Friday, June 1, 2012

JK ahusishwa kwenye mgogoro wa shule wilayani Muleba

MGOGORO wa mmiliki halali wa shule ya sekondari Katoke wilayani Muleba kati ya Mbunge wa zamani wa Muleba Kaskazini Ruth Msafiri na wananchi umechukua sura mpya baada ya madiwani  kudai kuwa Rais Jakaya Kikwete alitoa mchango wa mabati kuunga mkono juhudi za wananchi.

Kufuatia kuendelea kufukuta kwa mgogoro huo Kamati ya elimu,afya na maji kupitia kwa mwenyekiti wake Geofrey Samson imewasilisha ushahidi wake mbele ya Baraza la Madiwani wa Wilaya hiyo kuthibitisha kuwa sekondari hiyo sio mali binafsi ya Ruth Msafiri.

Katika ushahidi huo kamati hiyo katika baraza la madiwani lililofanyika juzi ilisema kuwa Rais Jkaya Kikwete alitoa mchango wa mabati 350 baada ya kuelezwa kuwa ilikuwa shule ya sekondari ya kata ya Katoke.

Kwa mujibu wa Geofrey Rais Kikwete aliitikia kilio cha wananchi wakati amefika Wilayani humo kuhudhuria sherehe za siku ya Mashujaa zilizofanyika miaka mitatu iliyopita na kuhaidi kutoa mchango wa mabati kusaidia kukamilika kwa ujenzi wa shule hiyo.

Pia ushahidi mwingine uliowasilishwa na kamati hiyo ni jinsi vyanzo mbalimbali vya mapato ikiwemo fedha ya mfuko wa maendeleo ya Jimbo milioni 13,harambee iliyochangiwa na wadau mbalimbali ikiwemo Benki ya NMB tawi la Muleba shilingi milioni tano na Wizara ya Maliasili na Utalii milioni sita.

"Shule ya sekondari ya Kata ya Katoke ijulikanayo kama sekondari ya Ruth Msafiri ilianzishwa kama shule ya sekondari ya kata chini ya ufadhili wa vyanzo mbalimbali ikiwemo fedha ya mfuko wa maendeleo ya jimbo"anasema sehemu ya taarifa ya Kamati hiyo.

Kwa mujibu wa Kamati hiyo Ruth Msafiri alianza kudai shule hiyo ni mali yake binafsi baada ya muda wake wa Ubunge kumalizika na kutochaguliwa tena na kuwa tangu wakati huo ushirikishwaji wa kamati ya ujenzi ulikoma pamoja na kuwa uanzishwaji wa shule hiyo ulipitia vikao mbalimbali katika ngazi ya kijiji na kata.

Katika Baraza hilo msemaji wa kambi ya upinzani Julius Rwakyendera alisema ushahidi uliotolewa unathibitisha kuwa shule ya sekondari ya Katoke ni mali halali ya wananchi na kuwa inasikitisha mtu aliyewahi kupewa dhamana ya uongozi na wananchi kuonyesha kuwa sio mwamnifu.

Pia katika mchango wa ushahidi uliotolewa na Kamati ya elimu.afya na maji Diwani wa Kata ya Muleba Mjini Hassan Milanga(CUF) alishangaa ukimya wa Serikali katika mgogoro huo na kuwa kama suala hilo lingemhusisha yeyote kutoka kambi ya upinzani angekuwa tayari amefikishwa mahakamani.

Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Msaafu Fabian Massawe alifanya ziara katika Kata ya Katoke ambapo Ofisa Mtendaji wa Kata hiyo Faustine Rweyemamu alisema shule hiyo sio mali binafsi ya Ruth Msafiri kwani February,28,2009 serikali ya kijiji cha Katoke iliitisha kikao cha dharula chini ya Ruth na kuamua kutenga ekali 20 kwa ajili ya ujenzi wa sekondari.

Kwa mujibu wa Ofisa huyo  kuanzia wakati huo harakati za michango ya ujenzi zilianza ambapo Ruth Msafiri alikuwa msimamaizi mkuu akisaidiana na kamati ya ujenzi iliyochaguliwa.

No comments:

Post a Comment