Saturday, May 26, 2012

Nape uso kwa uso na Mgombea uraisi!

Mzee Leopord Rwizandekwe mkazi wa kijiji cha Katendaguro Tarafa ya Kiziba Wilaya ya Missenyi Mkoani Kagera ambaye mwaka 1965 alitaka kumng'oa mwalimu Nyerere kabla ya jina lake kuenguliwa na vikao vya Chama akisalimiana na Katibu wa Itikadi na uenezi wa CCM ngazi ya Taifa Nape Nnauye aliyetembelea wilaya hiyo jana.

Nape Nnauye akivishwa skafu na kijana wa Umoja wa Vijana wa CCM wa Wilaya ya Missenyi baada ya kuwasili katika uwanja wa Mashujaa kufungua Baraza la Vijana

Hotuba inaendelea
Na Mwandishi wetu-Missenyi
KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa CCM Nape Nnauye amesema chama chake kimejaa mamluki ambao ndani ya chama hicho wamebaki kama kiwiliwili huku mioyo na mapenzi yao yakiwa kwa vyama vya upinzani.
Kiongozi huyo wa ngazi ya juu ya chama hicho ametoa kauli hiyo jana wilayani Missenyi Mkoani Kagera wakati akifungua Baraza la Vijana ambalo pia lilihudhuriwa na viongozi wa ngazi ya Mkoa na baadhi ya wananchi.
Katika ufunguzi huo Nape alisisitiza wanataka kukirudisha chama kwa wananchi badala ya kundi la watu wenye fedha na kuwa chama hicho hakiwezi kutetereka hata kikibaki na wanachama wachache.
"Kuna mamluki ambao ndani ya chama wamebaki mwili tu wakifikilia upinzani,lazima tufanye mageuzi ili tuendane na wakati hata nikibaki peke yangu CCM haitakufa"alisema Nape
Katibu huyo wa Uenezi na Itikadi wa CCM alilazimika kutumia muda mwingi kuweka sawa hali ya mambo baada ya muasisi wa Chama hicho Abdul Mwanandege awali katika salamu zake kumuonya Nape kuwa chama kinaweza kumfia mikononi.
Kwa mujibu wa muasisi huyo alisema kuwa amefuata nyayo za baba yake aliyekuwa CCM tangu ujana wake na kumkumbusha kuwa wamemkabidhi chama ila awe makini kisije kikamfia mikononi.
Katika hali iliyoonekana kuwaondolea hofu wazee wa chama hicho Nape alisema anawahakikishia kuwa CCM kiko imara na kuwa hawatakuwa tayari kukabidhi nchi kwa watu aliodai ni makundi ya wanaharakati.
"Dola wanapewa chama cha siasa hatuwapi makundi ya wanaharakati kazi yetu kubwa ni kutekeleza ahadi zetu wapiga kura hawatatuuliza tulijibuje kelele za hao wahuni"alitahadharisha Nape
Aidha Nape alilieleza Baraza hilo na baadhi ya wananchi waliohudhuria kuwa wataendelea kusimamia mageuzi ya kukibadilisha chama ili kiendelee kuwa salama huku akijifananisha na panya aliyedai hakosi mkia.
Katika hotuba yake Nape alionyesha hofu iliyokikumba chama hicho baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) siku za karibuni kuvuna mamia ya wanachama kupitia kampeini yake ya Vua gamba vaa gwanda kuwa pia CCM itazindua kampeini ya Vua gwanda vaa Uzalendo.
Kwa mujibu wa Nape kampeini hiyo itaanza hivi karibuni na kuwa uzalendo ndiyo dawa pekee unaoweza kupandwa ndani ya mwananchi kuliko hayo magwanda yanayovaliwa na kuvulia wakati wa kulala.
Awali Katibu wa UVCCM Wilaya ya Missenyi Philbert Ngemera katika taarifa yake alimwambia Nape kuwa miongoni mwa mambo yayaochangia vijana kukikimbia chama hicho ni ugumu wa maisha kwa madai kuwa chama hakiwajali na hata baadhi ya maeneo kukosa vijana wanaojitokeza kugombea uongozi.
Mbali na Katibu huyo kusema kuwa maeneo mengine hakuna uongozi unaoaminiwa katika kuweka matarajio ya vijana pia alisema kuna malalamiko ya vijana kuwa wanaopata nafasi za uongozi ni wale watoto wa vigogo.
"Vijana hawajitokezi wanasema maisha yamekuwa magumu na chama hakiwajali,kuna kero ya upandishaji holela wa bidhaa tunaomba mbinu"alisema Katibu huyo.
Baraza hilo lilifanyika katika uwanja wa Mashujaa Wilayani Missenyi ambapo miongoni mwa viongozi wa Chama waliohudhuria ni Mjumbe wa Halmashauri kuu ya chama hicho(Nec) Costansia Buhiye ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera.

No comments:

Post a Comment