Tuesday, September 11, 2012

Waandishi Kagera wataka RPC Iringa ang'olewe

HOTUBA FUPI YA KUPOKEA MAANDAMANO YA KULAANI KIFO CHA DAUD MWANGOSI NA RAIA WENGINE WALIOUWAWA KATIKA MAZINGIRA YENYE  UTATA NA POLISI

Ndugu waandishi wa habari wa Mkoa wa Kagera leo tumeungana na waandishi wengine kote nchini kulaani  tukio la kuuawa kwa aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha television cha Chanel Ten Daud Mwangosi,pamoja na raia wengine waliopoteza maisha katika mazingira yenye utata.

Kifo cha marehemu Daud Mwangosi sio tu kuwa kiliishitua jamii ya waandishi wa habari hapa nchini,bali pia kifo chake kimekuwa sehemu ya mjadara katika vyombo vya habari vya Kimataifa hasa baada ya mazingira ya kifo chake kuonyesha alifia mikononi mwa Polisi.

Leo tumefanya maandamano ya amani kuonyesha kutoridhishwa kwetu na matumizi makubwa ya nguvu za jeshi la Polisi ambao mara nyingi wamehusishwa na vifo vya raia wasio na hatia yakiwemo mauaji ya Daud Mwangosi ambaye alikuwa akitekeleza majukumu yake ya kazi.

Matukio ya vifo katika maeneo mbalimbali nchini yameliweka jeshi la Polisi katika uhusiano wenye shaka kati yao na waandishi wa habari ambapo wajibu wa msingi wa askali Polsi ni kuwalinda raia na mali zao.

Kwa mujibu wa ushahidi wa picha katika eneo la tukio,mauaji ya Mwangosi yalikuwa ya kikatiri,unyama na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.Ni mauaji yaliyolifedhehesha taifa ambalo tangu mwaka 1961 tumejipatia sifa ya taifa lenye utulivu na linaloheshimu na kulinda haki  ya kuishi kwa raia wake.

Hivyo wakati tukiendelea kuomboleza kifo cha mwenzetu pamoja na raia wengine waliopoteza maisha katika mazingira yenye utata unaohusishwa na nguvu kubwa za jeshi la Polisi sisi waandishi wa habari wa Mkoa wa Kagera tunatoa tamko lifuatalo.

Kwamba tunataka  askali wanaohushwa na tukio la kifo cha Daud Mwangosi wasimamishwe kazi ili kupisha uchunguzi unaoendelea ufanyike kwa uhuru na haki.

Kwamba kwa kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa Michael Kamuhanda alikuwepo katika tukio hilo na alikataa kutoa msaada wa kuokoa maisha ya Mwangosi wakati askali wake wakiendelea kumsurubu, tunamtaka awajibike au wajibishwe na nafasi yake apewe RPC atakayekuwa tayari kutekeleza kwa vitendo ulinzi na usalama wa raia.

Kwamba kama tutaona mwenendo wa suala hili hauleti tija na kutoridhishwa na majibu ya tume iliyoundwa tutashirikiana na taasisi nyingine zinazotetea haki za binadamu ili kutafuta njia bora ya kuishitaki Serikali.

MWISHO tunalitaka Jeshi la Polisi kuweka utaratibu utakaowawezesha wanahabari kufanya kazi yao bila dharau na kujengewa hofu inayotokana na  vitisho vya Polisi. Tunataka Serikali iandae utaratibu ambao  wanahabari,wanasiasa na polisi watautumia kufanya kazi hasa katika kipindi hiki ambapo nchi inakua katika demokrasia ya vyama vingi ili kuepusha nchi isitumbukie katika mazingira ya hatari zaidi.


No comments:

Post a Comment