Timanywa
Aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Jenerali Tumainieri Kiweru ambaye wakati wa kutambulishwa aliitwa kwa jina la 'Afande'akifuatilia kwa umakini uapishaji wa Wakuu wapya wa Wilaya za Mkoa wa Kagera
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian Massawe amewataka wakuu wapya wa Wilaya kupambana na umasikini wa kipato katika maeneo yao ili kuinua pato la Mkoa wa Kagera.

Katika hotuba aliyoitoa mara baada ya kuwaapisha wakuu wapya wa wilaya walioteuliwa hivi karibuni,Kanali Masawe amesema ni aibu mkoa wa Kagera kuwa katika nafasi ya 19 kwa kiwango cha umasikini ikilinganishwa na mikoa mingine.

Amewataka kuongeza pato la Mkoa wa Kagera kwa kusimamia shughuli za kilimo chenye tija huku akiwaonya wananchi wanaoendekeza uzurulaji na ulevi badala ya kutumia muda huo katika shughuli za uzalishaji.

Katika sherehe za kuwaapisha wakuu wapya wa wilaya zilizofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa pia Knali Massawe amewataka viongozi na wananchi kutembelea vivutio mbalimbali katika wilaya za Mkoa wa Kagera kama njia ya kuvitangaza.

Akitoa shukrani kwa niaba ya wakuu wapya wa wilaya walioapishwa,Mkuu wa wilaya ya Missenyi Kanali Issa Njiku amesema watazingatia maelekezo waliyopewa na kuhaidi kufanya kazi kwa kushirikiana na viongozi wengine katika maeneo yao ili kufikia lengo la kurudisha heshima ya Mkoa wa Kagera katika shughuli za kiuchumi na kijamii kama ilivyokuwa baada ya Uhuru.