Monday, August 13, 2012

Chato kubinafsisha ujenzi wa nyumba za walimu

Mwanafunzi Leah Sebastian anayesoma darasa la tano shule ya Msingi Katoju iliyopo Kijiji cha Buhanga Kata ya Bujugo Wilaya ya Bukoba Vijijini akitoka katika shughuli za shamba.
Hawa ni wanafunzi wa shule ya Msingi Kajure iliyopo katika Kisiwa cha Bumbire Wilayani Muleba
Phinias Bashaya,Chato
Halmashauri ya wilaya ya Chato Mkoani Kagera inakusudia kubinafsisha mpango wa ujenzi wa nyumba za walimu baada ya majadiliano yanayoendelea baina yake na serikali za vijiji ili kupata ardhi kwa ajili ya mpango huo.
 Hatua hiyo inalenga kukabiliana na tatizo la uhaba mkubwa wa nyumba za walimu ambalo  wadau wanalinaelezea kuwa miongoni mwa sababu za kudorora kwa maendeleo ya elimu wilayani humo.
Katika ripoti ya utafiti wa Mradi wa  Uwezo Tanzania 2011, wilaya ya Chato ilishika nafasi ya 66 miongoni mwa wilaya 132 zilizofanyiwa utafiti nchini katika stadi za kusoma Kiswahili, Kiingereza na kufanya Hisabati za kiwango cha darasa la pili.
 Kwa mujibu wa viongozi wa  halmashauri, wilaya ya chato ilikuwa na upungufu wa nyumba  1615 za walimu ambao ni sawa na aslimia  87.5 ya mahitaji ya nyumba 1845  kwa ajili ya kuwawezesha walimu kuishi kwenye mazingira ya shule zao.
Ofisa elimu wa Wilaya ya Chato Ishengoma Kyaruzi alisema uhaba wa nyumba za walimu ni miongoni mwa maeneo ya vipaumbele vya halmashauri hiyo ambayo yanakwazwa na ukosefu wa raslimali ikiwamo fedha na ardhi.
Alisema  kuwa mbali na kutafuta ardhi, halmashauri ya wilaya hiyo ilikuwa inaandaa utaratibu wa kuwapata wawekezaji ambao watajenga nyumba na baadaye kuzipangisha kwa walimu kwa malipo nafuu.
Alidokeza mkakati huo wakati akitoa mada kwenye mdahalo ulionadaliwa na Asasi za Kiraia Mkoani Kagera kwa ubia na The Foundation for Civil Society kujadili changamoto za elimu.
Naye katibu wa Chama Cha Walimu wilayani Chato Victoria Laurent alisema kuwa kukosekana kwa nyumba za walimu kwenye maeneo ya shule kumeathiri viwango vya taaluma kwa kiasi kikubwa.
“ Tunaomba mamlaka kujenga mazingira mazuri ya kufundishia na kujifunzia ambayo bila kuwapo ndoto zakufikia malengo ya millennia zitakuwa zimeishia hewani” alisema Kiongozi huyo wa CWT.
 Alisema kutokana na walimu kuishi mbali na shule ilikuwa vigumu kuwahi ratiba za masomo sambamba na kushindwa kuzuia uharibifu wa mali na samani za shule unaotokea  baada ya saa za masomo.

No comments:

Post a Comment