Saturday, April 21, 2012

Brigedia Adam Mwakanjuki kuzikwa kesho Zanzibar

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
21/04/2012

Aliyekuwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Brigedia Mstaafu Adam Clement Makanjuki anatarajiwa kuzikwa hapo kesho jioni katika makaburi ya Mwanakwerekwe Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Dk.Khalid Muhammed imeeleza kuwa mwili wa Marehemu unatarajiwa kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume majira ya saa tatu na nusu za asubuhi.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa mara baada ya kuwasili Mwili huo utapelekwa katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani Kikwajuni Zanzibar ambapo Viongozi wa Kitaifa,Mabalozi na Wawananchi watapata fursa ya kuuaga mwili wa Marehemu.

Mara baada ya shughuli hiyo kumalizika Mwili utapelekwa katika Kanisa la Anglikana Mkunazini mnamo saa nane za mchana kwa ajili ya Ibada maalum.

Marehemu Brigedia Mstaafu Adam Clement Makanjuki alifariki Dunia hapo Juzi katika Hospitali ya Lugalo jijini Dar es Salaam baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Kabla ya kifo chake Marehemu aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zikiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba na Utawala Bora,Waziri wa Kilimo,Mifugo na Mali Asili,Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi,Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Marehemu amefariki akiwa na umri wa miaka 70 ameacha Kizuka na watoto watano.

IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR

21/04/2012

No comments:

Post a Comment