Friday, October 19, 2012

Waziri ashangaa abiria kulala kwenye sakafu ya kokoto

Naibu Waziri wa Uchukuzi Dk Charles Tizeba akitoa ufafanuzi wa jambo linaloihusu Wizara yake katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera
Dk Tizeba akisalimiana na baadhi ya Maofisa waliofika kumpokea katika uwanja wa ndege Bukoba
Baadhi ya wageni walioambatana na Waziri Tizeba wakiwa katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera
Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Uchukuzi White Majula akitoa ufafanuzi wa malipo ya fidia kwa wananchi wa Bukoba shilingi bilioni 1.9 ili kupisha ujenzi wa jengo la abiria katika uwanja wa ndege wa Bukoba
Phinias Bashaya,Bukoba
NAIBU Waziri wa Uchukuzi Dokta Charles Tizeba ameshangazwa na hali inayowakabili  abiria wa mikoa ya Tabora na Kigoma ambao hulazimika kulala kwenye sakafu ya kokoto wakati wakisubiri usafiri wa treni.

Alionyesha kukerwa na hali hiyo alipokuwa katika ziara yake mjini Bukoba mapema wiki hii wakati akizungumzia uchakavu wa miundombinu ya reli na kulaumu  wahusika kupuuzia suala la ujenzi wa maeneo ya kupumzikia abiria.

“Nilishanga abiria wa Tabora na Kigoma kulala kwenye sakafu ya kokoto wanaposubiri usafiri wa treni,huwezi kuamini kuwa hawa ndio abiria wa Kitanzania wa mwaka 2012”alilalama Tizeba

Alihoji iweje Shirika la  Reli(TRA)lishindwe kuboresha maeneo ya kupumzikia abiria na kuwa kwa kushindwa kufanya hivyo baadhi ya abiria hukwepa kutumia huduma za usafiri zinazotolewa na shirika hilo.

Pia Waziri Dokta Charles Tizeba alisema kuwa wananchi wanalazimika kutumia usafiri wa mabasi kwa sababu  meli na treni havitoe huduma zinazoridhisha, huku akiubeza usafiri wa mabasi na kuufananisha na majeneza yanayotembea.

Aidha alikagua maeneo mbalimbali yaliyopo chini ya Wizara yake ikiwa ni pamoja na uwanja wa ndege wa Bukoba,eneo la Omukajunguti unapotarajiwa kujengwa uwanja wa ndege wa Kimataifa Wilayani Missenye na bandari za Kemondo na Bukoba.

Akizungumzia hali mbaya ya vyombo vya usafiri majini alisema abiria wanakerwa na hali ya uchafu wa meli zinazosafiri ndani ya Ziwa Victoria  na kuwa abiria wanakimbilia usafiri mwingine kukwepa hali inayowafanya waonekane kama walioko mahabusu.

Kuhusu Meli ya Mv Lihemba inayofanya kazi Ziwa Tanganyika alisema itafanyiwa ukarabati mkubwa na Ujerumani.Meli ya Mv Lihemba inatajwa kuwa kongwe zaidi duniani  ikiwa na umri wa miaka mia moja ambayo tangu mwaka 1913 inaendelea kufanya kazi za kusafirisha abiria na mizigo.

No comments:

Post a Comment