Tuesday, May 29, 2012

Vijana wa Bukoba wamvaa Nape

TAMKO LA VIJANA WA BUKOBA MJINI WAISHIO DAR ES SALAAM

Ujio wa Nape: Kagera Tumedharauliwa na Uzalendo Umedhihakiwa

Tumejaribu kutafakari  kwa kina juu ya nini hasa kilimsukuma Nape kufika Kagera na kushiriki mazishi ya muasisi wa TAA, mzalendo na mpigania uhuru aliyetelekezwa na Taifa lake, Dr. Vedasto Kyaruzi  na bado ki-ukweli hatujapata majibu.

Tunapata shida kujua dhima ya safari ya Nape kwa kuwa shughuli hasa alizozifanya akiwa Kagera zina kinzana kimaadili na kitamaduni na maombolezo ya misiba ya Kiafrika na hasa misiba ya Kihaya.

Mjumbe aliyetumwa mahsusi toka mbali kupeleka pole kwenye msiba hategemewi atumie muda wake mwingi majukwaani kufanya siasa, tena katika mazingira ya ugenini. Lakini mpita njia ambaye amefahamishwa tukio na akahiari kufika msibani, akiendelea na shughuli zake si ajabu hata kidogo.

Nape aliingia Bukoba tarehe 25/05/2012. Na ni uungwana kukiri kuwa alifika Kashai-Matopeni msibani kutoa salamu za pole.  Lakini baada ya hapo alielekea Missenyi ambako tunaarifiwa alikuwa na mikutano ya hadhara.

Watanzania mtakumbuka vema kuwa katika mikutano hiyo ndiko Nape alitoa kauli ya kutokuwa tayari kukabidhi nchi kwa wahuni! Labda ili Watanzania muweze kupima vema uelewa na akili za Nape, tuwafahamishe kuwa Missenyi ndiko iliko Kyaka na ambako maziko ya Dr. Kyaruzi yamefanyika.

Tunashindwa kuelewa, hiyo mikutano ilikuwa safisha njia ya mazishi au inahusiana vipi na mtu aliyepeleka ujumbe wa maombolezo?

Linalochanganya zaidi ni hili la Jumamosi tarehe 26/05/2012. Hii ndiyo siku ambayo Dr. Kyaruzi alipumzishwa rasmi kaburini alale kwa amani. Lakini kwa Nape akiwa Kyaka hii ilikuwa siku maalumu ya kutangaza operation yake mpya ya kisiasa “Vua Gamba, vua Gwanda, Vaa Uzalendo”.

Katika hili, ukiachilia ukinzani wa matukio kimaadili na kitamaduni, tunapata mishangao mingine; hivi Nape alikwenda Kyaka kuzika au kuzindua operation ya kisiasa? Na Je, huyu kijana anahubiri uzalendo upi? usiokuwa na utamaduni, Uzalendo wa kuwatelekeza na kushindwa kuwaenzi watu waliopigania uhuru wa nchi hii?

Kama huo ndiyo uzalendo anaohubiri Nape, basi hauhitaji operation wala kampeni maana tayari tunao magwiji. Na hapo kwa tafsiri hii, ujio wake na matukio yake kwenye maeneo ya msiba vinanapata maana halisi.

Katika Taarifa ya Uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki,  Chama Tawala kimearifiwa kuwa moja ya kosa lililofanyika ni kumteua mgombea ambaye mila hazikuwa zinampa fursa na tafsiri njema kufanya shughuli kama ya siasa  katika muda mfupi baada ya msiba wa Baba yake.

Ikiwa kosa hili la Kitamaduni limechangia Chama kupoteza Jimbo, basi pia chama kiwe tayari kwa makosa ya Nape kupoteza zaidi zaidi ya Kijiji cha Burifani na Kata nzima ya kyaka. Na hatutoshangaa iwapo Nape au Taasisi iliyomtuma ikishindwa kuomba radhi!

