Thursday, August 9, 2012

CCM Kagera yawaonya wagombea

Katibu wa CCM Mkoa wa Kagera Avelin Moshi
Mgombea nafasi ya UVCCM ngazi ya Mkoa wa Kagera Yahya Kateme
Katibu wa UVCCM Mkoa wa Kagera Adia Rashid
Mgombea nafasi ya Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Kagera(aliyekaa katikati)Wilbroad Mutabuzi
Wapambe!
Hawa nao walikuwepo kushuhudia urejeshaji wa fomu za mgombea wanayemuunga mkono
Phinias Bashaya,Bukoba
CHAMA Cha Mapinduzi(CCM)Mkoani Kagera kimewaonya wagombea kupitia Jumuiya ya Umoja wa Vijana(UVCCM)dhidi ya uvunjaji wa kanuni za umoja huo kufuatia kuibuka kwa siasa za kupakana matope.

Akizungumzia zoezi la kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali ikiwemo nafasi ya Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa lililokamilika wiki iliyopita,Katibu wa chama hicho Mkoa wa Kagera Avelin Moshi alisema hawatasita kuwaengua wagombea watakaokiuka kanuni.

Alisema ni kinyume cha kanuni mgombea kuandaliwa vikao visivyo rasmi vya kukutana na wajumbe na kuwa hilo likiruhusiwa linaweza kuwanyima fursa ya kuchaguliwa wagombea ambao hawana uwezo wa kuwazungukia wajumbe.

“Vijana inabidi wawe na subira tunataka wapatikane viongozi wapya watakaokisaidia chama sio bora viongozi,mgombea atakayekusanya wajumbe jina lake litaondolewa hilo halihitaji kikao”alisema Mushi

Pia vuguvugu la uchaguzi ndani ya umoja huo linaonekana kuwagawa wenyeviti wa UVCCM ngazi za Wilaya ambao baadhi yao walijitokeza kupiga madai ya kumuunga mkono mgombea mmoja Yahya Kateme ambaye pia ni Mwenyekiti wa umoja huo wilaya ya Karagwe.

Wiki iliyopita wenyeviti wa wilaya za Muleba(Athumani Kahara)Ngara(Faris Mohamed) na Missenye(Revocatus Babeiya) walinukuliwa wakitangaza msimamo wa kumuunga mkono mgombea huyo wakati akirejesha fomu huku wakitaka wagombea wanaokimbilia mikoani uchaguzi unapofika kukataliwa.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Wilaya ya Bukoba Vijijini Prudence Kibuka na Chifu Kalumuna wa Bukoba Mjini waliueleza mtandao wa www.bukobapamoja.blogspot kuwa kauli za wenzao zilijaa ubaguzi na wao kutangaza kumuunga mkono Wilbrod Mutabuzi ambaye pia anawania nafasi hiyo.

Kwa mujibu wa Mutabuzi alisema huu sio wakati wa majigambo na kutafuta kuchafuana na kuwa hizo ni dalili za woga wa mpinzani wake na kutaka isubiliwe siku ya uamuzi wa wanachama wa umoja huo wakati wa uchaguzi.

Alisema uongozi wa chama unaanzia kwenye Jumuiya hiyo na kuwa hajakurupuka kuwania nafasi hiyo kwani ana uzoefu katika nyanja mbalimbali za uongozi  na uwezo mkubwa wa ubunifu wa miradi ianyoweza kuisaidia Jumuiya kujiendesha kwa mafanikio.

Mwenyekiti  anayemaliza muda wake Deusdedith Katwale hatetei tena nafasi yake ya Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa kwa kile alichodai kuwa ni kukabiliwa na majukumu mengine.Hata hivyo Wilaya anayotoka ya Chato ilimegwa kutoka Mkoa wa Kagera na kuwa sehemu ya Mkoa mpya wa Geita.

No comments:

Post a Comment