Friday, October 12, 2012

RCC ya Kagera yapiga 'stop'mradi wa bilioni kumi na moja

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian Massawe
Phinias Bashaya,Bukoba
KAMATI ya Ushauri ya Maendeleo ya Mkoa wa Kagera (RCC)imesitisha mkataba wa ujenzi wa  mradi wa jengo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa utakaogharimu zaidi ya shilingi bilioni kumi na moja  na kuagiza yawepo mazungumzo  na Serikali kutafuta njia nzuri ya kutekeleza mradi huo.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya mjadara mkali wa wajumbe ambao baadhi yao ilikiwemo kundi la wabunge wakidai mradi huo ambao hadi unasitishwa ulikuwa umetumia zaidi ya bilioni moja kuwa ulikuwa ni mzigo kwa kuendelea kuzalisha madeni.

Walisema kuwa pamoja na lengo zuri la kuwa na ofisi za Mkuu wa Mkoa katika Kata ya Kahororo mradi huo ulikuwa hautekelezeki kwa sasa na baadhi kushauri watafutwe wawekezaji watakaoweka vitega uchumi katika jengo hilo lenye vymba tisini.

Mbunge wa Bukoba Vijijini Jasson Rweikiza alisema Mkoa hauna uwezo wa kuendeleza mradi huo akidai uamuzi haukuwa sahihi,huku Mbunge wa Nkenge Ansupter Mshama akipendekeza jengo hilo litumike kwa shughuli za utalii.

“Mlianza vyema lakini huu sio wakati unaofaa kuwa na mradi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa yenye vyumba tisini,tulifanye jengo la utalii wananchi hawawezi kuchangia jengo wakati huo ukawataka wachangie zahanati”alisema Mshama

Hata hivyo kundi jingine la wajumbe miongoni mwao akiwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Kashunju Runyogote walitetea ujenzi wa mradi huo ingawa changamoto ilikuwa ni tatizo la upatikanaji wa fedha usiokwenda na mipango ya utekelezaji.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Nassoro Mnambila aliwaeleza wajumbe wa kikao hicho kuwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali iliutaka Mkoa utafakari tena kama kuna umuhimu wa kuendelea na mradi huo ilhali Serikali ikiwa inasuasua kutoa fedha za ujenzi wa ofisi hiyo.

Naye Mwenyekiti wa kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian Massawe alisema wataendelea kufanya mazungumzo na Serikali kushauriana jinsi ya utekelezaji wa Mradi huo na taarifa itawasilishwa katika kikao kijacho.

No comments:

Post a Comment