Friday, April 20, 2012

JAPAN yakabidhi pikipiki nane kukusanya takwimu za kilimo Mkoa wa Kagera

Bukoba
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian Massawe amekabidhi pikipiki nane kwa Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya na Manispaa kwa ajili ya kukusanya takwimu mbalimbali za kilimo kutoka  vijijini katika Mkoa wa Kagera.
Pikipiki hizo zimetolewa na serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika ikishirikiana na shiririka la Kimataifa Uhusiano la nchini Japan (Japan International Cooperation Agency, (JICA)   ambalo limewakilishwa na Bi. Akasaka Kyoko.
Mhe Massawe pia amewasisitiza Wakurugenzi wa Halmashauri na Manispaa kutunza pikipiki hizo na kuzifanyia kazi iliyokusudiwa na si vinginevyo. Aidha aliwaomba maafisa kilimo kutumia vitrndea kazi hivyo kukusanya taarifa sahihi.
Pamoja na pikipiki hizo JICA pia waliendesha mafunzo ya ukusanyaji takwimu na kugawa kompyuta moja na vifaa vingine  kwa kila Halmashauri ya wilaya na manispaa kwa ajili ya kusaidia kukusanya na kutunza takwimu za kilimo vijijini.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian Massawe akihakiki pikipiki zilizotolewa kama ziko imara kwa ajili ya kutumika kufanya kazi ya kukusanya takwimu za kilimo katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kagera.
Mkuu wa Mkoa aliwashukuru JICA kwa kujitolea kuleta maendeleo Tanzania na hasa katika mkoa wa Kagera. Pia amewahakikishia JICA kuwa serikali itaendelea kuhamasisha wananchi kuondokana na kilimo cha kujikimu na kuhamia katika kilimo chenye tija.
Na: Sylvester Raphael

AFISA HABARI- MKOA WA KAGERA
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian Massawe akimshukuru Bi. Akasaka Kyoko Mwakilishi wa Shirika la kimataifa la Japani (JICA) kwa ufadhili wa Pikipiki za kukusanya Takwimu za Kilimo vijijini

Mkuu wa Mkoa wa Kagera  Kanali Mstaafu Fabian Massawe akikabidhi Pikipiki kwa Wawakilishi wa Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya na Manispaa.Picha zote kwa Hisani ya Afisa Habari wa Mkoa wa Kagera.






No comments:

Post a Comment