Mbali na vioja vya Nape hapo juu, kwa wasifu wa marehemu Dr. Kyaruzi, kila mmoja atakubaliana nasi kuwa Taasisi yoyote (iwe dola au chama) kuwakilishwa na mtu wa ngazi ya Nape ni dharau ya hali ya juu na ichukuliwe ni dhihaka si kwa jamii iliyostaharabika tu, bali hata kwa watu walipendao Taifa lao na kuuenzi Uzalendo. Inakuwa vigumu kuamini kuwa pamoja na ugumu wa ratiba, Rais alikosa muwakilishi makini wa hadhi inayobeba uzito sawia na mchango wa Dr. Kyaruzi katika Taifa hili.

Tukio hili linaleta hisia za ubaguzi wa Taasisi za dola na chama katika kutoa uzito kwenye majanga, matatizo na misiba ya watu wa Taifa hili. Ni majuzi tu Taifa lilipotelewa na Mcheza Sinema nguli ambaye hapo awali hakuwahi kupata heshima yoyote ya Kitaifa.

Lakini tuliona jinsi viongozi wa Serikali na Chama walivyohamia msibani na Serikali kujipa jukumu la kuubeba msiba na shughuli za maziko. Haikupita muda, Rais akiwa ziarani Marekani, Rais wa Malawi alifariki duniani. Pamoja na uchovu wa safari tulimwona Rais akiingia nchini na kutoka kuwahi mazishi ya Rais wa nchi jirani.

Kulingana na umuhimu wa msiba huu, Rais hakusubiri hata atatue matatizo makubwa yaliyokuwa yanaikabili serikali yake kiasi cha kutishiwa kuanguka. Lakini pia ni kawaida kusoma taarifa za Rais anazoandika katika mitandao ya kijamii kila anapokuwa njiani kuelekea kwenye misiba ya watu wa kawaida walioko katika maeneo mbalimbali Jijini Dar es Salaam. 

Hili linatuongezea huzuni na kutuongoza kuamini kuwa misiba ya watu wa maeneo nje na Dar es Salaam haigusi hisia za Rais hata kama ni ya Watu waliotoa mchango mkubwa kwa Taifa hili.

Haya yaliyotokea kwa Dr. Kyaruzi alimanusura yatokee pia kwenye msiba wa MKUU wa Majeshi Mstaafu Jenerali  Ernest Mwita Kyaro. Huyu alikufa siku chache baada ya mazishi ya Kanumba na msiba wake ulikosa sura ya Kitaifa. Isingekuwa kelele za wana-Mitandao ya Kijamii (MyKj) na wahandishi wa habari, hata Bunge lisingesimama kwa dakika moja kutoa salamu.

Tabia hii ya kutelekeza wazalendo wa Taifa hili inaonekana kumea kwa kasi. Na uthaminisho wa serikali kwa watu wa Dar es Salaam unaonekana kuwa juu kuliko wa wale walioko nje ya Dar es Salaam.

Kwa Tamko hili tunamtaka Nape Nnauye, Katibu Mwenezi wa CCM kama kweli alikuja kuwakilisha Taasisi yoyote katika msiba wa Dr. Kyaruzi, basi aiombe radhi jamii yetu kwa dharau kubwa aliyoonyesha katika msiba huu. Na kama alikuwa mpita njia tu, basi atujuze ili Jamii na historia ya Taifa imwandike rasmi Dr. Kyaruzi kama muasisi wa TAA na mzalendo aliyepigania uhuru wa Taifa lake ambaye hakuenziwa wakati wa uhai wake na hata mazishi yake hayakuhudhuriwa na mwakilishi wa Kitaifa.

Na mwisho tunamtaka Rais wa Jamhuri ya Tanzania kama Taasisi awe Rais wa Watanzania wote; wa Dar es Salaam na Mikoani.


Asiye na utamaduni ni mtumwa. Tanzania ni moja

Imetolewa na:
Erick Mwemezi Kimasha
Mhamasishaji Jamii Mkuu
Vijana wa Bukoba Mjini Waishio Dar es Salaam

Barua Pepe:       ekimasha@ksgroup.co.tz
Simu:           0713-177-372

No comments:

Post a Comment